Jumamosi. 23 Novemba. 2024

Tafakari

Jumapili, Novemba 10, 2024

Jumapili, Novemba 10, 2024.
Dominika ya 32 ya Mwaka wa Kanisa

1 Fal 17: 10-16;
Zab 146: 6-10 (K) 1;
Ebr 9: 24-28;
Mk 12: 38-44.


DHANA YA UKARIMU KWA KUTOA

John F Kennedy alisema “… usiulize nchi yako imekufanyia nini bali uliza nimeifanyia nini nchi yangu.” Tunaweza kuitumia na sisi katika hali ya kiroho, “tusiulize Mungu amenipatia nini bali jiulize umemfanyia nini Mungu”. Tabia yetu ya kibinadamu ni kupenda kutoa kidogo na kutegemea kupata kikubwa. Kwa mfano tunakwepa kulipa kodi, huku tukitegemea serikali ifanye huduma zote kwa ajili ya manufaa yetu. Tunapoteza muda wetu bila kufanya chochote lakini tunategemea maisha yawe mazuri na bora. Hatufanyi kitu chochote kwa Mungu lakini muda wote tunaomba neema na maisha mazuri.

Liturjia ya leo inatualika sisi tujitazame tuwe watu wakutoa sana bila kutegemea kulipwa kingi au kurudishiwa. Tunapo toa kingi na kumwachia Mungu tunampatia muda wa kututizama na kutujali kama sisi tunavyojali. Tunakuwa na ile hali ya kumtegemea Mungu. Tunapomtegemea yeye daima hatatuangusha kamwe.

Katika somo la kwanza mjane wa Serapta alikuwa hana kitu cha zaidi cha kutoa lakini kwa ukarimu wake akatoa kile kidogo alicho nacho kwa ajili ya nabii wa Mungu, alienda nyumbani na kuchukua kidogo alicho nacho. Hakulia kwanini Mungu hakumpatia mahitaji muhimu. Hakuwa na wasi wasi atakunywa nini au atakula nini, lakini alitegemea Mungu atamlinda na kumtunza na ndio maana alitoa kwa ukarimu, na hatimaye kukatokea muujiza. Debe lake halikupungua.

Katika hali ile ile mjane katika somo la Injili leo tunamuona naye anatoa kile alichokuwa nacho. Alitoa kila kitu alichokuwa nacho ndio maana Yesu anamsifu, kwa kusema kwamba mama huyu ameweka nyingi kuliko wengine. Hii ni kwasababu hakubaki na chochote kwa ajili ya nafsi yake. Mama huyu hakulalamika kwa Mungu kwa akidogo alichokuwa nacho yeye alijisikia salama na akatoa kwa moyo wote na kumrudishia Mungu kama shukrani. Hawa wanawake wawili walikuwa na moyo wa kutoa si kwasababu walikuwa na vingi, bali ni kwasababu walikuwa na matumaini yao yote kwa Mungu. Hawakuwa na wasiwasi familia zao zitakuwaje. Walitoa kwa moyo wa ukarimu.

Ukarimu wa kweli hautoki kutokana na mali tulizonazo katika stoo zetu bali unatokana na Imani yetu kuu tulionayo kwa Mungu, kwamba Mungu ndiye mpaji wetu, ndiye mtoaji wa vyote. Kijana mmoja siku moja alitaka kuona ni namna gani muombaji anavyojisikia, alivaa nguo chafu na kwenda kukaa karibu na muombaji mmoja, akamsalimia. Huyu kijana akamlilia mwenzake na kumwambia sijapata chochote leo. Akamuomba kama anaweza kupata chochote cha kula. Bila kusita huyu akatoa mkate wake mmoja ambao alikuwa ameupata siku hiyo, akaukata na kumpatia. Kijana huyu aliguswa sana kwamba pamoja na shida zake lakini amekua tayari kushirikisha kile kidogo alichokuwa nacho. Hapo akampeleka yule ombaomba nyumbani kwake akampatia sehemu ya mali yake na kumwambia kwasababu ya kile kipande cha mkate, mimi nami nakumegea mkate wangu. Akajifunza dhana ya kushirikisha vile vitu ambavyo Mungu amempatia, kuwapati wengine kwa uhuru.

Tujichunguze leo, hivi mimi nimekuwa mkarimu kwa ndugu zangu, majirani, marafiki na watu wote kama vile Mungu alivyo na ukarimu kwangu? Je, nimelalamika kwa hali ngumu katika maisha yangu? Nipo tayari kujifunza namna ya kuwa mkarimu na kushirikisha yale yote ambayo Mungu amenipatia kutoka katika mikono yake.

Sala:
Bwana, nisadie mimi niweze kuwa mtu wa sala na kukuabudu kweli. Nisaidie mimi niweze kukupenda kwa mapendo yako pekee. Nisaidie niweze kuwa mkarimu kwa yale ulionipatia na wengine, hasa wale waliowahitaji.
Amina.

Maoni


Ingia utoe maoni