Jumanne. 07 Mei. 2024

Tafakari

Alhamisi, Februari 29, 2024

Alhamisi, 29 Februari 2024
Juma la 2 la Kwaresima

Yer 17:5-10;
Zab 1:1-4, 6;
Lk 16:19-31


UPENDO WA MUNGU KWA MASKINI


Katika mfano wa Injili ya Leo tuna mtu mmoja ambaye ametajwa kwa jina, Lazaro. Mfano wa tajiri na Lazaro ni mfano ambao unabaki kuwa maarufu. Ni Lazaro tu anayetambulika katika hali hii? Kwanini Lazaro? Inawezekana ni kwasababu ya nafasi walio nayo maskini machoni pa Mungu. Mfano huu unatuonyesha ni kwa jinsi ghani Mungu anavyo chukizwa na ukosefu wa haki wa kuwafanya wana wake kuwa waombaji na kuwafanya kula makombo yanayotoka katika viti vya jirani zao walio na Mafanikio. Yesu anatuita kutoka moyoni mwake kwa ajili ya maskini. Anatuita tumuone kila mmoja hata wale maskini kabisa na walio katika hali ya mwisho kabisa, na kuwahudumia katika hali ya utu na heshima wanayostahili kama wanadamu wenzetu na watoto wa Mungu.

Kama ilikuwa ni kuchagua ungechagua nini? Kuwa tajiri na kuponda maisha kila siku, ukivaa mavazi ya kitani, kuwa na kila kitu unachopenda ulimwenguni? Au kuwa maskini uliye mwombaji, uliyefunika vidonda vyako, kuishi katika njia ya milango, ukihisi njaa?. Ni swali rahisi sana kujibu katika hali ya kawaida. Maisha ya utajiri na mafanikio yanavutia katika hali ya kwanza kabisa. Lakini swala ni kwamba hayapaswa kuchukuliwa katika hali ya kawaida, tunapaswa kuzama ndani kabisa na kulinganisha watu hawa wawili na matokeo ya maisha yao ya ndani ya roho yao ya milele.

Kwa maskini alivyokufa, “alichukuliwa na malaika katika kifua cha Abraham”. Na kwa tajiri, maandiko yanasema kwamba “alikufa na kuzikwa” na kwenda kwenye “ulimwengu mwingine ambapo alikuwa akiteseka” Sasa ni yupi unayependa kuchagua? Lengo la mfano huu ni rahisi kabisa, tukiwa hapa duniani tunapaswa kutubu, kuacha dhambi, kusikiliza Maandiko Matakatifu, kuamini na kuweka mioyo yetu kuelekea lengo letu la utajiri wa mbinguni.

Tajiri huyu angeweza kumuona Lazaro na kujali utu wake na thamani yake, yeye aliyekuwa amelala katika mlango wake, na kumuona kwa mapendo na huruma. Lakini hakufanya hivyo. Alikuwa amejikita sana juu ya nafsi yake. Dhambi zilimfunika macho akashindwa kumuona Lazaro. Tutafakari leo, kama unaona dhambi yeyote ndani yako inayo fanana na huyu tajiri katika maisha yako, ungama dhambi leo na kuziacha. Na kama umezoea kujikita katika ubinafsi, ukijiingiza katika anaasa za hali ya juu, kumbatia umaskini wa roho, na kujitahidi kuunganika na Mungu tu na baraka nyingi zinazokuja kwetu kwa kukumbatia yote yale aliyo yafunua kwetu.

Sala:
Bwana, niweke huru kutoka katika hali isio faa. Nisaidie mimi niweze kubaki katika heshima ya kuwaheshimu watu wote, na kujitoa mwenyewe kuwahudumia. Yesu, nakuamini wewe.
Amina.

Maoni


Ingia utoe maoni