Alhamisi. 02 Mei. 2024

Tafakari

Jumapili, Aprili 07, 2024

Tafakari ya Pasaka
Aprili 7, 2024
------------------------------------------------
JUMAPILI, DOMINIKA YA 2 YA PASAKA, JUMAPILI YA HURUMA YA MUNGU.

Somo la 1: Mdo 4: 32-35 Lina beba maelezo ya jumuiya ya kwanza ya Wakristo walivyo shirikishana vitu kwa pamoja, na kuwatunza wahitaji.

Wimbo wa Katikati. Zab 118: 2-4,15-18,22-24 Mungu ni mwema na upendo wake na huruma yake haina mwisho.

Somo la 2: 1 Yn 5: 1-6 Yohane anatuambia kwamba tunaweza kuushinda ulimwengu kwa Imani kwa Yesu, ambayo inatufanya sisi watoto wa Mungu.

Injili: Yn 20: 19-31 Yesu anawatokea wafuasi wake kwa mara ya kwanza, na tunaona majibu ya Tomaso, ambapo kutokuamini kwake kulimpelekea kuja kusema “BWANA WANGU NA MUNGU WANGU”.

------------------------------------------------

HURUMA YA MUNGU: MSAMAHA WA DHAMBI

Leo ni siku ya nane naya mwisho katika oktava ya Pasaka. Na siku ya leo tunaadhimisha Jumapili ya huruma ya Mungu. Ni siku ambayo geti la huruma ya Mungu hufunguliwa kwetu na Mungu kutukirimu huruma yake hata zaidi ya jinsi ambavyo tunaweza kudhani au kutumaini. Leo tunakumbushwa juu ya huruma ya Mungu isiyo na mipaka. Injili ya leo inaonesha mamlaka ya Yesu yakuwapa mitume Roho Mtakatifu ambaye ndiye atakaye wasamehe watu dhambi zao. Yesu Mfufuka anakuwa hai tena kati ya wafuasi wake. Anafungua miyo yao na kuitia shauku na kuwafungulia maandiko, na kuumega mkate. Anafungua macho yao na kujidhihirisha kwao.

Sehemu ya kwanza katika Injili Yesu anawahidia Roho Mtakatifu wafuasi wake. Kwa njia hiyo anawapa mamlaka yakuangusha uovu wote na nguvu za muovu. Na sehemu ya pili inaonesha sehemu maarufu ya Tomasi yakutokuamini. Ingawaje inaonekana kuwa katika methali hivi. Tomasi anaonekana kutokutenda chochote kibaya, alitaka tu aone kile kitu ambacho wengine wameona. Injili ya Marko inasema kwamba Yesu aliwatokea wale kumi na mmoja na kuwaonya juu ya ugumu wa mioyo yao, kwasababu hawakuamini kwamba amefufuka” (Mk 16:14). Katika Injili ya Luka Yesu mfufuka anaongea na mioyo ya mitume ambayo ina wasi wasi “kwanini mna wasi wasi mioyoni mwenu?” (Lk 24:38). Katika sehemu ya mwisho ya Injili ya Mathayo inasema pia wakati Yesu alivyo watokea mitume katika mlima wa Galilaya, wenigne walikuwa na wasi wasi (Mt 28:17). Kwahiyo wote pia walikuwa na wasiwasi, sio tu maskini Tomasi.

Yohane Mwinjili anawakilisha habari hii sio kwamba anataka Tomasi aonekane mbaya au kumuweka mtume katika hali mbaya. Alitaka kusisitiza juu ya swali la jumuiya yake ya Kikristo ambalo daima walisisitiza na kuuliza. Iliwawia vigumu sana kuamini, wakajikuta katika msongo wa mawazo yenye mashaka mengi, walitaka kuona na ikiwezekana washike na kuhakikisha ni kweli Bwana amefufuka kweli. Walishangaza: je hata sisi hatuwezi kuwa kama wao? Haya ni maswali ambayo sisi wenyewe tunauliza kila wakati. Je, inawezekana na sisi tuweze kushuhudia Bwana Mfufuka? Je, kuna chochote cha kuonesha kwamba yuu mzima? Sasa inakuwaje hata atutokei ? Haya ni maswali ambayo sisi tunauliza siku hizi. Yohane anataka kumchukua Tomasi kama sehemu ya kila mfuasi anayepata shida katika kumwamini Yesu. Yohane anataka kuwafundisha waumini wa jumuiya ya kwanza na sisi kwamba maisha ya Yesu mfufuka yanaenda zaidi ya fahamu zetu, maisha ambayo huwezi kuyashika, kuyanusa, wala kuyaona. Yanaweza kupatikana tu kwa Imani. Mtu hawezi kuwa na Imani kwenye kitu ambacho kinaonekana. Kama mmoja anataka kuona, kupata jibu, kugusa lazima aikatae Imani. Lakini kwa Yesu, wana heri ambao hawajaona lakini wanaamini. Wana heri kwasababu Imani yao ni ya kweli na haina mashaka. Ambaye anaona anauhakika na ushahidi, ana nyenzo zisizopingika. Sasa inakuwaje kwa ambaye hajakutana na Yesu mfufuka? Kama Tomasi atahitaji kuona na ushahidi ili aweze kuamini, lakini ni wazi kwamba hatapa kamwe ushahidi.

