Alhamisi, Agosti 15, 2024
Alhamisi, Agosti 15 2024
Juma la 19 la Mwaka
SIKUKUU YA KUPALIZWA BIKIRA MARIA MBINGUNI
Ufu 11:19, 12:1-6, 10;
Zab 45:9-11, 15 (K) 10;
1Kor 15:20-26;
Lk 1:39-56
MALENGO YA JITIHADA ZETU!
Katika sikukuu ya Kupalizwa Mbinguni kwa Mama wa Mungu, tunafanya sherehe ya Bikira Maria kutoka katika hali ya ubinadamu mpaka kufika hali ya mwenye heri. Kwa kumtafakari Bikira Maria katika utukufu wake, tunaelewa kuwa hapa duniani sio kwetu bali tu wapitaji, pia tunaelewa kuwa tunatakiwa kuishi hapa duniani tukiwa tumejawa na tamaa ya vitu vya mbinguni basi kwa kufanya hivyo tutarithi vivyo vitu katika ufalme wa milele. Kwa kusema hivyo basi tujitahidi kutunza amani na utulivu wa mioyo yetu, japokuwa tumesongwa na magumu ya maisha. Mwangaza wa Bikira Maria akiwa amechukuliwa mbinguni huendelea kuonekana japokuwa wingi zito la huzuni na mateso limetanda.
Katika sikukuuu ya Kupalizwa Mbinguni Bikira Maria tunakumbuka kushiriki kwa Bikira Maria katika Ufufuko wa mwanae, kwa kupalizwa mbinguni mwili na roho, alipomaliza kile alichokijia hapa duniani. Kupalizwa Mbinguni kunatuonyesha kile kitakachotutokea pale tutakapofufuliwa siku ya mwisho. Kupalizwa mbinguni ndio lengo kuu la maisha yetu kama Wakristo.
Kama vile Mt. Paulo atuambiapo kuwa, tutafufuliwa na miili yetu iliyo tukuka kama ilivyokuwa kwa Kristo. Kwa ile nguvu ya Yesu mfufuka tutaweza kuungana na Baba katika utukufu wa Kristo, kama vile Bikira Maria anavyoshiriki katika muungano huo kwa sasa. Kupalizwa Mbinguni ni siku ambayo tunaitwa kutafakari kwa kina malengo ya maisha yetu, na urithi wa uzima wa milele.
Kwa kusema hivyo basi tujitahidi kuyawaza hayo kila siku. Inatulazimu kufikiria kuwa tumesimama na Bikira Maria na mwezi nchini ya miguu yake, akiwa wamevaa taji la jua na nyota kichwani mwake. Pia inatubidi kumwona yule joka limefungwa, na kila mmoja wetu kwa neema aliyopewa na Mungu na kwa msaada wa Bikira maria anatakiwa kumzaa Kristo katika maisha yake. kwa kufanya hivyo basi tutakuwa na uhakika wa kufufuliwa mwili na roho.kwa kufanya hivyo basi tunakuwa tumepata maana halisi ya maisha yetu, na kwamba ukweli unaoelezewa katika mafundisho ya kanisa juu ya kupalizwa Bikira Maria ndio utimilifu wa matamanio ya maisha yetu.
Sala:
Ewe mama uliyejaa msamaha, utukufu wako unisaidie kuyabeza na kuyachukia yale yaliyo ya dunia na kutamani yale yaliyo ya mbinguni.
Amina
Maoni
Ingia utoe maoni