Ijumaa. 22 Novemba. 2024

Tafakari

Alhamisi, Januari 18, 2024

Januari 18, 2024

JUMA LA 2 LA MWAKA



1Sam. 18:6-9; 19:1-7

Zab. 56:1-2, 8-12 (K) 4

Mk 3: 7-12



KATIKA SAFARI YA KUKUTANA NA YESU!



Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu. Leo neno la Bwana katika asubuhi ya leo linaanza kwa kuliangalia somo la kwanza. Hapa tunakutana na ugomvi ukitokea kati ya Daudi na Sauli baada ya Daudi kumwua Goliathi. Ukweli ni kwamba Sauli kama mfalme wa Israeli ndiye aliyepaswa kwenda kupigana na Goliathi lakini alimwogopa Goliathi. Daudi akajitolea kwenda kupigana naye na kumshinda na watu wakafurahi-wanawake wa Israeli waliusifu ushujaa wake. Lakini Sauli anakasirika, anamuona Daudi kama mshindani anayetafuta kuuchukua ufalme wake na hivyo anaanza kutaka kumwangamiza.

Lakini uamuzi huu wa Sauli ulikuwa ni shida tupu kwani kwani Mungu yupo upande wa Daudi. Mwishowe Sauli anaanza kujitutumua kupigana na Daudi mwishowe Sauli atakufa tena kifo cha aibu.

Ndugu zangu, Sauli angemkubali Daudi na kumpokea, angesaidia katika kuuimarisha ufalme wake. Lakini badala yake alimuona kama adui wa Ufalme wake na ndio maana aliishia kuupoteza ufalme badala ya kuuimarisha ufalme. Hili liwe fundisho kwetu ndugu zangu. Katika maisha tutakutana na watu ambao kwa kweli Mungu kawabariki na wanauwezo kuliko sisi. Tuwakubali na kuwapokea watu hawa kama zawadi. Tusiwaone kana kwamba ni tishio kwetu. Mara nyingi huwa tunaanza kupambana na kuwapiga vita na mwishowe tunaishia kupoteza. Lakini tukiwakubali, nakwambia huwa wanatusaidia na sisi kungaa. Wengi wetu ni maskini kwa sababu tumepambana na waliobarikiwa, kupingana nao bila sababu, kushindana badala ya kuwafanya watusaidie watufanye tungae.Tumeishia kuwaonea wivu na kubakia katika umaskini kila siku.

Katika injili, fundisho hili linadhihirika rasmi. Wale wanaomkubali mwenye uwezo, wale wanaomkubali Yesu ndio tunaosikia anawaponya. Wangemkataa Yesu na kuanza kupambana naye, wasingefika popote. Hivyo, ndugu zangu, tujifunze kuwapokea wale waliopewa uwezo kwani watatufanya nasi tungare. Ukipambana nao unazidi kuwa maskini mwenyewe kiroho kwani hutakubali hata kupewa tafakari na mtu fulani kwani utajiona najua kila kitu. Kubali kipaji na uwezo wa mwenzio na shirikiana naye utashangaa Mungu naye atakuinua pia.

Maoni


Ingia utoe maoni