Jumanne, Aprili 25, 2017
Jumatatu, Aprili 25, 2016,
Juma la 5 la Pasaka
Sikukuu ya Mt. Marko, Mwinjili
1Pet 5:5-14
Zab 89:2-3,6-7,16-17 (K. 2);
Mk 16:15-20.
KUWA TAYARI KWA NEEMA YA MUNGU.
Leo Kanisa linasherehekea sikukuu ya Mt. Marko, Mwinjili. Yeye aliandika Injili ya pili ambayo kadiri ya utamaduni, inaelezea mahubiri ya Petro. Marko alijihusisha zaidi na kutangaza imani na kuendeleza kanisa la mwanzo. Akiwa ni mzaliwa wa Yerusalemu, alikuwa akitembea na Paulo, Petro na Barnaba katika safari za kitume. Anafahamika kama mwanzilishi wa kanisa la Alexandria huko Misri.
"Enendeni ulimwengu mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe" (Mk.16:15) Mwongozo huu anaotoa Yesu kwa mitume wake ni rahisi na wakueleweka lakini ni wa ajabu mno. Wimbo wa katikati unakazia wito huu ukisema, "nitaziimba rehema zako milele Ee Bwana, kinywa changu kitatangaza wema wako nyakati zote. Je ni nani awezaye kufananishwa nawe Ee bwana uliye mawinguni." Yesu aliwatuma wafuasi wake, watu wa kawaida, akawajaza nguvu ya ajabu ili waihubiri Injili kwa wongofu wa dunia. Hii haikuhusiana na uwezo na utaalam wao wa kuhubiri, bali mwitikio wao kwa neema ya Mungu ifanyayo kazi ndani yao. Hivyo tunapokuwa tayari kuipokea neema na Injili yake, ndivyo neema itakavyotujia zaidi. Kama vile mwitikio wa Maria kupokea mpango wa Mungu, ulileta mabadiliko makubwa katika historia ya mwanadamu. Mwitikio wetu utakuwa chanzo cha mengi makubwa ambayo hata hatukutegemea.
Sala; Ee Bwana niangaze nipate kuwa tayari kupokea neema yako. Amina
Maoni
Ingia utoe maoni