Jumanne. 30 Aprili. 2024

Tafakari

Jumanne, Mei 23, 2017

Jumanne, Tarehe 23, 2017,
Juma la 6 la Pasaka

Mdo 16: 22-34;
Zab 138: 1-3,7-8 (K. 7);
Yn 16:5-11.


MAISHA NDANI YA ROHO MTAKATIFU

Katika somo la kwanza, tunakutana na Paulo akiwa amejazwa na Roho Mtaktifu akisifu na kumshukuru Mungu kwa kumpa yeye pamoja na ndugu zake kushiriki katika mateso ya Kristo. Hii ni neema kamili ya Roho Mtakatifu ilikuwa ikifanya kazi ndani mwao. Akiwafundisha wafanye mema na kwa wakati muafaka. Hata milango ya gereza ilipo funguka yeye na wenzake hawakukimbia. Ushuhuda huu na wa wenzake ulimfanya yule mlinzi wa gereza kubadili maisha yake yeye na familia yake. Wanaongozwa na Roho Mtakatifu kuokoa maisha ya yule mlinzi wa Gereza, aliyekuwa sababu ya mateso yao pia.

Katika somo la Injili, mioyo ya wafuasi ilijazwa na huzuni, lakini pia walikuwa wakijitahidi kuamini kile ambacho Yesu alikuwa akiwaambia.Yesu aliwaambia kwamba atapaa kwenda kwa Baba yake na kwamba ilikuwa ni vizuri yeye aondoke. Kwasababu akiondoka atamtuma Msaidizi kwao.

Katika hali yya kibinadamu, ilikuwa vigumu kwa wafuasi kumwacha Yesu aondoke tu kwasababu ya wao kumzoea na kuongea naye kila wakati. Ni hakika kwamba walimkosa sana kuendelea kumuona kwa macho yao kama walivyo zoea kumuona, kumshika na kumsikia akiongea. Lakini Yesu aliweka wazi kwamba hata kama anaondoka bado atakuwa nao daima. Na kwamba atamtuma Msaidizi Roho Mtakatifu ambaye atakuwa pamoja nao na kuwaongoza katika ukweli wote, akiwapa nguvu, na kuwafundisha ukweli wote. Watakuwa wawakilishi wake sasa ulimwenguni kwa nguvu ya Roho Mtakatifu.

Hatukuwa na bahati ya kumuona Yesu kama wanafunzi wake walivyokuwa. Lakini tuna bahati ya kuwa nasi kila siku. Na tuna bahati ya kupokea utimilifu wa Roho Mtakatifu. Tumepokea kipaimara, lakini tunaweza kushindwa kumruhusu Roho Mtakatifu akae ndani yetu na kutufanya wapya. Tunapo karibia sikukuu ya Pentekoste, kubali na jinyenyekeshe na kukiri kwamba unamhitaji Roho Mtakatifu aweze kuwa ndani ya maisha yako. Amini kwamba Yesu anataka umpokee yeye katika Utimilifu. Na wala usiwe na wasi wasi kuruhusu muunganiko huu utokee kwako. Tunapaswa kuisikiliza sauti ya Roho Mtakatifu ambaye yupo ndani mwetu na ambaye anajaribu daima kutuelekeza kwenye ukweli.

Sala: Roho Mtakatifu, naomba uje ndani mwangu. Ninaomba unisaidie kuwasha moto wako katika maisha yangu. Ninakuomba nikupokee wewe ambaye uliahidiwa na Yesu katika utimilifu wote. Roho Mtakatifu, Yesu mwana wa Mungu, Mungu Baba mwenye huruma, najiaminisha chini yako. Amina.

Maoni


Ingia utoe maoni