Jumatatu, Februari 12, 2024
Jumatatu, Februari 12, 2024
Juma la 6 la Mwaka wa Kanisa
Yak 1:1-11;
Zab 119: 67-68.71.75-76;
Mk 8: 11-13
MIUJIZA KUTOKA MBINGUNI!
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo neno la Bwana katika asubuhi ya leo tunaanza kwa kuliangalia somo la kwanza toka katika kitabu cha Yakobo. Hiki ni kitabu kilichoandikwa kutoa muongozo kwa jamii ya Wakristo wa mwanzo hasa juu ya fundisho la kuhusu neema na matendo ya sheria kwa kanisa ambalo lilikuwa katika hatua zake za uchanga na lilikuwa likisumbuliwa na madhulumu toka kwa maadui wa nje na pia lilikuwa likijitahidi kuyapatia msingi mafundisho yake makuu.
Katika sehemu tunayoisikia leo, Yakobo anatambua mateso ya hawa Wakristo na majaribu waliyokuwa wanayapata na pia juu ya changamoto kama za umaskini walizokuwa wanazipata. Wakristo hawa walikuwa wakiishi kama jumuiya ndogo kati ya wengi waliokuwa wapagani. Changamoto waliyoipata Wakristo ni kwamba walitengwa kwa sababu ya dini yao. Hawakupata wa kuwapatia ajira, walinyanganywa ardhi yao na walikosa wa kuwatetea. Hivyo, walikumbwa na jaribu la kutaka kuacha dini yao ili nao wapate ajira. Hivyo, Yakobo anawaandikia akisema kwamba hayo ni majaribu tu. Wasikubali yawafanye wakate tamaa. Yasiwafanye waache ukristo ili waajiriwe, wavumilie, ni majaribu tu, ni mapito tu, yote haya yanamwisho wake. Yanakujaga maishani na kupita tu lakini hadi yapite lazima uwe imara ili yasikusombe. Wawe na hekima kutambua kwamba vitu vya dunia na utajiri wake vinakwisha.
Ndugu zangu, fundisho hili la Yakobo ni la uhalisia mkubwa kwa sababu hadi leo changamoto hasa za umaskini ni sababu ya watu kukubali kumtumikia shetani. Tupo tayari kufanya matendo ya ushetani kwa sababu tunaogopa umaskini. Tunaona mali zikiisha, matajiri wakubwa wanakwenda na kuwaachia wengine mali zao ambao hata hawakuwasaidia kufanya kazi au hata mali zao zinaishia kuibwa na wengine tu ambao hata hawakuwasaidia kufanya kazi. Hayo yote tunaona. Lakini umwambie mtu ati awe na hekima asitegemee pesa-weee? Hakuelewi. Nitakusikiliza sasa hivi lakini baada ya dakika tano nikiona changamoto kidogo tu ya fedha basi nitakuwa tayari kufanya hata tendo la uovu.
Yakobo anasisitiza leo tuwe na hekima. Yanayotokea kwa wenzetu, jinsi mali zinavyoshindwa kumfikisha mtu popote yatufanye tuwe na hekima zaidi.
Katika somo la injili tumesikia Yesu akikataa kutoa ishara kwa mafarisayo kwa sababu alijua kwamba walikuwa wanamjaribu na kumchezea chezea tu na hata angeitoa wasingeweza kumwamini. Ni hivyo hivyo na kwetu sisi ndugu zangu. Yesu anatoa ishara kila siku. Yanayotokea kwa mwenzako ni ishara tu. Wapo wengi walioshindwa kuvumilia majaribu yaletwayo na changamoto mbalimbali kama umaskini. Wakaishia kutumia njia za uovu kama wizi, kudhulumu mali za wengine, kudhulumu mirathi ya mayatima, kugushi vyeti na kuiba mali za watu lakini sasa wako wapi? Mali imewafikisha wapi?. Iwe ishara kwetu-ya kuijenga Imani yetu. Tusipoyaona haya kama ishara ya kujenga Imani yetu, basi tusitegemee ya ziada. Haya ndio ya mwisho.
Maoni
Ingia utoe maoni