Ijumaa. 01 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatatu, Mei 01, 2017

Jumatatu, Mei 1, 2017.
Juma la 3 la Pasaka

Kumbukumbu ya Mt. Yosefu Mfanyakazi

Mdo 6:8-15;
Zab119:23-24,26-27,29-30, (R. 1);
Yn 6:22-29.

Au masomo ya kumbukumbu
Mwa 1:26-2:3; au Kol 3:14-15, 17, 23-24
Zab 90:2-4, 12-14, 16 (K. 17);
Mt 13:54-58.


MT. YOSEFU MFANO WA WAFANYA KAZI

Injili ya leo inaongelea kuhusu lile kundi la watu wanaomtafuta Yesu, siku baada ya kuongeza ile mikate. Kumtafuta huku haikuwa kwasababu ya upendo kwake, bali kufaidika kutoka kwake. Yesu, anawaambia wazi kwamba wanamtafuta kwasababu walikula mikate, Yesu anawaeleza wawe na lengo lingine la kumtafuta. Sababu iwe ni kwasababu anataka kuwapa chakula cha kiroho.

“Je, unamtafuta Yesu kwasababu njema?” pengine mara nyingi tunamtafuta Yesu kwasababu ya faida fulani, pengine ili kupata gari, nyumba, mchumba, uponyaji wa ugonjwa. Yesu anatuonya tuangalie tusimtafute kwasababu ya vitu vinavyo haribika tu, bali tutafute uzima wa milele.

Kanisa leo lina adhimisha kumbukumbu ya Mt. Yosefu Mfanyakazi. Mungu alimwamini na kumpa jukumu la kumtunza Mama wa Mungu na Mwana wa Mungu, na kuwa mlinzi wa nyumba ya Mungu. Hakuna mtu mwingine yeyote aliyekuwa na nafasi hii pekee. Kupenda kwake kazi ilionesha unyenyekevu wake, aliishi kwa kadiri ya matakwa ya Mungu. Alikuwa mtu mwenye haki. Kilicho mfanya akubalike machoni pa Mungu ilikuwa kwasababu ya Imani yake na utii wake. Kujitoa kwake kulionesha unyenyekevu na kumtegemea Mungu. Na hata baada ya kupata upendeleo kutoka kwa Mungu, hakuacha kufanya kazi.

Katika hali hii tunaweza kusema kwamba yeye ni somo wa wale wote wanaofanya kazi, kazi ambayo ni kuonesha unyenyekevu na tegemeo letu kwa Mungu. Leo tunawakumbuka watu wote duniani wanao fanya kazi kwa manufaa ya uzuri wa wanadamu wote. Tuwaombee kazi zao zisiharibu mpango wa Mungu kwa mwanadamu bali zilinde utu na uhai wa kila mwanadamu kama Mt. Yosefu alivyo linda uhai wa Yesu dhini ya Herode.

Sala: Asante, Mt. Yosefu kwa kumfundisha Yesu kufanya kazi yako. Tunakushukuru kwa kuzipa kazi za mikono thamani na utakatifu. Tunaomba tuweze kuzipa heshima kazi na kuwa tayari kwa ajili ya wengine kama wewe. Mt. Yosefu, mlinzi wa nyumba ya Mungu. Utuombee.
Sala: Bwana, sina pumziko, hadi nitakapo pumzika kwako. Amina.

Maoni


Ingia utoe maoni