Ijumaa. 22 Novemba. 2024

Tafakari

Jumapili, Oktoba 29, 2023

Jumapili, Oktoba 29, 2023
Juma la 30 la Mwaka

Sikukuu ya Watakatifu Simon na Yuda, Mitume

Kut 22:20-26;
Zab 17:2-4, 47, 51;
1Thes 1:5-10;
Mt 22:34-40


UPENDO:ALAMA YA UFUASI WA KIKRISTO!

Masomo ya leo yanatualika tutafakari juu ya msingi wa maisha ya kila mfuasi wa Kristo yalipojengwa: upendo kwa Mungu na jirani. Wakati mwingine tunapotezwa katika mawazo mabaya kuhusu upendo kwa Mungu na kwa jirani. Ni vizuri kutafakari juu ya hili mara kwa mara. Mwalimu wa Sheria alimuuliza Yesu swali ili kumtega. “ni Amri ipi iliyo kuu zaidi katika sheria?’ Ni wazi uhusiano wa Yesu na hawa viongozi wa dini unaonekana ulikuwa una malumbano. Walikuwa wakimjaribu hata kumtega. Lakini kama kawaida Yesu aliendelea kuwanyamazisha kwa maneno yake ya hekima.

Yesu alimjibu mwalimu wa sheria kwamba “umpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote kwa akili zako zote… “hii ni amri kubwa kuliko zote na ya pili, “mpende jirani yako kama nafsi yako” (Mt 22:37-39). Yesu anatoa ufupisho wa sheria zote za maadili zinazo patikana katika Amri kumi za Mungu. Amri tatu za mwanzo, zinasisitiza upendo kwa Mungu kwa moyo wote. Na amri nyingine zinasisitiza upendo kwa jirani. Sheria ya maadili ya Mungu ni rahisi kama hizi amri mbili tu zinavyosema.

Mfuasi wa Kristo anapaswa kufuata sheria ya upendo. Sheria hii ina nyanja mbili –upendo kwa Mungu na upendo kwa jirani, na hii inakuwa ni alama ya ufuasi wetu. Nini maana ya kumpenda Mungu na jirani? Kwanza kabisa upendo wa Mungu ni kuuelewa upendo wa Mungu kwetu sisi. Sisi ni dhaifu kabisa na hatuwezi kumpenda Mungu kama inavyopaswa. Lakini kwa njia ya Kristo tunaweza kufahamu kwamba Mungu anatupenda. Hivyo kufahamu upendo wa Mungu licha ya kwamba mtu ni dhaifu inamfanya mtu ampende Mungu kama shukrani. Na huu ndio mwanzo wa upendo. Wakati mtoto mdogo anavyofahamu upendo wa mama juu yake, hauleti chochote kwa Mama. Huu ndio upendo wetu kwa Mungu. Wakati tunavyo ufahamu upendo wa Mungu sisi hatuongezi chochote kwa Mungu, hatuta anguka kwenye dhambi tutafana na yale yanayo mpendeza yeye. Inamfurahisha Mungu tunavyo pendana sisi kwa sisi. Mmoja akianza kumpenda Mungu, anaanza pia kuwapenda wengine.

Somo la kwanza leo kutoka katika kitabu cha kutoka linaelezea amri ya Mungu kwa wana wa Israeli: upendo kwa jirani. Ni wakati gani upendo wangu kwa jirani utakuwa mkamilifu? Tunapo wapenda majirani zetu tunatamani na wao wapate nafasi katika ufalme wa Mungu. Tunakuwa tunatamani kama wataishi katika neema ya Mungu siku zote za maisha yao. Na hivyo waweze kuishi milele kwa sababu ya neema tuliopokea kutoka kwa Kristo. Tukiwapenda wenzetu namna hii hatuwezi kuwanyima chochote au mahitaji yeyote wanayo taka kwetu. Tunakumbuka alichosema Yesu, kwamba mlicho watendea wadogo hawa mlinitendea mimi. Tunaenda kuwatembelea watu walio katika mahitaji mbali mbali kwa njia ambazo zipo katika uwezo wetu. Na huu ndio upendo kwa jirani.

Mt. Paulo katika barua yake kwa Wathesalonike katika somo la pili leo, anawakumbusha umuhimu wa kuongoka katika Imani ya maisha ya Kikristo, ambapo ni kumtumikia Mungu na kumtumikia Mwanae Yesu Kristo aliye mfunua Baba na Roho kwetu.

Tafakari juu ya wito wa kumpenda Mungu na jirani kwa jinsi ulivyo. Fikiria juu ya neno “wote” kupenda kwa moyo “wote”, na ukitafakari kuhusu hili utatambua njia ambazo umeshindwa kutoa kitu kwa ajili ya Mungu na hata kwa jirani. Ukiona upungufu wako, anza tena kwa kujikabidhi katika kuwa zawadi kwa Mungu na kwa jirani.

Sala:
Bwana, ninachagua kukupenda wewe kwa Moyo wangu wote, akili na utashi wote na nguvu. Nipe neema niweze kuishi amri hizi mbili za upendo na kuziona kama njia za kuelekea kwenye utakatifu wa maisha. Ninakupenda Bwana wangu. Yesu nakuamini wewe.
Amina

Maoni


Ingia utoe maoni