Jumanne, Juni 04, 2024
Jumanne, Juni 4, 2024,
Juma la 9 la Mwaka
2 Pet 3: 12-15,17-18
Zab 90:2-4,10,14,16; ;
Mk 12: 13-17.
KUTEMBEA KATIKATI YA MITEGO!
Mafarisayo na Maherodi walijaribu kumtega Yesu katika maongezi yake. Walijaribu kutumia akili yao ili kumfanya Yesu aongee maneno ya kumpinga Kaisari na hivyo kupata kisingizio cha ugomvi na utawala wa Kirumi. Lakini chakushangaza walichokuwa wakisema kuhusu Yesu kilikuwa cha kweli na ilikuwa fadhila kubwa.
Walisema mambo mawili ambayo yalionesha unyenyekevu wa Yesu na uaminifu wake: “twajua ya kuwa wewe u mtu wa kweli,” na “wala hujali cheo cha mtu; kwa maana hutazami sura za watu; lakini katika kweli waifundisha njia ya Mungu”. Yesu haingii katika mtego wao na anafanya kwa hekima kubwa na kumalizana nao.
Tukitafakari juu ya fadhila hizi mbili, tunatambua kuwa maisha yetu ni mara chache sana yanakuwa namna hiyo. Kwanza kabisa, sisi tuna hangaika sana na maneno ya wengine. Ni vizuri kusikiliza wengine na kuwasiliana nao katika hali ya utambuzi. Mawazo ya wengine yanaweza kuwa chanzo cha kugeukia maisha mazuri. Lakini wakati mwingine tunaruhusu wengine watupeleke kwenye dhambi kwasababu ya hofu na woga. Wakati mwingine mawazo mabaya na ushauri mbaya unaongoza maisha yetu. Yesu hakuingia katika mawazo mabaya ya wengine wala hakuruhusu kupelekwa na kutenda kunyume.
Pili, Yesu hakuruhusu “cheo” cha mtu kumpelekesha. Cheo cha mtu wala madaraka havi mfanyi mtu kuwa mkweli zaidi kuliko wengine. Kilicho cha muhimu ni uaminifu na ukweli wa kila mtu. Yesu alizitenda fadhila hizi kiaminifu.
Tutafakari pia sisi kama maneno haya yanaweza kusemwa yakitulenga sisi. Tukazane kuishi maisha ya unyenyenyekevu na kweli na hivyo tutavuka vikwazo na mitego iliyotegwa katika njia yetu ya maisha.
Sala:
Bwana, ninataka kuwa mtu mwaminifu. Ninataka kusikiliza mawaidha mazuri ya wengine lakini sio mawazo yakunipeleka kwenye dhambi. Nisaidie niweze kukutafuta wewe na ukweli wako katika kila kitu. Yesu, nakuamini wewe.
Amina.
Maoni
Ingia utoe maoni