Jumanne, Aprili 11, 2017
Jumanne, Aprili 11, 2017,
Juma Kuu
Isa 49: 1-6;
Zab 71: 1-6, 15, 17;
Yn 13: 21-33, 36-38.
KUWA HURU KUMCHAGUA YESU!
Ni juma la mwisho Yesu yupo na wafuasi wake kabla ya kufa. Wote kumi na tatu wanakula mlo wa Pasaka na ni muda muhimu. Yesu anaeleza kuhusu yule atakaye msaliti “amin nawaambieni mmoja wenu atanisaliti”. Hakuna aliye amini kwamba atakuwa yeye, “hakika sio mimi”. Majivuno ni kitu ambacho kinatufanya tusikubali makosa yetu na hili ndilo linalo tokea wakati wa mlo huu. “Mtanipa nini kama nikimtoa kwenu?” ndivyo Yuda anavyomsaliti kwasababu ya tamaa. Petro anamkana kwasababu ya woga wa maisha yake mwenyewe, anasema uongo ili aweze kukwepa hatari.
Yesu alikuwa na moyo wa Kibinadamu na alimpenda Yuda kwa mapendo ya Kimungu kwa njia ya moyo wake wa kibinadamu. Kwa matokeo ya upendo huu mkamilifu wa Yesu kwa Yuda, moyo wa Yesu unasumbuka. Si kwamba Yesu mwenyewe aliumizwa au kuwa na hasira kwa usaliti wa Yuda. Bali, ni kwamba moyo wa Yesu ulichomwa kwa uchungu kwamba Yuda anapotea, ambaye alikuwa anampenda kwa mapendo kamili. Yuda alikuwa na uhuru kamili, lakini alichagua kumsaliti Yesu. Hili ni kweli hata kwetu pia. Sisi tuna uhuru kamili na tumepewa uwezo huo huo ambayo Yuda alikuwa nao kumpenda Yesu kwa mapendo kamili au kumsaliti. Tunaweza kuruhusu zawadi yake ya ukombozi iingie katika maisha yetu au kuikataa. Ni juu ya uwezo wetu kamili.
Juma kuu ni kipindi cha kuzama ndani kabisa na kujitazama upo katika barabara ipi. Kila wakati na kila siku unaitwa na Mungu kumchagua yeye kwa upendo wako wote. Lakini kama ilivyokuwa kwa Petro na Yuda, mara nyingi tunamkana na kumsaliti. Tunashindwa kabisa kutoa maisha yetu katika hali ya sadaka na kwa ukarimu kama alivyo fanya Bwana. Katika juma hili kuu, tujitafiti kwa undani kabisa, kama nipo tayari kutafuta msamaha kwa Yesu wa Huruma? Tumrudie Yesu na tumfuate na msalaba katika juma hili.
Sala: Bwana, ninakupenda wewe, lakini ninatambua kuwa nina kuhuzunisha moyo wako kwa kukusaliti kwangu. Nisaidie niweze kuona dhambi yangu katika kweli juma hili. Kwa kuiona ninaomba niachane na kile kinacho nifanya daima niwe mbali nawe katika kukupenda, ili niweze kutembea nawe katika msalaba na kushiriki utukufu wako. Yesu, ninakuamini wewe. Amina.
Maoni
Ingia utoe maoni