Jumapili, Januari 14, 2024
Jumapili, Januari 14, 2024
Juma la 2 la Mwaka wa Kanisa
Sam 3: 3-10; 19
Zab 39: 1-4-7,10
1Kor 6:13-15,17,20
Jh 1: 35-42
Ndugu zangu wapendwa, masomo yetu ya leo yanatualika kuiungama imani yetu ikiwa ni pamoja na kumtangaza Yesu Kristo katika mazingira yetu. Sisi kama wafuasi wa Yesu Kristo, na kama wakristu tulio hai ni wajibu wetu kumtangaza Yesu Kristo kwa wengine. Kama sisi tunajinadi kuwa wakristo, tunashindwa je kumtangaza Yesu Kristo kwa wengine? Je ukristu wetu uko wapi? Masomo yetu ya leo yanatualika kuwajibika katika hili.
Katika somo la kwanza tumesikia jinsi Eli alivyomtambulisha kijana mdogo aitwaye Samueli kwa Mungu. Kijana huyu alikuwa hana maarifa au uelewa wowote juu ya mambo ya Mungu. Lakini Eli alimsaidia kuitika wito wa Mungu alipokuwa anaitwa. Na ni katika njia hii Eli alimshirikisha Samueli katika kumuelewa na kuyatambua mapenzi ya Mungu juu yake.
Katika somo la pili, Mt. Paulo anawashirikisha wakorintho imani ya Yesu Kristo aliyoipata alipokuwa njiani kuelekea Damaskasi. Anawaambia kuwa wanapaswa kuishi kwa uaminifu katika ukristu wao. Na katika Injili, tunasikia jinsi Yohane Mbatizaji alivyowatambulisha wanafunzi wake wawili kwa Yesu Kristo ambaye ni Mtu kweli na Mungu kweli, kama “Mwanakondoo wa Mungu”. Na hao wanafunzi wanaamua kumfuata na kukaa pamoja naye. Mmojawapo wa hao wanafunzi alikuwa ni Andrea. Naye anachukua jukumu la kumleta Petro nduguye kwa Bwana Yesu na kumtambulisha kwake. Katika injili ya nne ambayo ni ya Yohana, Andrea anaonekana kuwa na majukumu ya kuwatambulisha watu mbalimbali kwa Bwana Yesu. Katika Injili ya leo Andrea anamleta nduguye Petro kwa Yesu Kristo (Yoh. 1/40). Pia kabla ya Yesu Kristo kuwalisha watu elfu tano kwa mikate mitano na samaki wawili, Andrea ndiye aliyemuonesha Bwana Yesu yule kijana aliyekuwa anauza hiyo mikate pamoja na hao samaki (Yoh 6/8). Na kabla ya karamu ya mwisho, Andrea aliwatambulisha watu wa Kigiriki kwa Bwana Yesu (Yoh 12/20-22). Hivyo Andrea anatambulika kwa kuwaleta watu kwa Yesu Kristo, ambaye ni Mtu kweli na Mungu kweli.
Sasa tujiulize maswali machache. Ni jinsi gani sisi tumejaribu kumtambulisha Yesu Kristo kwa wenzetu, au ni mara ngapi tumefanikiwa kuwaleta wenzetu kwa Yesu Kristo? Ni mambo gani yanayotufanya tushindwe kuikiri imani yetu mbele ya wenzetu? Vijana wana kauli mbiu yao ambayo ni kumleta Yesu Kristo katika mazingira yao ikiwa ni pamoja na katika familia wanazotoka. Je ni kweli wanatekeleza hili? Na kama tunaamini kwamba Injili ni habari njema sasa ni kwa nini tunashindwa kuwashirikisha watu wengine? Je tunaweza kujitetea kuwa sisi hatuna maarifa juu ya Mungu au hatumfahamu Yesu Kristo vizuri?
Wakati tunapokuwa na mambo mazuri yanayoifurahisha nafasi, huwa tunawashirikisha wenzetu. Kama ikitokea mtu akahujumiwa katika mambo yale ayapendayo, utamsikia akisema “Aa, wameizulumu nafsi yangu bwana”. Lakini ni nini kilicho muhimu kwangu mimi zaidi ya imani yangu kwa Bwana Yesu? Ndugu zangu wapendwa tunapaswa kumtambulisha Yesu Kristo katika mazingira yetu na kwa watu tunaoishi nao. Injili ya leo inatualika kuchukua hatua na kuacha ukaidi wetu wa kumtangaza Yesu Kristo kwa wengine. Kama tunaamini kwamba injili ni habari njema na, kuwa Bwana Yesu ni hazina kubwa inayomilikiwa na mioyo yetu, sasa ni kwa nini tunakuwa wagumu kuwashirikisha imani yetu tulionayo kwa watoto wetu, marafiki zetu na watu tunaoishi nao, na hasa wale ambao wanaitafuta imani hii? Hili ndilo swali muhimu ambalo lipo katika injili yetu na kila mmoja wetu anapaswa kujiuliza. Hakuna mtu anayeweza kutusaidia kulijibu swali hili. Tunapaswa kulijibu sisi wenyewe kila mtu katika muonekano wake. Ni dhahiri kwamba tunahitajika kuwajibika katika kumtangaza Bwana Yesu kwa watu wengine.
Basi tumwombe Mwenyezi Mungu atupe nguvu,uwezo na ujasiri ili tuweze kumtangaza Bwana Yesu katika mazingira yetu na katika jamii tunamoishi.
Maoni
Ingia utoe maoni