Jumapili. 12 Mei. 2024

Tafakari

Alhamisi, Februari 23, 2017

Alhamisi, Februari 23, 2017,
Juma la 7 la Mwaka wa Kanisa

Kumbukumbu ya Mt. Policarpo(Askofu na Shahidi)

YbS 5: 1-8;
Zab 1: 1-4, 6;
Mk 9: 41-50.


KILA MKRISTO NI SHAHIDI!

Kila Mkristo anashiriki kazi tatu za Kristo, pamoja na kristo kila Mkristo anaitwa kushiriki unabii, ukuhani na ufalme. Leo Yesu anatukumbusha kuhusu kazi yetu ya Kinabii. Kuwa na nabii ni kutoa ushuhuda ulimwenguni. Tunakuwa manabii tunavyo wajali maskini, tunapowasaidia wanaoteseka, wagonjwa, tunaposimamia haki na kweli. Kwa kufanya hivyo tunakuwa wafuasi halisi wa Kristo.

Katika Injili Yesu anatuonya sisi “Chumvi ni nzuri, lakini chumvi ikipoteza ladha itakolezwa na nini tena?” (Mk 9:50). Wakati mwingine tumekuwa Wakristo tulio poteza ladha. Tumeshindwa kutoa maisha ya ushuhuda. Tunaogopa ukweli na hivyo tunawaongoza wengine kukwepa ukweli. Maisha yetu yanayopaswa kuwa maisha ya kinabii kila wakati, mara nyingi yamekuwa kihoja mbele za watu. Sifa za nabii wa kweli hasemi jambo kwasababu ya kufurahisha watu au kujitukuza mwenyewe au kumtukuza mtu, sifa za nabii wa kweli anasema jambo kwasababu ni kweli, hata kama inamgarimu. Tunaitwa kuwa walinzi wa wale wanyonge wa Mungu-wale walio wadogo kwa miaka au kwa hali zao za kiuchumi na hata wale walio wadogo katika maisha ya kiroho.

Kwa kuongeza chumvi kwenye chakula inaleta ladha. Haibadilishi chakula sana kuwa kitu kingine, bali kina leta ladha kwa chakula kilichopo. Chumvi ina hali pia ya kuhifadhi chakula ili kisishambuliwe na bakteria. Kazi hizi mbili za kuleta ladha na kuhifadhi ni vizuri kuziangalia. Tulete ladha katika maisha ya watu kwa kumfanya Kristo atawale katika maisha yao na tuhifadhi hali hii ya utakatifu kwa kuishi kile anacho tufundisha Yesu. Kwa kutiwa chumvi kwa moto-maana yake tunatakaswa na Mungu. Moto unatakasa na kufanya safi. Moto ulitumika kusafisha vyombo, kutakasa dhahabu na ulitumika pia kufua vyuma na kutengeneza vitu au picha mtu anayotaka. Sisi nasi pia. Tunapaswa kutakaswa na moto wa Mungu katika kila hali. Dhambi inapaswa kuondolewa na kutakaswa kwa moto wa Mungu, ili tuweze kutengenezwa na kuwa katika picha ya Mungu.

Kwahiyo tukubali wito wetu leo. Tuwe manabii wa kweli na kusali kwa Bwana ambaye anasikiliza matatizo ya wanyonge, ili aweze kutubariki tuweze kupata nguvu ya kuwasaidia wale wote walio maskini na wasio jiweza. Tusijiamini wenyewe tu bali tuwe wanyenyekevu na maskini wa roho ili tuweze kuurithi ufalme wa Mbinguni. Tuombe neema ya Mungu ili tuweze kutumia zawadi alizotupa, mikono, macho, akili na utashi ili kufanya kazi na kuwasaidia wadogo.

Sala: Bwana Yesu tunayaweka maisha yetu katika mikono yako. Ninakuomba Bwana unitakase na dhambi zangu zote. Ninakuomba mateso na msalaba katika maisha yangu yaweze kuwa neema ya kweli ambayo kwayo utanifanya nikuwe katika uvumilivu na fadhila zote. Najitoa kwako Bwana, niweze kuwa shahidi na nabii wa ulimwengu. Yesu, nakuamini wewe. Amina

Maoni


Ingia utoe maoni