Jumapili, Machi 17, 2024
Machi 17, 2024
------------------------------------------------
JUMAPILI, DOMINIKA YA 5 YA KWARESIMA
Somo la 1: Yer 31:31-34 tunaelezwa juu ya “Agano Jipya” ambalo atafanya na watu wake, “Nitaweka sheria yangu ndani yao na kuiandika katika mioyo yao”.
Wimbo wa katikati: Zab 51: 3-4, 12-15 uniumbie moyo safi Ee Mungu.
Somo la 2: Ebr 5: 7-9 Somo linatoa asili na matokeo ya sadaka ya Yesu: ingawaje alikuwa Mwana, alijifunza utii kwa kuteseka.
Injili: Yn 12: 20-33 Yesu anatuonesha sheria ya uzima. Punje ya ngano ni lazima ianguke ardhini na kufa na kutoka huko huchipua na kutoa matunda. Aliongelea kuhusu nafsi yake mwenyewe
.
------------------------------------------------
KIFO CHA YESU KIMETUWEKA HURU KUTOKA KATIKA DHAMBI
Tupo karibu na sikukuu ya pasaka. Katika kipindi hichi cha kwaresima tulianza kwa kushiriki kile Yesu ambacho alikishiriki katika jangwa, uwezo wake wakupingana na vishawishi maisha yake yakujikatalia na kusali. Na mwishoni mwa kipindi hiki kanisa linataka sisi tukaze macho yetu juu ya mafumbo ya mateso na kifo. Na hili ni ushuhuda katika Injili, ambapo Yesu analinganisha nafsi yake na punje ya ngano ambayo hufa ardhini lakini huota na kuleta matunda. Yesu alikufa msalabani na kutoka huko ubinadamu wote ukapata uzima.
Katika somo la kwanza nabii Yeremia anatupatia ufunguo tuweze kuelewa liturjia ya leo, ambapo ni kutafakari juu ya tumaini jipya, nyakati za Kimasiha, ambapo Mungu ataanzisha agano jipya na watu wake. Ni agano jipya ambapo litafanya katika Mlima wa Kalvari ambapo litaondoa Agano la kwanza la mlimani Sinai. Kuvuka bahari ya shamu kuna fananishwa na kuvuka kutoka katika dhambi na kwenda katika uzima, kutoka utumwani na kwenda kwenye uhuru wa Wana wa Mungu. Yesu ambaye alikufa na kufufuka na kutoa matunda kama punje ya ngano ndiye tumaini letu leo. Mungu alimtoa Mwanae msalabani ili katika msalaba watu wote waweze kupata tumaini jipya.
Katika barua kwa Waebrania, kitendo cha Yesu kufa Msalabani kinaelezewa katika lugha kuu. Utii wa Yesu kwa Mungu ni mfano kwa wote, hata pale ambapo utii huu unatutaka sisi tupande katika kalvari na kuweka miguu yetu katika msalaba wa Kristo msulubiwa, sio katika kulilia mateso yake, bali tuweze kukumbatia mateso yake kwa kutazama na kupitia mateso yetu wenyewe.
Katika Injili ni kipindi cha Pasaka na watu wengi wamekuja kuhiji katika hekalu, hata baadhi ya Wagiriki. Wanamfuata Filipo na kumwomba ombi moja “tunataka kumuona Yesu” Filipo anaenda kwa Andrea na Andrea anaenda kwa Yesu na Yesu anaenda kwao. Na Yesu anawaambia hawa Wagiriki, hawa watu wa mataifa “Muda umefika kwa Mwana wa Mtu kutukuzwa” huu ndio muda wa ufunuo, muda wa msalaba, muda wa kujaribiwa. Katikati ya giza mwanga utaangaza. Ishara ya Yesu inayotumika kutambulisha lengo lake na hata lengo letu pia ni punje ya ngano ambayo inpaswa kufa ardhini na kuchipua. Isipo fanya hivyo itabaki tu kuwa punje ya ngano. Lakini kama ikifa na kuoteshwa katika udongo, na kupata maji kwa wakati wake, hali nzuri ya hewa, kwa kupaliliwa na hali yetu ya kibinadamu na kupata nguvu kutoka kwa Mungu, inazalisha matunda mengi. Yesu anaongelea kuhusu kifo chake mwenyewe. Mungu atasikia kilio chake na kupokea mapendo yake nasi kupata uzima.
Sisi nasi tunapaswa kuwa tayari kujitolea nafsi zetu ili kwa njia ya kujitolea maisha yetu, watu waweze kupata matunda na kuwa karibu Zaidi na Mungu. Hatupaswi kubaki hivi hivi tu, kwasababu ya ubinafsi wetu, tutakuwa ngano tu (punje moja tu) lakini tukiwa tayari kufa kwa kutoa maisha yetu kuwahudumia wengine, tutaleta Baraka nyingi sana na Mungu atatukuzwa nasi kupata utakatifu. Lazima pia tuwe tayari kufa katika vilema vyetu ili tufufukie katika utu mpya, tuangamize utu wa kale kwa kuuzika ardhini (kuacha dhambi zetu) na kuchipua kwa kuanza maisha bila dhambi.
Huruma ya Mungu inaingia kwa nguvu zote katika ubinadamu wetu, yule ambaye anaweza kuelewa nguvu ya huruma ya Mungu ilio ndani ya Kristo ni hasa katika mateso yake. Tukiwa tumesongwa na ulimwengu ambao unapoteza maana ya Mungu, na kujikita katika hali ya dhambi. Liturjia yetu leo inatukumbusha pia kuhusu mwaliko wetu wa kutambua huruma ya Mungu na kujingoa katika mizizi ya dhambi zetu. Na kujikita katika Imani ambayo inatupatia na kuthibitisha tumaini letu la ukombozi wetu, bila ya kutumia vibaya na kukufuru huruma ya Mungu. Ni muda wa wongofu, ni muda wakuanza maisha mapya katika Kristo, ambaye alipokea msalaba kama ishara kamili ya kutukomboa kutoka katika utumwa.
Sala:
Ee Mungu wa huruma, tunakuomba utusaidie tuweze kuishi katika mapendo yale ambayo yalimfanya mwanao afe kwa ajili yetu sisi.
Amina
Maoni
Ingia utoe maoni