Jumapili, Agosti 11, 2024
Jumapili, Agosti 11, 2024,
Tafakari ya kila siku
Juma la 19 la mwaka wa Kanisa
1 Fal 19: 4-8
Zab 34: 1-8
Efe 4:30--5:2
Yn 6: 41-51
MIMI NDIO MKATE MKATE WENYE UZIMA
Ujumbe wa neno la Mungu leo unaongozwa na zaburi yetu ya wimbo wa katikati isemayo: onjeni na kuona jinsi bwana alivyo mwema. Yeye huwapigania wanyonge, wanyonge wakimlilia wanaokolewa kwenye shimo la uharibifu na nyuso zao kuwa na furaha na pia Mungu humtuma malaika wake kuwaokoa wale wanaomcha na kuwalinda na kuwapigania na kuwaonyesha wema wake.
Zaburi hii ndugu zangu ni ya Daudi na aliitumia kuonyesha jinsi Mungu alivyokuwa kawatuma malaika wake kumuokoa hasa kwa adui yule wake mkubwa yaani Sauli.
Lakini leo basi kwenye masomo yetu, tutasikia kwamba anayeokolewa namna hii ni nabii Elia. Yeye basi anakimbizwa na kumlilia Mungu na Mungu basi anamtuma malaika wake kumpigania. Nasi tuwe kama Elia, tumlilie Bwana katika unyonge wetu, tumwambie atume malaika wake waje wakatuokoe kama alivyoweza kumwokoa Elia Nabii.
Zaidi tutasikia tena Elia akionja wema wa Bwana tena kwa kulishwa mkate na malaika na kwa njia ya mkate huu kupata nguvu ya kusonga mbele. Sisi nasi tunaonyeshwa na kuonjeshwa wema wa Bwana kila siku kwa kualikwa kuushiriki mkate mtakatifu ambao ni Yesu mwenyewe ambaye anayejitoa katika maumbo ya mkate na divai akitualika tumshiriki kwenye maumbo haya.
Kwenye somo la kwanza, tunakutana na habari za nabii Elia. Yeye amechoka kabisa, anakimbizwa na Jezebeli aliyekuwa mke wa mfalme Ahabu wa Israeli. Anatafutwa ili auawe. Sasa, yeye anakimbia, anakimbilia jangwani na jangwani anafika sehemu yenye kichaka akiwa na njaa kali. Anapofika hapa, anakata tamaa, anaona kazi anayofanya sio kitu, haijaleta matunda yoyote. Anaamua kumuomba Mungu amuue. Lakini Bwana anakuja kwake na kumwonyesha wema wake na kumpatia matumaini makubwa.
Cha kwanza anamtumia malaika anayekuja kumlinda, halafu malaika huyu anamletea chakula safi kabisa na kumwambia ale, halafu tena anamuongezea chakula na kumwambia kwamba kile chakula ni cha muhimu sana na kitampatia nguvu ya kusafiri kwani ana safari ndefu. Na kweli kile chakula kinakuwa na nguvu ya ajabu kwani kwa njia ya chakula hiki, anaweza kutembea kwa muda wa siku arobaini usiku na mchana, alitembea maili 300 hadi kufika mlima horebu na hapa basi aliweza kukutana na Bwana aliyempatia matumaini na kumweleza ni nini cha kufanya maishani mwake. Kweli ndugu zangu, huyu Elia aliuonja wema wa Bwana kwani kile chakula alichopewa na huyu malaika, kilikuwa na nguvu ya ajabu. Hiki hakikuwa chakula cha kawaida kabisa. Kingekuwa ni chakula tu kama makande au chips tunazokula hapa, kamwe kisingweza kumfikisha.
Halafu cha pili ni kwamba akiwa njiani, alipatiwa ulinzi wa ajabu kabisa na kuweza kufika hadi kukutana na Bwana bila shida yoyote.
Ndugu zangu, hata sisi tunachochakula kinachofanania na hiki alichopewa Elia na Yesu amekielezea kwa undani kwenye injili yetu ya leo.
