Jumatatu. 06 Mei. 2024

Tafakari

Ijumaa, Machi 22, 2024

Ijumaa, Machi 22, 2024
Juma la 5 la Kwaresima

Yer 20: 10-13;
Zab 17: 2-7;
Yn 10: 31-42.


IMANI ILIYO JARIBIWA

Lirtujia ya leo inampa changamoto kila mfuasi wa Kristo kuangalia uwiano wa maneno yake na matendo yake kama yanaendana. Katika masomo ya leo tunasikia nabii Yeremia akiwa katikati ya matatizo na Yesu akiwa katikati ya Wayahudi wakijianda kutaka kumpiga mawe. Nabii Yeremia aliongea kwa jina la Mungu na kwa niaba ya Mungu na sio kwa ajili yake mwenyewe. Maneno yake hayakupokelewa na wasikilizaji wake. Hili lilileta matatizo kwa Yeremia. Na kwa upande wa Yesu pia, maneno yake hawakuyapokea pia.

Tukiwa tunakaribia juma kuu, na hasa ijumaa kuu, tunaona kwamba chuki inakuwa sana juu ya Yesu. Kumchukia Yesu na kufikia katika kitendo cha kutaka kumuua kwa mawe ni kitendo cha kutokufikiri. Taratibu taratibu wale waliokuwa wanamchukia Yesu chuki yao ilikuwa hata kufikia kilele cha siku ambayo Yesu anayatoa maisha yake kwa ajili yetu na kwa mapenzi makubwa kukabili kifo. Tukikutana na mabaya na uonevu tunapaswa kuwa kama Yesu alivyofanya. Tunapaswa tuyakabili bila woga. Aliyakabili katika ukweli na hakukubali uongo.
Ukweli wa mambo ni kwamba, kadiri tunavyosogea karibu zaidi na Mungu, ndivyo tunavyo shambuliwa zaidi na kuchukiwa zaidi. Kitu muhimu katika kuelekea utakatifu ni kwamba katikati ya madhulimu, mateso, magumu, na uchungu, tunapaswa kusimamia ukweli. Mara nyingi inashawishi kufikiria kwamba huenda tumefanya kitu kibaya wakati mambo hayaendi. Kitu kimoja ambacho Mungu anataka tutambue katika misalaba yetu, ni kuitakasa Imani yetu na kusimamia neno lake na ukweli. Huu ndio muda ulio muhimu kuliko muda mwingine wowote, ambapo tunatakiwa kusimama imara. Ni rahisi kusema tunamtumainia Mungu wakati maisha yakiwa yanaenda vizuri na inakuwa vigumu kumwamini wakati misalaba yetu inakuwa mizito. Kabili hofu yako na muombe Mungu akubadilishe katikati ya hayo matatizo. Ukifanya hivyo, utagundua kwamba mahangaiko makubwa katika maisha yanabadilika kuwa Baraka kubwa.

Sala:
Bwana, tunapokaribia kumbukumbu ya mateso na kifo chako, nisaidie niunganishe matatizo yangu na yako. Nisaidie kuona katika mahangaiko yangu ya kila siku, uwepo wako na nguvu yako. Nisaidie niweze kuona mpango ulionao kwa changamoto hizo. Yesu, nakuamini wewe.
Amina.

Maoni


Ingia utoe maoni