Alhamisi. 21 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatatu, Agosti 26, 2024

Tafakari ya kila siku
Jumatatu, Agosti 26, 2024.
Juma la 21 la Mwaka


2 Thes 1:1-5, 11-12;
Zab 96:1-5,
Mt 23:13-22


KUONDOA SURA YA UNAFIKI!


Mafarisayo na Masadukayo walikosa ukweli wa dhamira zao, zilizo hitajika kumpendezesha Mungu. Dhamiri ni hekalu ambamo mtu binafsi hukutana na Mungu na tunasikia sauti ya Roho Mtakatifu ikiongea nasi ndani kabisa mwa moyo. Kwenda kinyume na dhamiri hizo ni kwenda kinyume na kile kilicho cha kweli, ni kujikatalia wenyewe kilicho muhimu kwa wokovu wetu. Dhamiri iliyo hai ni thamani kuu ambayo tunaweza kuwa nayo katika maisha ya sasa. Inatupa Amani, uaminifu na kutuhakikishia kuvumilia katika kutenda mema.

Yesu ni mkali kweli kwa wale wote ambao wanaleta makwazo kwa wengine na kuwaongoza katika upotevu, hasa wale wenye jukumu la kuwafundisha wengine njia ya wokovu. Ni dhambi mbaya kuonesha mfano mbaya na kuwaongoza wengine kwenye dhambi na kukwepa ukweli. Wokovu wa kila mmoja wetu unaunganishwa pamoja; tunapaswa kujengana wenyewe katika njia ya Kristo. Wengine wana haki ya kuona mifano yetu mizuri na kuongea kwetu ukweli. Yesu anataka tuwe waaminifu kwa yale tunayosema na kutenda, ili utu wa maisha yetu uweze kuonekana wazi kwa wote.

Tafakari leo, kama unateseka na dhambi ya binafsi ya kutokuwa na haki ya kuonesha mfano mzuri. Je, wewe ni mtawa? Waonesha mfano mzuri? Je wewe ni padre? Unaonesha mfano mzuri? Tafakari juu ya maisha unayoishi mbele ya kondoo uliokabidhiwa, Yesu anatukumbusha tena kurudi nyuma na kujichunguza kama tunacho wahubiria tunakiishi! Kama sivyo basi, Yesu anatualika tuanze tena upya na kumuiga yeye mwenyewe alivyokuwa mfano kwa kundi nzima. Tufanye hivyo ili tusifanye kazi bure.

Sala:
Bwana, ninapo anguka katika dhambi ya kutokujitambua na kuwa na majivuno, ninakuomba unishushe na kuniweka katika kiini cha ndani cha wito wangu. Ninaomba unipe hekima, nguvu na huruma katika maisha ili niweze kuwasaida wadhambi wote wakurudie wewe. Yesu, nakuamini wewe.
Amina.

Maoni


Ingia utoe maoni