Yesu anasema kwamba yeye ndiye mkate ulioshuka kutoka mbinguni na atakayeula mkate huu, yaani utampatia nguvu sio za kutembea kwa siku arobaini kama zile za Elia bali nguvu za kuishi milele. Kwa waisraeli, wakisikia mkate kutoka mbinguni, walichojua wao ni ile mana. Lakini yeye anasema kwamba yeye ni zaidi ya ile mana. Mana haikuwa na uwezo wa kuwafanya watu waishi milele, haikuwa na uwezo wa kutoa neema, nguvu za kiroho zimwezeshazo mwanadamu kupambana na magumu ndani ya huu ulimwengu. Mana ilitoa nguvu za kimwili tu. Na ukweli ni kwamba wale wote walioila ile mana kule jangwani, karibu wote hata hawakuweza kufika nchi ya ahadi. Kile kizazi cha mwanzo chote kilikufa kule jangwani. Hivyo, mana ilikuwa dhaifu sana.
Basi Yesu anasema kwamba mkate auotoa ni mwili wake ili wanadamu waule kwa ajili ya wokovu wa ulimwengu. Yesu amekamilisha hili katika ekaristi ndugu zangu. Yeye basi ameamua kujinyenyekeza na kuamua kukaa kwenye umbo dogo la mkate na divai kwa ajili ya yeye kutufikia kirahisi ili tuupate uzima. Hivyo, Ekaristi ni namna ambayo Mungu anatualika tuweze kuushiriki wema wake, tuuone wema huo na kuukubali na kuupokea.
Katika siku ya leo, naomba nizungumzie mambo yafuatayo kuhusu Ekaristi
Kwanza, Ekaristi ni Yesu mwenyewe; ndio ule mkate ulioshuka toka mbinguni ili kuupatia ulimwengu uzima. Ekaristi kweli ni wema wa Mungu umeonyeshwa kwa ulimwengu. Ina nguvu Zaidi ya kile chakula anachopewa Elia leo. Kile chakula kilikuwa ni cha malaika na kilimpatia nguvu za ajabu hadi akaweza kukutana na Bwana. Ndivyo ilivyo kwa Ekaristi. Nayo ina nguvu ya ajabu itakayotupatia nguvu za kuweza kukutana na Bwana ile siku ya mwisho. Hivyo, tukiamini chakula hiki, tukialike kitupatie ulimwengu uwezo mkubwa, kitupatie wanadamu nafasi ya kufika mbinguni, ndicho kitakachotuokoa jamani.
Mkate huu upo katika umbo la kawaida, una ladha ya kawaida na kuna watu wangalitaka labda uwe na sukari nyingi sana lakini ni kwamba ni mkate simple. Hivyo ni rahisi kuudharau. Lakini una nguvu za ajabu. Ni tofauti na ile mana. Mana haikuwa na nguvu za kuokoa lakini huu mkate unatoa neema, na kuokoa. Na hivyo ukizidisha mazoea nao hasa mabaya mwishowe tunaishia kutokuuona kana kwamba kuna chochote kipya ndani ya huo mkate. Hivyo, lazima tuzidishe adabu njema kwa huu mkate na tuupende kila wakati na siku zote.
Kingine ni kwamba kuna urahisi wa kukinai kirahisi, kukinai mkate huu na kuona kwamba ndani yake hakuna cha ziada. Waisraeli baada ya kupewa ile mana, mwanzoni waliifurahia lakini siku zilipopita, walianza kuikinai. Ndivyo ilivyo na kwetu sisi. Upo urahisi wa kuikinai Ekaristi, kuona kwamba haina jipya zaidi. Ukweli ni kwamba waisraeli walikuwa wakitamani kile chakula cha wamisri na kuona kilikuwa kitamu sana bila ya kujua kwamba kile kilikuwa chakula cha utumwani.