“Hakuna hata mmoja aliyetengwa na huruma ya Mungu na kanisa linawakaribisha wote bila kumkataa yeyote. Milango yake daima ipo wazi, ili wale wote wanaoguswa na neema ya Mungu waweze kuja kusamehewa. Hata Dhambi ikiwa kubwa vipi, ndivyo kanisa linavyo ongeza upendo wakukupenda na kukuribisha yule anayetubu…” . Maneno haya aliyasema Baba Mtakatifu Fransisko wakati akitangaza mwaka wa huruma ya Mungu (2016)

Alirudia kwakusema “Mungu daima hachoki kutusamehe sisi, bali sisi wanadamu tunachoka kumuomba msamaha na kutafuta huruma yake. Yesu ambaye ametuambia tuwasamehe ndugu zetu saba mara sabini, ametupatia sisi mfano. Mfano ambao daima unatupatia tena sisi furaha yetu, anatufanya sisi tunyanyue tena vichwa vyetu na kuanza maisha mengine. Kwahiyo tusikimbie kutoka katika ufufuko wa Yesu, wala tusikate tamaa, hata lije jambo la namna gani. Tunaomba chochote kisitutie nguvu isipokuwa ufufuko wa Yesu mwenyewe, ambao unatupatia nguvu daima” (FURAHA YA INJILI, 3)

”Jumapili ya huruma ya Mungu imekuwa ikiadhimishwa tangu siku nyingi kama ibaada binafsi. Lakini mwaka 2000, Baba Mtakatifu, Mt. Paulo wa II, ambaye kwakweli katika hali ya kawaida alionesha mfano mzuri wa huruma ya Mungu, aliiweka Jumapili hii ya huruma ya Mungu wakati alipo mtangaza sister Faustina kuwa Mtakatifu. Ambaye alipata Baraka ya kushuhudia huruma ya Mungu na kuandika katika kitabu chake cha kumbukumbu ambacho alikiita huruma ya Mungu. Alikuwa akiandika kila siku ya nane baada ya Pasaka, undani wa huruma umefunguliwa. Ninamwaga huruma kama bahari kwa roho zote zile ambazo zinahitaji huruma yangu. Roho ambayo itaenda katika kitubio na kupokea Yesu wa Ekarisi (Komunyo) itapokea msamaha kamili na maondoleo ya adhabu. Siku hiyo milango yote ya huruma ya Mungu hufunguliwa kama bahari. Msikubali roho yoyote ile kuacha kuja kwangu, hata kama dhambi zake ni nyekundu kiasi ghani. Huruma yangu ni kubwa kiasi kwamba hata roho ya mwanadamu hata malaika hainauwezo wakuishinda milele yote.”

Leo katika jumapili ya huruma ya Mungu, tunakumbushwa juu ya huruma ya Mungu iliyo kuu. Injili yenyewe inaonesha Yesu akitoa mamlaka kwa mitume wake kwa kuwapatia Roho Mtakatifu kuondolea watu dhambi. Tusiache kukimbilia huruma hii ya Mungu. Lakini sisi pia tunapaswa kuwa mawakala wa huruma ya Mungu. Mungu anatuonesha huruma nyingi, lakini sisi nasi anatuhitaji tuoneshe huruma hiyo kwa wengine. Tukisikia sauti ya Yesu mfufuka ambayo ipo kwa ndugu zetu kama Tomasi basi tumgeukie Mungu na kuwa naye daima. Tushirikishane mapaji yetu kama jumuiya ya kwanza ilivyofanya katika somo la kwanza. Kama vile Yesu alivyokuja katikati ya mitume, sisi nasi tukishirikishana mapaji yetu, Yesu naye atakuja kati yetu nasi tutamtambua kwakushirikishana zawadi /mkate anao tujalia kila siku.

Sala:
Bwana wa huruma, nisaidie leo niweze kuelewa nini maana ya huruma yako. Nisaidie niweze kuingia katika huruma yako ambayo unataka kunipatia mimi. Nikiwa napokea huruma yako mwenyewe, nisaidie na mimi pia niweze kuwa mjumbe wa huruma hiyo ili wote waweze kuona na kukutukuza wewe. Yesu, ninakutumaini wewe.
Amina

Maoni


Ingia utoe maoni