Jumapili, Mei 11, 2025
Jumapili, Mei 11, 2025.
Dominika ya 4 ya Pasaka
Mdo 13: 14, 43-52;
Zab 100: 1-3, 5;
Ufu 7: 9, 14-17;
Yn 10: 27-30.
MCHUNGAJI MWEMA ANAITA KONDOO WAKE!
Dominika ya nne ya kipindi cha Pasaka, inajulikana kama “Dominika ya Kristo Mchungaji mwema”, Injili inachukuliwa kutoka sura ya 10 ya Yohane ambapo Yesu anazungumza juu ya yeye mwenyewe kama "Mchungaji Mwema". Yesu ametupa takwimu ya Mchungaji Mwema ambaye anajua kondoo wake anawaita, yeye huwalisha na anawaongoza wao. Kwa sababu hii, Kanisa linachukulia Dominika hii kuwa maalumu kuwa “Siku ya Kuombea Miito Duniani”.
Leo, Kanisa zima linatukumbusha hitaji letu kuomba, kama Yesu mwenyewe alivyo waambia wanafunzi wake, hivyo kwamba "mwombeni Bwana wa mavuno apeleke watenda kazi katika mavuno yake" (Lk 10: 2). Tangu hapo awali Kanisa “ kwa asili yake ni umisionari" (Ad Gentes, 2), wito wa Ukristo unazaliwa ndani ya watu kutokana na kazi ya umisionari. Kusikia na kufuata sauti ya Kristo Mchungaji mwema, maana yake ni kuruhusi tuvutwe naye na tuongozwe naye, kujiweka wakfu kwake maana yake kumruhusu Roho Mtakatifu kututumia sisi katika mabadiliko haya ya umisionari, na kuamsha ndani yetu tamaa, furaha na ujasiri wa kutoa maisha yetu wenyewe katika utumishi wa Ufalme wa Mungu.
Katika mzizi wa kila wito wa Kikristo tunaona harakati hii ya msingi, ya kuacha nyuma faraja yetu na mambo yote yanaotupendezesha nafsi zetu na kukita maisha yetu katika Yesu Kristo. Ina maana ya kuondoka, kama Ibrahimu, na kuacha sehemu yetu ya asili na kwenda mbele kwa uaminifu, tukijua kwamba Mungu atatuonesha njia ya nchi mpya. Hii "kwenda mbele" isi tazamwe kama ishara ya mpango tu wa maisha ya mtu binafsi, hisia ya mtu, utu wa mtu mwenyewe. Kinyume chake, wale ambao wanamfuata Kristo wanapata uzima kwa wingi kwa kujiweka wenyewe bila kujibakiza katika utumishi wa Mungu na ufalme wake. Wito wa Kikristo kwanza kabisa ni wito wa upendo, upendo ambao hutuvuta sisi na kutuelekeza nje ya sisi wenyewe. Kuitika wito wa Mungu, maana yake kumruhusu yeye atusaidie kujiacha wenyewe kwakuondokana na usalama wetu wa uongo, na kutoka nje na kuenenda kwenye njia inayo ongoza kwa Yesu Kristo, aliye asili na hatima ya maisha yetu na furaha yetu.
Katika siku hizi kwanza tunaombwa tuombee Kanisa liweze kupata wachungaji wema na waadilifu wa kufanya kazi ya Kristo ya kueneza Injili, na kwamba Kanisa liweze kupata vijana wengi wanoitwa kwenye wito wa upadre na utawa ikiwa ni pamoja na watoto wetu wenyewe.
Sala:
Baba wa huruma, uliyemtoa mwanao kwaajili ya wokovu wetu na ambaye anatutia nguvu kila wakati kwa zawadi ya Roho wako, tujaliye sisi jumuiya ya Wakristo tulio hai, upendo na furaha, vilivyo vya muhimu kwa maisha ya kindugu, na vinavyojenga ndani ya wadogo mwamko wa wito wakujitoa wenyewe wakfu kwako na kwaajili ya wito wa uenezaji wa neno lako.
Amina
Maoni
Ingia utoe maoni