Ijumaa. 23 Februari. 2024

Tafakari

Jumapili, Februari 11, 2024

Jumapili, Februari 11, 2024

DOMINIKA YA 6 YA MWAKA B WA KANISA

Law 13:1-2, 44-46
Zab 32:1-2.511
1 Kor 10:31—11:1
Mk 1:40-45


HATA KUONGEA KUHUSU UKOMA WA DHAMBIUkoma hata leo neno lenyewe linaonekana kuwa “kali” na kuogopesha kama linavyosikika. Siku hizi kuna dawa ya ukoma lakini daima kila mwaka yapo mengi yanayo ibuka-ingawaje idadi inapungua. Lakini wakati wa Wawalawi na kipindi cha Yesu dawa ilikuwa haijulikani bado. Kwasababu ya masababishi ya ugonjwa hayakujulikana, na hivyo mtu alikuwa akitengwa na jamii iliyokuwa na afya njema. Hakuna aliyependa kuwa mkoma ili atengwe na jamii yake na familia yake.

Katika masomo yetu ukoma ni ishara ya dhambi. Tunaweza hata kuongea kuhusu ukoma wa dhambi. Tunaweza kuelewa hili kwasababu dhambi inaonekana ikitendwa lakini kwanini dhambi za watu hazieleweki! Kuna kitu ambacho kimevunjika katika ubinadamu wetu, na kama Paulo anavyosema tunatenda dhambi hata pale mahali ambapo hatutaki kutenda dhambi.

Somo la kwanza leo linatoka katika kitabu cha Walawi, ambacho ni moja ya kitabu kati ya vitabu vya zamani vya Wayahudi, moja ya kitabu cha zamani katika Biblia yetu. Sura ya 12 na 15 inashughulika na magonjwa mbali mbali na kwanini magonjwa mengine yalihitaji watu watengwe kutoka katika jamii ya watu wengine, hakika ni ili wasiwaambukize wengine. Unaweza kuona kwamba mmoja alikuwa akipatwa na ugonjwa alibidi kujificha asije akaleta balaa kwenye jamii yake.

Somo la pili linatoka katika waraka wa kwanza wa mtume Paulo kwa Wakorintho. Somo kubwa kutoka katika somo hili nikwamba tunapaswa kuepuka kuwadhuru wengine na tunapaswa kujitahidi kutafuta furaha ya wote. Tunaweza kuelewa hili kwamba kama Wakristo tunaitwa kuwapenda kila mmoja na kuwatumikia wote kwa mapendo, na kuweka ubinafsi pembeni na kutafuta uzuri wa kila mmoja wetu. Hii ni moja ya amri. Paulo analifikiria hili kama njia ya kuleta wokovu kwa wengine. Sisi ni wamisionari hivyo tunapaswa kufikiria kila wakati ni jinsi gani tutawavuta wengine kwa Yesu.

Somo la Injilii kutoka katika Injili ya Marko, inatuleta tena kwenye ugonjwa wa ukoma. Mkoma katika Injili ya leo anataka kuponywa. Imani yake kwamba Yesu anaweza kumponya ni kubwa kiasi kwamba Yesu anamwambia. “takasika”. Na hivyo ugonjwa unamwacha. Ingawaje Yesu anamwambia huyu mkoma akae kimya, huyu mkoma hawezi kukaa kimya. Mkoma anatangaza kila mahali kwamba ameponywa na Yesu.

Dhambi katika kanisa la Mwanzo inaonekana kama ukoma. Tulitwa na Yesu kuwa watakatifu na safi kwa njia ya ubatizo. Kanisa la mwanzo walipata ugumu kutambua ni namna gani mtu aliyebatizwa anaweza tena kurudi kwenye dhambi. Lakini dhambi ni kama ukoma ambao unarudi tena na tena mpaka pale utakapo pata tiba kamili. Dawa ya ukoma wa kiroho ni Imani kwa Yesu Kristo. Leo tujitazame wenyewe tujichunguze ni kitu gani kinanifanya niwe na ukoma wa kiroho? Imani yangu je nimeacha kutumia dawa yangu, ambayo ni Imani kwa Yesu na kushikama naye? Ni dawa gani natumia?

Wapo wadhambi wengi katika jamii yetu, ambao wanahitaji kusaidiwa na kurudishwa katika kundi la Mungu. Je, kama jamii tunafanya jitihada yeyote kuwarudisha katika kundi la Kristo? Au tunawaumiza kwa maneno mabaya na kujikuta tunawatenga na jamii na kuwafanya wawe kama wale waliotengwa na jamii kwasababu ya ukoma? Je, tunaahukumu ka kutumia wema wetu? Hatujioni sisi kua wema zaidi kuliko wao na kuwafungia mlango wa kuja wa Yesu?

Leo pia ni mwaliko kuwasaidia wagonjwa walio katika jamii yetu, tusikubali tutawaliwe na dhambi ya utengano. Tuwatengenezee mazingira mazuri, waweze kumuona Yesu kwa njia yetu kama Paulo anavyotuambia tutafute uzuri wa wengine. Kama wakristo tuache kuona kwamba kuwa na mgonjwa nyumbani ni aibu au ni mkosi. Tuwatafutie wagonjwa huduma za kiroho, mwite padre daima ili aweze kupokea sakramenti mbali mbali na hasa kumpokea Yesu kama hawezi kwenda kanisani. Mara nyingi tunawasahau kuwapatia huduma kama hii muhimu kwa roho zao. Jitahidi huwezi jua nawe siku moja watajitokeza wengine wakuuguze katika hali yako ukipatwa na ugonjwa.

Cha muhimu tena kabisa katika dominika hii ya 6 ya Mwaka ni kwamba, je, nina mpango wa kuacha dhambi zangu? Je nipo tayari kumuita Yesu aje kunitakasa kwa njia ya sakramenti ya kitubio? Ninaacha huu ukoma wa dhambi unitafune mpaka lini? Au nitaweka ugumu wa moyo wangu na kusema siwezi kwenda kuungama kwa Padre mwanadamu kama mimi? Je, nipo tayari kutangaza utukufu wa Mungu baada ya kukutana na Yesu kama yule mkoma?

Sala:
Ee Yesu nakuomba unikase na ukoma wa dhambi zangu, ili niweze kutangaza sifa zako bila kukoma, niwasaidie wakoma wenzangu niwalete kwako kwa njia ya matendo yangu ili uwatakase. Yesu nakutumaini wewe.
Amina

Maoni


Ingia utoe maoni