Alhamisi. 21 Novemba. 2024

Tafakari

Jumamosi, Agosti 03, 2024

Jumamosi, Agosti 3, 2024
Tafakari ya kila siku
Juma la 17 la Mwaka wa Kanisa


Yer 26: 11-16, 24;
Zab 69: 14-15, 29-30, 32-33;
Mt 14: 1-12


UCHAGUZI SAHIHI!

Masomo ya leo yanahusu mateso ya watumishi wa Mungu. Yeremia aliteseka, huku Yohane anauwawa kwasababu ambazo zina uoga ndani yake. Tuangalie tabia za Herode na Herodia ambao wanahusika na kifo cha Yohane Mbatizaji. Herode alikuwa mtu wa ulimwengu. Aliishi pia kwa hofu na woga. Pengine Herode alikuwa na vingi vya kunywa katika siku yake ya kuzaliwa mpaka akatoa ahadi ambayo hakufikiri sana, ambayo mke wake Herodia alipata nafasi wa kutimiza nia yake ovu. Herode anafanya kitu bila kufikiri ili kumfurahisha mke wake. Mtu wa majivuno, Herode anaamuru Yohane akatwe kichwa na akapewa mkewe. Ni ajabu Herodia hata dhamiri yake haikuwa na wasi wasi katika kutenda uovu wake kwa kumshauri mwanaye aombe jambo baya.

Pengine sisi kama wazazi tunawashauri watoto wetu watende matendo ghani? Pengine wakituletea fedha au mali ambazo kwa hakika unatambua sio halali tunawashaurije, tunajaribu hata kuchunguza kapata wapi pengine kuendana nahali yake ilivyo? Je! pengine tumezoea kutenda maovu kiasi kwamba dhamiri zetu hazitushtaki tena? Lugha tunazotumia, hatuhalalishi lugha mbaya nakuchukulia tu hali ya kawaida? Je tunamkumbuka Mungu tunapofurahi au tunapopatwa na mateso au tunaamua tuu maamuzi yetu bila kujali amri za Mungu kama Herode? Je tunalinda uhai wa binadamu wenzetu? Tunatambua kwamba uhai wa kila mtu ni zawaidi ya pekee kwa Mungu? Je, tunawaua wenzetu kwakuwasema vibaya na kuharibu utu wao, kiasi kwamba wanashindwa kueleweka na jamii?

Ujumbe wetu leo ni kwamba tujiulize tunakabilianaje na maswala ya maadali tunayokumbana nayo. Je tunafikiria kuhusu uovu wetu na kujaribu kuwafanya wengine wafanye hayo hayo, tukiwaambia wafanye ni mazuri ili sisi wenyewe tufiche uovu wetu? Kitu chema kinatoka kwenye kitu chema. Huwezi kutenda dhambi utegemee neema. Tubadili mienendo yetu tuishi kadiri atakavyo Mungu.

Sala:
Ee Roho Mtakatifu angaza giza la moyo na akili yangu ili kila wakati niweze kuchagua lililo jema na unipe nguvu ya kuishi kadiri ya hilo jema.
Amina.

Maoni


Ingia utoe maoni