Jumamosi, Aprili 13, 2024
Jumamosi, Aprili 13, 2024
Juma la 2 la Pasaka
Mdo 6:1-7
Zab 33:1-2,4-5,18-19,22
Yn 6:16-21
KUTULIZA DHORUBA ZETU!
Katika Injili ya leo Yesu anatembea juu ya maji na anawaambia mitume wake “Jipeni moyo ni mimi. Msiogope”. Injili ya leo inatutia nguvu na kutuambia tusiogope tunapo kutana na dhoruba na mawimbi ya maisha. Hatupaswi kuogopa tupo na Yesu.
Kuwa katikati ya bahari wakati wa giza inaogopesha sana. Kila upande unaoneakana kuwa sawa na huwezi kuona nchi kavu. Tunajisikia kama vile hatujazungukwa na kitu. Mitume wametoka, na wapo baharini wakati wa giza. Watakuwa wamejisikia kama vile wamepotea katikati na hamna kitu. Lakini katikati ya hali hii, Yesu anawajia akiwa anatembea juu ya maji. Na kuwaambia “jipeni moyo ni mimi. Msiogope”.
Tunaona katika maisha haya ya mitume mfanano wa maisha ya kila siku ya wengi wetu. Wengi twaweza kujisikia kwamba hatuja zungukwa na mtu na hatuna msaidizi, tupo wenyewe na tunapotea. Injili inatufunulia kwamba Yesu anakuja kwetu haijalishi tupo sehemu ghani au tumejikuta katika hali ghani. Yeye hatusubiri sisi tuende kumtafuta, bali anakuja na kuingia katika maisha yetu, alimradi tunamtambua na kumkaribisha.
Pengine maisha yetu yamejazwa na kazi nyingi, lakini tunajisikia wa pweke. Pengine maisha yetu ni yale ambayo hatuna watu wengi wanaotupenda na tunajikuta tupo wenyewe na kutengwa. Au pengine tunajifanya kuvaa sura ya kuonesha kwamba nina kila kitu lakini ndani mwangu nina hangaika. Katika hali yeyote ile ambayo unaweza kujikuta Yesu anataka kuja kwetu na kutufariji. Msikilize akisema “jipe moyo ni mimi. Usiogope”. Hali katika maisha inaweza kuwa inatisha na kutupa mashaka na woga. Lakini tutakapo ruhusu kumwelekea Yesu, hofu inapotea. Tutambua ndani mwetu kwamba Yesu yupo na mambo yataenda vizuri kwasababu yeye anaongoza kila kitu. Mwache aingie katika mashua ya moyo wako na umwache aongoze. Anakuja kwako na anasubiri jibu lako.
Sala:
Bwana, ni mara nyingi nimeshindwa kushuhudia uwepo wako wa Kimungu katika maisha yangu. Ni mara nyingi nimeshindwa kukuona ukija katika maisha yangu. Nisaidie niweze kutambua kuwa kila mara upo. Niweke huru kutoka katika hali mbali mbali za maisha, na nipe ujasiri wa kukukaribisha wewe katika maisha yangu. Yesu nakuamini wewe.
Amina.
Maoni
Ingia utoe maoni