Ijumaa. 17 Mei. 2024

Tafakari

Alhamisi, Julai 28, 2016

Alhamisi, Julai 28, 2016,
Juma la 17 la mwaka C wa Kanisa

Kumbukumbu ya Mt. Alfonsa wa Muttathupadathu.

Yer 18: 1-6;
Zab 145: 2-6;
Mt 13: 47-53


MFINYANZI MTAKATIFU!

Katika lirtujia ya neno la Mungu leo, mwalimu mwenye hekima anatumia mifano miwili kutoka katika uhalisia wa maisha yetu ya kila siku ili kutufundisha kitu cha hali ya juu. Anatumia, udongo, chungu na mfinyanzi na mfano wa neti inayotumiwa na mvuvi kuvulia samaki. Wakati la kwanza likitueleza kuna maovu duniani, mabaya, mapungufu na dhambi ambayo Mungu atahukumu siku moja, na lingine linatuambia kwamba mpango wa Mungu ni kutusafisha nakututakasa kutoka katika maovu yote na kutufinyanga na kutubadili siku kwa siku ili tufanane naye. Ni Neema ya Kimungu ambayo Mungu anaiweka ndani mwetu ambayo itatutakasa na kutubadili.

Mungu ambaye ni Mfinyanzi Mtakatifu ametupa njia nyingi za sisi kujivika neema yake, Neno la Mungu, sakramenti ya Ekaristi na Kitubio, maisha ya sala, kufunga na kuomba toba, huruma na kufanya matendo ya huruma, kuvumilia kila wakati na kubeba misalaba yetu kila siku na mengine mengi. Yote haya yatatuongoza kwenye njia ya utakatifu na neema. Sasa tujivike neema ya Mungu isiyo na kikomo ambayo yeye mwenyewe kama Mfinyanzi Mtakatifu yupo tayari kutupatia ili kukua katika neema mpaka hapo tutakapo pata yote katika ukamilifu wote kwenye Ufalme wake.

Sala ya Mt. Alfonsa: Ee Bwana Yesu, nifiche katika madonda ya Moyo wako Mtakatifu. Niondoe katika hamu yangu ya kupenda kupendwa na kuheshimiwa. Nifanye mimi niwe mmoja nawe. Amina.

Maoni


Ingia utoe maoni