Jumatano. 30 Oktoba. 2024

Tafakari

Jumapili, Agosti 25, 2024

Agosti 25, 2024,
Dominika ya 21 ya Mwaka

Yos 24: 1-2, 15-18;
Zab 34: 1-2, 15-22 (K) 8;
Efe 5: 21-32;
Yn 6: 60-69.


YESU NI SAUTI YA MUNGU


Mwalimu mmoja, aliwauliza wanafunzi wake: “Je, sauti ya Mungu inasikika namna gani?” Wanafunzi walipatwa na mshangao, hawakujibu swali hilo. Wanafunzi wote walikuwa wanashauku ya kusikia namna gani mwalimu wao angejibu swali lile. Mwalimu alianza: Sauti ya Mungu ni kama ileya rafiki yako wa karibu, na kama mtu unayemwamini, mtu ambaye unayeweza kuongea naye mambo yako ya faragha yaani mambo yako ya sirini. Sauti ya Mungu husikika kama Mama yako au Baba yako au Dada yako au Kaka yako, wakati ambapo wanakufariji kwa sababu mara kwa mara penigine umeota ndoto mbaya majira ya usiku. Unawasikia wakiwa karibu na kitanda chako wakisema: “Usiogope! usiogope! Nipo karibu yako usijali”. Yesu ni sauti ya Mungu. Katika sauti hiyo tunaweza kusikia faraja ya rafiki, maneno yenye nguvu na ushujaa kutoka kwa mkubwa, maneno ya amani na msamaha kutoka kwa Mungu.

Katika Injili ya leo, wakati baadhi ya wafuasi waliposhindwa kumfuata Yesu kwa sababu waliona misemo yake haikubaliki, Yesu Kristo aligeuka na kuwaelekea wafuasi na kuwauliza, “je, nanyi pia mwataka kwenda zenu?” Simoni Petro akamjibu, “Bwana, twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele. Nasi tumesadiki, tena tumejua, ya kuwa wewe ndiwe Mtakatifu wa Mungu.”

Petro na wanafunzi wengine walikuwa na Yesu kwa muda fulani, walisikia kinywa chake kikitamka maneno ya msamaha; waliona pia nguvu ya maneno yake pale alipokemea mapepo toka kwa watu; waliona sauti yake ikiwaponya wagonjwa, vilema na wenye ukoma; waliona sauti yake ikiwainua wafu na kuwapa uhai.

Katika maneno na matendo ya Yesu kuna ishara ya mambo ya mbinguni. Yeye alisema, “mbingu na dunia zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe.” Yesu aliumega mwili wake na alimwaga damu yake ili kutupatia uzima wa milele. Yeye alisema anayekula mwili wangu na kunywa damu yangu anao uzima wa milele. Yeyote anayeamini maneno haya ya Yesu na kuyashika kikamilifu katika Ekaristi Takatifu atakuwa na uzima wa milele. Leo tunaalikwa sote tukiri imani yetu na kuungana na Petro tuseme, “Bwana, Wewe unayo maneno ya uzima wa milele.” Yoshua naye kama Yesu katika somo la kwanza anawapa wazee wa Israeli uhuru wa kuchagua kumtumikia Mungu au kumwacha. Daima Mungu hamsukumi mtu yeyote kumchagua, amekupa uhuru kamili ili uweze kumchagua kwa moyo wote na kama hutapenda kumchagua basi itakuwa umeamua mwenyewe. Na kitakacho kuhukumu ni matokeo ya uhuru wako mwenyewe. Mchague Mungu ili ubaki salama katika maisha ya neema.

Sala:
Ee Bwana Yesu, Naomba kusikiliza maneno yako ya uzima wa milele kila wakati.
Amina!

Maoni


Ingia utoe maoni