Alhamisi, Oktoba 19, 2023
Alhamisi, Oktoba 19, 2023.
Juma la 28 la Mwaka wa Kanisa
Rom 3: 21-30;
Zab 130: 1-6 (K) 7;
Lk 11: 47-54.
UFUNGUO WA MAARIFA!
Injili ya leo inaongelea kuhusu kutokuelewana kati ya Yesu na viongozi wa dini wa wakati huo. Walimu washeria walimwelezea Mungu kama hakimu mkali sana na wakaweka sheria na miiko ambayo haikuwa na uhusiano kabisa na amri za Mungu. Wao kwa njia ya mafundisho ya uongo waliwahukumu na kuwaua Manabii, na baadaye walitengeneza makaburi kwa heshima yao. Leo Yesu anawanyoshea kidole, kwamba wanajizuia wenyewe nakujiwekea mizigo katika kuingia Ufalme wa Mungu na pia kuua hamu ya wengine ya kumtumikia Mungu.
Yesu anawaonya kwasababu “wamechukuwa ufunguo wa maarifa kutoka kwa wengine”. Na kujaribu kuwaweka wengine mbali na elimu ya Mungu wanayo paswa kuwa nayo. Ni nini ufunguo wa maarifa? Ufunguo wa maarifa ni Imani na elimu inayokuja tu kwakusikia sauti ya Mungu. Ufunguo wa maarifa ni kumuacha Mungu aongee na wewe na kufunua kwako undani wa ukweli wake. Ukweli huu unaweza kupokelewa na kuaminiwa kwa njia ya sala na kwa njia ya kuwasiliana na Mungu. Watakatifu ni mifano bora ya wale walio ingia ndani kabisa ya mafumbo ya maisha ya Mungu. Kwa njia ya sala na Imani waliweza kumfahamu Mungu kama alivyo jifunua kwao. Wengi wa watakatifu hawa wametuachia maandiko mazuri na ushuhuda wa mafumbo makuu ya maisha ya Mungu.
Tafakari leo, kama umechukuwa au umeweka ufunguo wa maarifa kwa watu kwa ajili ya mafumbo ya Mungu kwa njia ya maisha yako ya Imani na sala. Jikabidhi tena kwa Mungu ukimtafuta katika sala zako za kila siku na kutafuta yale yote anayopenda na kutufunulia.
Sala:
Bwana, nisaidie mimi niweze kukutafuta wewe katika maisha yangu ya sala ya kila siku. Nivute katika uhusiano wa ndani na wewe, ukifunua kwangu yote ambayo unataka niishi katika maisha. Yesu nakuamini wewe.
Amina
Maoni
Ingia utoe maoni