Ijumaa. 23 Februari. 2024

Tafakari

Jumatatu, Februari 05, 2024

Jumatatu, Februari 5 2024
Juma la 5 la Mwaka

1 Fal8: 1-7.9-13;
Zab 132: 6-10,
Mk 6: 53-56.

KUKIMBILIA KWA YESU

Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo neno la Bwana katika asubuhi ya leo tunaanza kwa kuliangalia somo la kwanza. Leo tunakutana na mfalme Solomoni ndio kamalizia kumjengea Bwana hekalu na leo analipeleka sanduku la Agano ndani ya lile hakalu-kwenye sehemu iitwayo patakatifu pa patakatifu. Na Bwana mara moja anafurahia kukaa ndani ya lile hekalu. Utukufu wake unatanda ndani ya hekalu la Bwana-na kipindi chote hiki Israeli yote ilibarikiwa ardhi ilikuwa na chakula cha kutosha, watu wakawa katika furaha kubwa tu. Bwana alikubali kukaa ndani ya hekalu na kuwabariki watu. Lakini mambo yalibadilika watu walipoanza kutenda dhambi wakiongozwa na mfalme Sulemani. Waliingia katika dhambi za kuitolea dhabihu miungu mingine. Nakwambia Mungu alikasirika. Ile nchi ikalaaniwa, ikawa haizaagi tena hata mazao vizuri, Bwana akawakimbia, mambo yakaanza kuwa magumu, njaa tu, hakuna kitu, na walipoendelea kutenda dhambi Zaidi, Bwana alikimbia kabisa ndani ya lile hakalu na ndipo alipokuja mfalme Nebuchadnezer kuliteketeza hakalu. Ndivyo ilivyo ndugu yangu, Bwana anastahili heshima, apewe haki yake. Ukiwa mtii kwake anakuja na kusafiri nawe katika hali zote, ziwe za shida au raha. Lakini ukikosa utii, anakukimbia.

Katika Injili tunakutana na Yesu akiwaponya watu mbalimbali. Watu wanakwenda kwa Yesu, wanamkimbilia, wanapatiwa ufumbuzi wa magonjwa yao nao wanafurahi. Nasi ndugu zangu siku hizi tunaye Yesu, yupo nasi katika sakramenti. Kwa sakramenti zake, Yesu hutuponya-hiki ni kitu kilichoahidiwa na Yesu. Lakini nasi tuna changamoto kama ilivyowakuta wale watu wa nyakati za sulemani. Kweli Bwana alikubali kukaa kule hekaluni na waliona kwa macho. Lakini wakamkimbiza kwa dhambi. Vile vile na sisi. Bwana hukaa katika sakramenti lakini tukiwa watu wa dhambi na kuzikufuru sakramenti zake, basi tutaishia kukumbwa na hiki kilichowakumba wana wa Israeli. Bwana atatukimbia ndani ya hizo sakramenti. Utazitumia lakini uponyaji hauji kwa sababu ya kukosa heshima na Imani. Tuwe na Imani leo. Ni muhimu. Kabla ya kupokea sakramenti au kuja kanisani au ukiwa katika sala, tuliza mawazo. Sali kwa Imani.

Maoni


Ingia utoe maoni