Jumatatu, Aprili 22, 2024
Jumatatu, Aprili, 22, 2024
Juma la 4 la Pasaka
Mdo 11:1-18;
Zab 42:2-3,43:3-4 (K. 42:3);
Yn 10:11-18.
KUMFUATA MCHUNGAJI MWEMA!
Sehemu ya Injili ya mchungaji mwema inatupa mambo manne kuhusu Yesu. Kwanza kabisa Yesu kwa kuwa Neno wa Mungu mwenyewe, sio tu mchungaji bali yeye mwenyewe ni chakula-malisho ya kweli ambaye hutoa uzima kwa wingi. Anatupa uzima kwa kujitoa mwenyewe, kwani yeye ni uzima (Yn 1: 4). Pili, huyu Mchungaji mwema anatoa maisha yake kwa ajili ya kondoo wake (Yn 10: 11). Msalaba upo katikati ya maelezo ya Mchungaji mwema. Na unaoneshwa sio kama kitendo cha vita kinacho mshtukiza Yesu bila kujua na kumshambulia kutoka nje, bali ni kama zawadi huru kutoka kwake. “Nayatoa maisha yangu, ili niya twae tena. Hakuna awezaye kuyatwaa kutoka kwangu, bali ninayatoa kwa hiari yangu mwenyewe”.
Tatu, kondoo ni wake katika hali ya kufahamiana na mchungaji, na hali hii ya kufahamiana ni hali ya kukubali kutoka ndani. Ina maanisha hali ya kuwa wake katika hali ya ndani ambayo ni zaidi ya ile hali ya kuwa na vitu vya kawaida. Na mwisho Kabisa, Mungu ndiye mchungaji ambaye anawaunganisha tena Waisraeli waliogawanyika na kutawanyika na kuwafanya watu wamoja kwani sio mataifa mawili tena (Ez 37: 15-17, 21). Hili ndilo la Muhimu kwa wayahudi walipo mpinga Petro kwa kutembelea nyumba ya Kornelio kama inavyo oneshwa katika somo la kwanza.
Sisi nasi tunaalikwa kwenye utume sisi kama wachungaji wa Kristo tunapaswa kuziokoa roho kwa ajili ya Mungu kwa kulijenga na kulifanya kanisa la Mungu kuwa moja. Je, tupo tayari kuchukua jukumu hili na kukumbana na changamoto?
Yesu, Mchungaji Mwema, anatuita sisi "kondoo," kwamba sisi ni dhaifu na wanyonge. Bila yeye, hatuwezi kufanya kitu (Yn 15: 5). Mchungaji Mwema atosha, Yeye atawaongoza kwenye malisho ya majani mabichi (Zab 23: 2). Jambo pekee linalohitajika kutoka kwetu sisi kondoo, ni kusikia sauti yake daima na kuifuata. Sisi sote kama kondoo lazima tuikimbie sauti ya yule muovu (Shetani). Sauti ya Yesu inahitaji kujitoa kweli, kujikana nafsi na kuacha yote, kubeba misalaba yetu, tofauti na sauti nyingine za ulimwengu huu zinazo onekana kuwa tamu na rahisi kuzifuata lakini mwisho wake kuangamia milele. Kusikiliza sauti ya Yesu ni katika Sala na Tafakari juu ya Biblia, kuwasikiliza ndugu zetu katika hali mbali mbali na mengine yanayo tujenga kiroho. Kusikiliza huja kwa Neno la Kristo (Rum 10:17). Tumuombe Mungu atusaidie kuisikia sauti ya Yesu ndani ya sauti nyingi za ulimwengu huu.
Sala:
Bwana, nisaidie niweze kutambua na kufuata sauti yako ya upole siku zote za maisha yangu. Ninaomba sauti hiyo iweze kushinda sauti zote zinazo shindana na utulivu wangu kwako. Ninakuchagua wewe, Bwana mpendwa kama mchungaji wa kuniongoza. Yesu nakuamini wewe.
Amina.
Maoni
Ingia utoe maoni