Na ndivyo na sisi, tunakuwa tayari kupendelea vitu kama pombe, au nyama kuliko ekaristi. Mtu akikuambia basi usishiriki ekaristi, hatusikitiki na kuona huruma kama mtu aliyeambiwa labda asinywe pombe au nyama kwa sababu ya kisukari. Pale tunalia, tunahuzunika, lakini ukisikia mtu kafungiwa ekaristi, hatuhuzuniki sana. Ndivyo ilivyokuwa. Mana ilikuwa ni chakula cha watu huru lakini ilionekana kuwa ya hadhi ya chini kuliko kile chakula cha misri-licha ya kwamba kilikuwa ni chakula cha utumwani. Ndivyo ilivyo basi ndugu zangu. Ni lazima tutambue hatari iliyoko kwenye kukinai ekaristi kwa haraka.
Tatu ni kwamba ukiona mtu ameaanza kuikataa ekaristi kwa makusudi tu, jua basi ndio mwanzo wake wa kuanguka. Muda sio mrefu utamuona ameishiwa nguvu na ukatoliki wake atauacha tu. Hii ni kwa sababu ekaristi ndicho kiini cha maisha ya ukatoliki wote. Bila ekaristi, hakuna ukatoliki. Ukishaiacha, basi ndio umekwisha. Hata wale wanaohama makanisa, cha kwanza wataanza kwa kutokushiriki ekaristi. Maadui wote wa kanisa huanza kwa kuipinga ekaristi. Basi sisi tunaokaaga mwaka hadi mwaka bila kupokea tutafute namna ya kubadilika ili tusije tukamuacha Yesu wetu.
Nne, Yesu basi amekubali kukaa kwenye huu mkate na hivyo lazima atengewe muda aabudiwe. Ni jambo lisiloeleweka ati tunajidai kusema ati Yesu kakubali kukaa kwetu na sisi tukakataa kumwambudu. Lazima aabudiwe, tuje kuabudu, asikae kanisani mwenyewe.
Tano, tunashindwa kuiona nguvu ya ekaristi maishani mwetu kwa sababu ya uchoyo. Kweli wanadamu ni wachoyo. Tuna masaa 24 kwa siku moja lakini kutoa hata dakika kumi kwa ajili ya Mungu hatutoagi. Nakueleza: kama Mungu angepata dakika kumi toka kwa kila mwanadamu kwa ajli ya sala, nakueleza tungekuwa mbali sana. Lakini tuko nyuma kwa sababu ya uchoyo wetu, hatumpatii Mungu nafasi. Nafasi ati ipo kwenye whatsap, vijiwe vya kahawa, na tv na vimada vyetu. Jamani, tubadilike, Ekaristi ni sadaka, ya Yesu amejitoa kwa ajili yetu. Nasi basi tujitoe kwa ajili ya wenzetu. Tusiache kutoa sadaka kwa ajili ya hawa wenzetu, kweli hili ni jambo la muhimu sana. Tusikae bila sadaka, mkristo ni mtu wa sadaka.
Ekaristi huliunganisha kanisa. Sote tunaalikwa kushiriki mkate mmoja. Hata maskini, tajiri sote tunashiriki mkate mmoja. Hakuna anayepata zaidi. Anayotoa kanisani hula mkate ule ule na neema ile ile hupokea.
Nasi tujifunze kukataza ubaguzi kwenye sherehe zetu. Suala la kuponi litoke. Unakuta ati kwenye sherehe moja kuna kuponi mbalimbali. Yule mwenye kutoa mchango mkubwa anaambiwa anywe bia kuanzia sita. Wa kutoa mchango kidogo wanakunywa bia chache zaidi. Tuepukane na tabia kama hizi ndugu zangu. Zitatuangusha sana.
Somo la pili Paulo anatueleza kwamba sisi ni wanachama pamoja na Kristo. Hivyo lazima tumwige. Na zaidi sisi tunaoshiriki kwenye mkate na mwili wake mmoja ni lazima tuwe watu wa kumuiga. Lazima tuondoe chuki, tuzidishe upendo, na hii itakuwa sadaka yetu bora kama Kristo mwenyewe alivyojitoa kwa ajili yetu. Amina.
Maoni
Ingia utoe maoni