Alhamisi. 21 Novemba. 2024

Tafakari

Jumapili, Juni 23, 2024

Jumapili, Juni, 23, 2024
Tafakari ya kila siku
Juma la 12 la Mwaka wa Kanisa

Ayu 38:1, 8-11;
Zab 107 : 23-26, 28-31;
2 Kor 5 :14-17;
Mk 4: 35-41


KATIKA BWANA YESU HAKUNA LO LOTE LINALO SHINDIKANA



Je chakula tunachokula siku ya leo tuna uhakika gani kwamba ni salama na kinaweza kuliwa? Vitu mbalimbali tunavyotumia kila wakati tuna uhakika gani kama salama na vinaweza kutumiwa? Kwa kuwa hatuna uwezo wala wataalamu wa kupima vitu hivyo kwa uhakika zaidi. Kwa hiyo tunatumaini kwamba kila kitu ni salama, kizuri na kinafaa. La sivyo tunageogopa kula chakula tunachonunua na kutumia tekinolojia ya kisasa.

Je itakuaje kwa watu na marafiki tunaowatumainia kwamba wao ni wema, na kwamba hawana silaha ambazo zinaweza kutudhuru na kwamba hawatuonei wivu? Kama tukiwa na wasiwasi itakuwa vigumu kuishi nao. Tunaweza kutafuta njia nyingine ya uhakika ambayo inaweza kufanya pia maisha kuonekana magumu zaidi.

Kwa namna hiyo kumtumainia Mungu ni muhimu sana ili kuweza kuishi maisha ya kikristu na ya maana zaidi. Hivyo basi twaweza kumtumainia Mungu siku zote naye yupo kwa ajili yetu. Hivyo masomo ya leo ndivyo yanavyotuambia.

Katika somo la kwanza tunamuona Ayubu alikuwa na matatizo makubwa sana. Alitaka kujua kwa nini alikuwa anateseka sana. Nyakati hizo mateso yalifikiriwa ni adhabu kwa dhambi. Lakini Ayubu alijua kwamba anaishi maisha mema, kwa nini Mungu alimpelekea majanga mbalimbali maishani mwake? Mwishoni Ayubu alipata majibu. Na katika dhoruba Mungu aliongea naye. Alimkumbusha Ayubu kwamba ni namna gani yeye na wanadamu wengine wanaufahamu mdogo, kwa mfano Mungu alimuuliza Ayubu nani alizuia bahari ili wao wasizurike? Ni sawa Ayubu alijua kwamba Mungu alifanya hivyo, lakini Ayubu hakuweza kujua kwa namna gani Mungu alifanya hivyo? Kama Mungu alifanya hivyo kwa busara na upendo, hakika Ayubu lazima kumwamini Mungu.

Katika somo la pili Mt. Paulo anawakumbusha wakorintho na sisi pia katika shida zote za maisha, ni upendo wa Kristo ambao unaonekana. Hakuna wasiwasi kwa upendo unaotoka kwa Bwana Yesu. Inabakia zamu ya kila mmoja kurudisha upendo wa Bwana Yesu kwa njia ambazo Paulo ameziorodhesha, kwa kufuata matendo ya Bwana Yesu, kwa kuishi si kwa ajili yako bali kwa kusiadia wengine na kwa kuona vitu vyote kwa imani mpya. Ambayo si kitu kingine bali kuamini katika upendo wa Bwana Yesu.

Katika Injili tunawaona wanafunzi wakiwa na Bwana Yesu katika bahari ya Galilaya. Gafla mawimbi yakaja. Bwana Yesu alikuwa amelala. Wanafunzi waliogopa na walianza kulia kwa kutaka msaada, mwalimu tunaangamia. Aliamka na kukemea mawimbi na aliamrisha pepo za bahari kutulia. Kisha Bwana Yesu aliwauliza wanafunzi, kwanini mlikuamnaogopa sana, na kwa nini mlikosa imani? Ujumbe wa masomo ya leo unaeleweka kabisa – kumuamini Mungu. Tunaweza kushindwa kutatua misukosuko na matatizo katika maisha, lakini tunaweza kujua kwamba hakuna mawimbi, hakuna majanga, hakuna kitu chochote kile kinachoweza kupinga mpango wa Mungu.

Maisha yetu ya sasa yana kila aina ya mawimbi, kama magonjwa, maafa, ukame, njaa, chuki, uonevu, usaliti na ubinafsi. Kwa kuwa kama wakristu tunaompokea Bwana Yesu aimaanishi kwamba tukiwa baharini hatutapata matatizo ye yote. Kwa namna nyingine Bwana Yesu anatualika kuweza kusafiri kwenye maji taabu zote za duniani, ikiwa tu tutamwamini na kumfuata maishani mwetu.

Kusafiri na kuwa wafuasi wa Bwana Yesu ni kusafiri katika mawimbi na siyo kuyakwepa. Wafuasi wa Bwana Yesu waliendelea kupambana na matatizo mbalimbali pamoja na kukataliwa. Hatimaye wengi wao walikuja kukumbana na vifo vya ukatili katika kumtangaza Bwana Yesu. Kilichowafanya wao waendelee na ufuasi ndicho kinacho tufanya sisi tuendelee. Uhakikia kwamba Bwana Yesu ni jibu la kero zote, na matatizo yote katika maisha. Katika Bwana Yesu hakuna lo lote linalo shindikana.

Maoni


Ingia utoe maoni