Jumapili, Agosti 04, 2024
Jumapili Tafakari ya kila siku
Juma la 18 la Mwaka wa Kanisa
Kutoka 16:2-4, 12-15
Waefeso 4:17, 20-24
Yn 6:24-35
WATU WANAMFUTA YESU
Siku moja mzee mmoja alikuwa na kijana wake mgonjwa. Alienda hospitali na kufika kule, huku hali ya mtoto wake ikiendelea kuwa mbaya zaidi. Lakini kwa bahati mbaya daktari hakuwepo na hivyo walimsubiri huku Nesi akimpigia simu aje kwaharaka kwani hali ya mtoto wa huyu mzee ilikuwa inaendelea kuwa mbaya. Mzee alikuwa akihangaika tena huku akilia, na mara gafla yule daktari akaja huku akikimbia anatokwa na jasho, huku ameshikilia simu sikioni akiongea na kujaribu kuvaa koti lake jeupe ili aanze kazi. Yule mzee akalalamika sana kwamba mtoto wake anakufa hivi hivi na Daktari anaongea na simu, hivi madaktari wa siku hizi wako je? Wanafundishwa nini? Aliongea huyu mzee.
Mara Daktari akaingia katika chumba cha matibabu mtoto akapelekwa wa yule mzee, daktari akampa matibabu na kumfanyia upasuaji mdogo, akaanza kujisikia vizuri na kuanza kupata hali ya kawaida. Ndipo yule daktari akatoka akamuaga Nesi harakaharaka na kuondoka. Yule mzee akamuuliza Nesi mbona huyu Daktari ana haraka namna hiyo? Yule Nesi akamwambia huyu daktari usimuone hivyo mtoto wake alipata ajali jana na kufariki hivyo tulivyo muita alikuwa katika mipango ya mazishi ya mtoto wake, ndio maana hajatulia kwakweli. Yule mzee akaumia kwasababu alikuwa ameshamuhukumu vibaya kwa kumuona kana kwamba amekosa maadili kumbe, daktari amejitoa sadaka kwa ajili ya mtoto wake.
Wana Waisraeli katika somo la kwanza Mungu amejitoa sadaka kwa ajili yao na hata Musa na Haroni wamejitoa sadaka kuwasaidia kutoka katika utumwa lakini wana wa Israeli hawalioni hilo wanalalamika jangwani. Wanawaza kama wengi wetu wakati mwingine tunamwambia Mungu. “Jioneshe kama wewe ni Mungu. Fanya kitu uoneshe nguvu yako ili sisi tukuabudu. Usijifiche”.
Hakuna kitu hata kimoja kinacho waridhisha watu. Sio wana wa Israeli katika Agano la Kale lakini pia hata watu wetu wa sasa. Wanajiona wapo katika hali mbaya na wanamuona Mungu kama ndio msababishi wa haya yote. Wanajiuliza hivi kuna Mungu kweli? Pengine hayupo. Mara nyingi wamekuwa wakipenda miujiza mikali ambayo wakati mwinigne ni udanganyifu huku wakitaka kupata ukweli kuhusu uwepo wa Mungu.
Katika somo la hili la kwanza kutoka katika kitabu cha Kutoka, watu wanataka kitu na Mungu anawapatia wanachotaka. Lakini ni ajabu kwamba wameanza kulalamika tena kwa kile alichowapa Mungu, kwasababu sio kile ambacho wanataka. Sisi pia tupo hivyo. Tunakila kitu lakini bado tunalalmika tunahitaji zaidi na zaidi. Tuna hiki lakini tunataka hiki, tuna vitu ambavyo wengine wanavihitaji. Tunajiuliza hivi tunaweza kuridhika na vitu tulivyo navyo na kumtafuta Mungu?
Somo la pili ni kutoka katika waraka kwa Waefeso. Tunaweza kuweka msisitizo katika mstari huu. “Tunaweza kuweka mbali mambo ya maisha ya zamani yaliojaa tamaa, uharibifu, na kufanywa upya katika Roho na kuwa na nafsi mpya”. Tamaa mbaya, hili ndilo somo la kwanza liliongelea. Kila wakati tunatamani. Lakini sio mara zote tunaangalia kama tamaa yetu inatuongoza kwa Mungu. Badala yake tunataka tamaa zetu ziheshimiwe hata kama ni mbaya au nzuri. Ni kweli kutamani kwetu kunapaswa kuheshimiwa lakini lazima kuongozwe kwa mfano wa Yesu mwenyewe. Na tujaribu kuishi kama yeye alivyoishi. Yesu daima alitamani mapenzi ya Baba yake. Katika kutimiza mapenzi ya Baba, alitufunulia Roho Mtakatifu, ambapo tunajifunza kwake kujitoa sadaka kwa ajili yaw engine.
Injili ya leo kutoka katika Injili ya Yohane. Watu wanamtafuta Yesu. Watu wanataka kumfuata Yesu. Wanachohitaji zaidi sio kile Yesu anachosema ila kile ambacho Yesu anawapa katika maisha. Yesu anawakumbusha kwamba ingawaje anauwezo wakuwapa mkate katika maisha haya, kitu ambacho wanapaswa kutazama zaidi ni maisha ya uzima wa milele. Ingawaje Injili inaishia hapo lakini tunajua kwamba watu waliishia kumkataa Yesu kwasababu walihitaji miujiza mingi na pengine mikate katika maisha haya-na sio hali ya kujitoa kwa ajili ya Ufalme wa Mungu na kujitoa sadaka kwa ajili ya chakula cha wengine. Ninahitaji nini? Tunahitaji nini? Je, tupo tayari kufanywa upya na Yesu na katika uelewa wa maandiko Matakatifu? Je tupo tayari kujitoa sadaka kwa ajili ya Mungu na jirani zetu?
Mungu ametutendea mengi mno, je, tunabaki tukilalamika na kuonesha kwamba hajafanya kitu? Leo tujikabidhi kwa Mungu hata tukiwa na matatizo makubwa namna gani yeye anauwezo wakutulisha katika jangwa kali namna gani la maisha yetu. Tumaini kwake linapaswa kuwa kubwa daima.
Maoni
Ingia utoe maoni