Ijumaa. 22 Novemba. 2024

Tafakari

Jumamosi, Januari 13, 2024

Januari 13 2024.

------------------------------------------------

JUMAMOSI, JUMA LA 1 LA MWAKA

Somo la 1: 1 Sam 9:1-4,17-19, 10:1 somo linaelezea jinsi Saulo anavyochaguliwa Mfalme na kutawadhwa na Samweli.

Wimbo wa katikati : Zab 20:2-7 Ee Bwana, nguvu zako zinampa Mfalme furaha.

Somo la : Mk 2:13-17 Injili inaelezea wito wa Mathayo. Inaelezea pia hasira inayo wakumba Mafarisayo kwasababu ya kumuona Yesu akila chakula pamoja na watoza ushuru na wadhambi.

------------------------------------------------



YESU NA HURUMA YAKE KWA WADHAMBI



Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi hii. Leo katika neno la Bwana tunamsikia Yesu akisema kwamba amekuja kwa wagonjwa na si kwa wenye afya; hawa ndio wadhambi kama akina Matayo mtoza ushuru, makahaba kama akina Maria Magdalena na yule mwizi aliyetubu akiwa msalabani. Cha kushangaza ni kwamba wale wagonjwa wanafurahi na kumpokea Yesu kwa furaha na ndio wanaourithi ufalme wa Mungu. Wanaojiona sio wagonjwa wao ndio wanaompinga Yesu; hawa ndio Wafarisayo na mwishowe tutasikia kwamba watajifungia hata ufalme wa mbingu.

Hapa tuna la kujifunza ndugu zangu, tunapokuja kwa Mungu, lazima tujione kuwa wadogo, wanyenyekevu. Hawa ndio wanaofaulu mbele ya Mungu. Lakini wanaokuja mbele ya Mungu wakijiona kwamba ni wafalme, nakwambia huwa hawafiki mahali na wote huishia hivihivi tu. Unapofika mbele ya Mungu, fika na udhaifu wako, fika na ujinga wako, fika na makosa yako. Usifiche makosa yako yote na kuanza kuonesha ukuu wako, ukubwa wako, majitoleo yako, jinsi utoavyo sadaka kama yule Mfarisayo alivyofanya mbele ya mtoza ushuru. Wewe hakikisha huachi udhaifu wowote, yeye anamwilika ndani ya roho zote na anatufahamu vizuri zaidi.

Hiki ndicho kitakachokusaidia kusimama mbele ya Kristo na kumpatia Kristo arekebishe udhaifu wetu. Mfalme Sauli tunayemsikia katika somo la kwanza japokuwa alikuwa na uzuri wake, alichokosa kama tutakavyoendelea kusoma huko mbeleni ni ile roho ya kujishusha, kuja kwa Mungu na udhaifu wake. Hiki ndicho alichokosa. Alikuwa anakwenda na makuu yake tu na hivyo alishindwa kumpatia Mungu nafasi arekebishe hayo mapungufu yake.

Hivyo, tunapokuja kusali leo, tusisahau kuja na mapungufu yetu. Yaoneshe mbele ya Mungu na hivyo utafanikiwa kumpatia Mungu nafasi. Usiwe kama yule mfarisayo aliyejikuja mbele ya Mungu na CV safi na kusahau ni dhaifu mbele ya Mungu. Twende mbele ya Mungu kama tulivyo nakufungua moyo wote na kumwambia wewe Bwana wanijua nilivyo dhaifu naomba unipe afya ya roho yangu na mwili pia.

Maoni


Ingia utoe maoni