Ijumaa. 18 Oktoba. 2024

Tafakari

Jumapili, Julai 21, 2024

Julai 21, 2024
Dominika ya 16 ya Mwaka

Yer 23:1-6;
Zab 23 (K) 1;
Efe 2:13-18;
Mk 6:30-34.


KAMA KONDOO WASIO NA MCHUNGAJI !


Wakati Yesu na wanafunzi wake walipoenda mahali pa faragha kwa ajili ya kupumzika, watu walienda mbio huko kumsikiliza na kupata Baraka. Makutano waliwaendea faraghani, lakini Kristo hakuwalaumu; waliingia bila kukaribishwa wala kutakiwa kwenye pumziko lao walilolistahili, lakini Yesu hakupatwa na uchungu wowote.Badala yake aliwaonea huruma akisema kwamba walikuwa kama kondoo wasio na mchungaji. Ilikuwa ni umati wa watu, ambaowalikuwa na hamu ya kufundishwa, lakini hapakuwa na mtu wa kuwafundisha; walihitaji kulishwa na mafundisho mazuri, lakini hapakuwa na wakuwalisha. Kwa hiyo, Alikuwa na huruma juu yao, na hakuwafundisha tu, pia aliwaponya waliokuwa wagonjwa.

Katika somo la kwanza nabii Yeremia anaonesha kasoro za wachungaji wa taifa la Mungu katika Agano la Kale. Katika nabii Yerernia, Mungu anakemea tabia mbaya za viongozi wa Israeli zilizopelekea taifa zima la Mungu kuangamia kwa kupelekwa utumwani katika uchi ya Babeli. Mungu anaahidi kuchipusha chipukizi la haki kutoka shina la Daudi, atakayemiliki ufalme na kutenda kwa haki. Utabiri huu unatimia katika Yesu Kristo aliye mchungaji mwema wa kundi lake

Yesu Kristo ni Mchungaji Mwema. Viongozi wa Agano la Kale walitambua na kujiona kuwa wamechaguliwa na Mungu kuliongoza taifa a Israeli, lakini walishindwa kutimiza wajibu wao ipasavyo. Kristo Yesu ni Mchungaji ya hakika. Alianza kuhubiri na kukusanya taifa la Mungu, amewagawia Mwili na Damu yake (Ekaristi Takatifu) na Neno lake, yaani mafundisho yake kwa watu wote

Katika maisha yetu na katika sehemu mbalimbali kama vile: familia, jumuiya, serikali, kanisa n.k. viongozi na watu wale wanapaswa kuiga mfumo wa Yesu. Tunakumbushwa tena leo wachungaji lazima wawe na upendo, huruma, upole, uvumilivu na unyenyekevu katika shughuli zao. Tukiwa tayari wafuasi wa Kristo tuwe na roho ya huruma kwa wengine.

Sala:
Bwana, Tusaidie kuwa viongozi vema kufuata mfano yako.
Amina!

Maoni


Ingia utoe maoni