Ijumaa. 03 Mei. 2024

Tafakari

Jumatano, Aprili 17, 2024

Jumatano, Aprili 17, 2024
Juma la 3 la Pasaka


Mdo 8:1-8;
Zab 66:1-7 (K. 1);
Yn 6:35-40.


JE, MATESO YANA KUVUNJA MOYO?


Kifo cha Stefano ni mwanzo wa mateso kwa jumuiya ya Kikristo. Lakini mbali na kujaribu kuupunguza ujasiri wa wanafunzi wa Yesu, kifo cha Stefano kinatia chachu na nguvu ya kuendelea kuhubiri. Kutawanyika kwa Wakristo kulikuwa na maana ya kuhubiri neno la Mungu sehemu mbali mbali na sio kukimbia kwa sababu ya hofu.

Injili ya leo inaendelea kufundisha jinsi gani Ekaristi itafanya kazi, ina maana gani, na kuna umuhimu gani kwa mpokeaji wa sakramenti kama anataka imsaidie. “hakuna hata mmoja atakaye kuja kwangu atakayeona njaa au kuona kiu” Yesu alisema. Lakini watu walikuwa na ugumu wakumuamini Yesu analalamika kwa upole “Ingawaje mmeniona hamtaki kuamini”. Sio kwamba walikuwa wamemuona tu bali walikuwa wameshaona mambo wakuu aliokuwa ametenda, kutembea juu ya maji, kuongeza mikate na samaki, kuwaponya wagonjwa na kufufua wafu. Lakini Yesu hakatishwi tamaa na mtu. Anawahakikishia; Yote alionipa Baba yatakuja kwangu, hakuna ambaye atakuja kwangu nimkatae.

Maneno ya Yesu ni muhimu kwani yanatuhakikishia sisi kwamba ni wakuaminika. Ni kweli kwamba tunaweza kuja kwake na kumuamini yeye, kumkabidhi mioyo yetu, yeye atatutendea vyema, kutujali na kututunza. Yesu anauwezo wakutujali zaidi ya hata sisi tunavyojijali wenyewe. Tunapokumbwa na dhoruba tusikate tamaa na kuogopeshwa na majaribu tukashindwa kumwamini.

Mt. Rosemaría Escriva anasema, "dhoruba ya mateso ni nzuri. Ina hasara gani? Kwani jambo ambalo limekwisha kupotezwa haliwezi kupotezwa tena. Mti ukiwa na mizizi iliyojishika chini sana, hakuna upepo uwezao kuungoa mti wa Kanisa, labda tu matawi yake makavu yataanguka”. Basi leo tuangalie maisha yetu kama tu matawi mabichi yaliojishika na kanisa au makavu yategemeayo kuanguka kutoka mtini muda wowote kutokana na upepo!

Sala:
Ee Bwana, Utusaidie kuishuhudia Injili na kukubali mateso yoyote yatokanayo na shughuli hiyo.
Amina.

Maoni


Ingia utoe maoni