Ijumaa, Januari 19, 2024
Januari 19, 2024
JUMA LA 2 LA MWAKA
1Sam. 24:2-20
Zab. 57:1-3, 5 (K) 1
Mk 3: 13-19
KUELEKEA MLIMANI!
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu kwa siku ya leo. Leo neno la Bwana tunaanza kwa kuliangalia somo la kwanza. Hapa tunamkuta Mfalme Sauli akimwinda Daudi ili amuue na Mungu anatoa onyo la kwanza kwa Mfalme Sauli kwamba unayemtafuta hutaweza kumshinda. Leo Sauli anajikuta amejipeleka mwenyewe mikononi mwa yule ambaye anamtafuta amuue na sasa kibao kingemgeukia yeye. Yaani yeye ndiye anaenda kujiua mwenyewe. Nguvu anazotumia kumwangamiza nazo Daudi ndizo hizohizo zinazomuangamiza yeye.
Sauli anapewa onyo hili na Mungu ili angalau abadilike lakini yeye ataweka tamaa mbele na hatabadilika.
Ndugu zangu, hapa twajifunza kitu muhimu sana juu ya kunia mabaya juu ya mwenzako. Unaponia mabaya juu ya mwenzako, ile nia yako mbaya ndiyo inayokuwa kiangamizo chako. Jinsi ulivyopanga kumwangamiza, na unavyotaka yeye ateseke ndivyo hivyo inavyokugeukia wewe kama ilivyomgeukia Sauli leo. Hivyo ndugu zangu, tuepuke kunia mabaya au uovu juu ya mwenzako kwani uovu humrudia; utakuja tu na kukusumbua; hata kama umemtendea aliye dhaifu uovu huo utakurudia tu. Hivyo, tuepuke kuwatendea uovu wenzetu ndugu zangu.
Katika Injili Yesu anawachagua mitume wake kumi na mbili. Hawa walikuwa ni watu muhimu sana. Hawa ndio wangepaswa wamwakilishe hapa duniani na kuendeleza utume aliouanza. Hivyo, Yesu alikuwa makini sana kwenye kuchagua. Tunasikia kwamba anakwea mlimani na kuwachagua akiwa juu ya mlima. Mlimani kwa wana wa israeli ni sehemu ya kukutania na Bwana. Yesu hapa anakuwa kama Musa mpya pale mlimani Sinai kabla ya kuwapatia makabila kumi na mawili ya Israeli amri na Agano la Mungu. Hawa mitume ndio wanaowakilisha kabila kumi na mbili za Israeli; kila mtume ni kama babu wa kabila. Nafasi hiyo waliitambua na kuichukulia kwa umakini mkubwa.
Nasi ndugu zangu tunashirikishwa katika utume huu kwa ubatizo wetu na ukristo wetu.
Kuwa mkristo ni kuwa mtume na kama mtume ni kwamba unakuwa baba wa kabila nzima. Yaani, unakuwa kuna watu mbalimbali wanao kutazama; wafanye watu hawa wamwone Kristo kwako wamtukuze Kristo, wakija kwako wafurahi, wapate matumaini, waone tofauti na hata kama ni wa dini nyingine wakamtukuze Mungu Bwana wa Israeli. Hivyo, mkristo kazi yake ni kuangalia kwamba huliangushi kabila lako, hulifanyi liteketee kama yale ya Israeli yalivyoteketea bali tunaenda nayo mbinguni. Hivyo, namna hii twaweza kutimiza wajibu wetu kama mitume wa Kristo. Ishi vizuri uwe chanzo cha baraka nakuonesha mfano.
Maoni
Ingia utoe maoni