Jumapili, Januari 21, 2024
Jumapili, Januari 21, 2024
Juma la 3 la Mwaka wa Kanisa
Yona-3:1- 5,10
1 Cor 7:29-31
Mk 1: 14-20
KUTUBU NA KUIAMINI INJILI
Tupo katika kipindi cha kawaida cha mwaka lakini tunasikia ujumbe ambao kwa kawaida tunausikia mara kwa mara katika kipindi cha kwaresima. Mwanzo wa utume wa Yesu alianza kwa kuwaalika wafuasi wake watubu. Kutubu katika hali hii ni kuwaalika wabadilike waelekee kwenye mwelekeo mwingine wa maisha mapya. Na tunaona kabisa maisha mapya ambayo Yesu anataka sisi tuyaanze, ni maisha ya “ KUIAMINI INJILI”.
Somo la kwanza leo tunaona habari ya ujumbe wa toba alio uhubiri Yona kwa Waninawi ulivyo fanyiwa kazi. Ulifanikiwa kwa asilimia mia moja, kwani watu wote walitubu hata mpaka mfalme mwenyewe. Ingawaje Yona mwenyewe hakutaka mji wenyewe utubu bali uangamie. Lakini kwasababu walisikiliza ujumbe wa Mungu wakatubu basi Mungu aliwasamehe kutoka katika uovu wao. Tunapaswa kutambua hili, watu walitubu na Mungu naye akaacha kuwaadhibu, (ni kama vile watu wanatubu na Mungu naye anatubu, ingawaje Mungu hatendi dhambi) sisi tuna bahati ya kusikia ujumbe wa namna hii mara nyingi. Kiini cha maisha ya Injili kwakweli ni kumwalika kila mmoja aache dhambi awe na maisha safi ya kuunganika na Mungu. Tunaitwa kusikiliza wito huu wa Injili na kubadili mienendo yetu isiyo mpendeza Mungu, tuguswe na ujasiri wa watu wa Ninawi walivyo badili mienendo yao mara moja na Mungu akawasamehe. Pia tunaweza kuwa na watu kama wakina Yona wakati wetu, wapo wanaohubiri watu wabadilike lakini pale mtu anapo badilika tunashindwa kukaa naye tena, inakuwa kana kwamba tungependa abaki tu hapo hapo kwenye dhambi ili tuendelee kumwambia acha dhambi tu bila kubadilika, wakati mwingine hata akibadilika tunakasirika kwasabau hatuna tena mtu wakumuonya. Au pengine kutokana na maovu aliyotenda tungependa tumuone Mungu akimshushia moto kutoka mbinguni kwasababu tunadhani dhambi zake ni kubwa sana. Tusiwe hivi ndugu zangu, tuige sifa ya Mungu ya kuwaonea huruma.
Somo la pili kutoka barua ya kwanza ya mtume Paulo kwa Wakorintho. Tunaambiwa kwamba ulimwengu huu unapita na hivyo matendo yetu yanapaswa kubadilika. Tunapaswa kuweka nguvu zote katika kumuona Mungu na njia zake. Kuna hatari ya kupenda kungangania matamu ya ulimwengu, na dhambi nyingine huonekana kuwa tamu, na hivyo wengi hatupendi kupokea ujumbe wa injili kwasababu tunajua tukipokea tu, tutaonywa tuache matamu hayo. Injili inaita kuacha kushikamana na mambo ya ulimwengu ambayo tunadhani ni ya muhimu sana kumbe ni ya muda tu na sio muhimu kwa maisha ya Ufalme wa Mungu . Tambua ni wapi ulipo kamatwa ambapo unashindwa kukaribisha Injili ya Yesu kisa tu unaogopa utaacha matamu yako.
Na katika somo la Injili ujumbe wa toba unaendelea tena. Yesu anahubiri Injili. Mara nyingi tunafikiria Injili kuwa tu ni maneno ya Yesu, lakini ukweli ni kwamba licha ya kuwa maneno ya Yesu ni “habari njema”. Je ni habari njema ipi aliohubiri na Yesu? Ni hii: aminini Kwamba Mungu anatupenda sisi akamtuma Mwanaye kwa ajili ya ukombozi wetu! Hata tusipo kubali ukweli huu, bado hatuwezi kukataa ujumbe huu kwani ndivyo lilivyo pendo la Mungu kwetu. Changamoto yetu kubwa ni kukubali Injili hii na kuiishi katika maisha yetu. Tunapaswa kuipokea itubadilishe kutoka ndani na kukubali kuwa wana wa Mungu. Tukiipokea tutawaleta pia na wengine katika mwaliko huu waweze kuwa karibu na Yesu na sakramenti zake. Tusivumilie kuwaona wenzetu wanabaki katika uchumba sugu, hawaendi kanisani, hawasali, na wala hawataki kuwa karibu na Mungu. Tuwasaidie na kuwaongoza na hasa kwa njia ya sisi wenyewe kuonesha mfano mzuri kwa kuiishi injili.
Katika somo la Injili pia tunamuona Yesu akiwaita Petro na Andrea ambao walikuwa wakivua samaki. Mara moja wanaitika wito wa Mungu na kubadili maisha yao. Wanaacha kila kitu na kumfuata Yesu. Baadae Yesu anamwita tena Yakobo, na hawa wote wanaacha yote na kumfuata Yesu. Ndugu zangu hivi ndivyo tunavyo paswa kufanya tunavyo kutana na ujumbe wa Injili, unapo ingia katika masikio yetu tunapaswa kuacha yote na kumfuata Yesu. Tusiwe na wasiwasi na kuanza kuangalia maslahi tunayopata tena kwa kupima kwa kuangalia faida ya ulimwengu unaopita kama Paulo anavyosema katika somo la pili. Tuachie vyote na kuanza maisha mapya. Tuogope kukamatwa na mali, urafiki mbaya, fedha, anasa, sifa, majivuno nk. Badala yake tusikiapo ujumbe wa toba “tubuni na kuiamini Injili” basi tuachilie yote hayo na kuanza maisha mapya kama mitume walivyo itikia wito wa Yesu na kumfuata. Mungu atusaidie tuweze kumsikiliza daima na kubaki katika hali ya usafi wa roho na mwili.
Maoni
Ingia utoe maoni