Jumamosi. 18 Mei. 2024

Tafakari

Ijumaa, Oktoba 20, 2023

Ijumaa, Oktoba 20, 2023,
Juma la 28 la Mwaka wa Kanisa

Rom 4: 1-8;
Zab 31: 1-2, 5, 11;
Lk 12: 1-7.


KUTEMBEA KAMA MTOTO WA MWANGA! (EFE 5:8)

“Ni rahisi kumsamehe mtoto anaye ogopa giza, kinacho shangaza zaidi ni pale watu wanapo ogopa mwanga” (Plato). Maneno haya kwa kweli yanamgusa kila mtu katika maisha. Mara nyingine inaonekana katika maisha kwamba haiwezekani kutoka katika giza hili kwenda katika mwanga, kutoka katika chuki kwenda kwenye upendo. Wengi wetu tunapenda kuwa kwenye giza zaidi kuliko kuwa kwenye mwanga.

Paulo katika barua yake kwa Warumi, anatupa aina mbili za watu wa mfano wa Imani. Abrahamu na Daudi. Abrahamu kwa Imani kubwa kabisa alimfuata Mungu. Licha ya kwamba angeweza kuwa na wasi wasi juu ya kutokuwa na mtoto na pia ni mzee lakini hakuwa na wasi wasi alimfuata Mungu na Mungu akambariki. Mfalme Daudi, ingawaje alitenda dhambi, anapokea msamaha kwasababu ya imani yake kwa Mungu. Wote wanafanywa wenye haki. Wimbo wa katikati unaonesha aina ya furaha ya mtu ambaye amesamehewa dhambi na Mungu, kwa kuomba kwake msamaha kunaleta msamaha wa dhambi zake na kuondoa maumivu.

Katika Injili, tuna viongozi wa dini ambao maisha yao ni tofauti kabisa na kile wanacho hubiri. Wao wanajiona wema lakini matendo yao yanawahukumu. Walikuwa katika giza la kujitakia haki wao wenyewe na kutazama mambo ya nje, na hawakuweza kuona mwanga katikati yao. Katika giza lao, waliwafunga wengine vile vile. Yesu MWANGA wa kweli anawafundisha watu wasifuate mienendo ya viongozi wao. Anawaambia waishi wanacho wafundisha.

Katika maisha yetu tunakutana na giza linalo sababishwa na dhambi zetu, wakati mwingine hata mambo yalio sababishwa na wengine. Tusipo yatibu kuna hatari ya kuzama zaidi kwenye giza hili na kupata madhara kila siku. Lakini leo masomo yetu yanatuita tuwe watoto wa mwanga. Hijalishi umekaa katika giza kubwa namna ghani, Mungu anakusubiri akutoe kwenye giza akulete kwenye mwanga. Sio kwa nguvu zetu na kazi zetu bali imani yetu kwa Mungu kwa njia ya Mwanae Yesu Kristo. Mungu anatuhakikishia hilo, tusiogope, kwani sisi ni wa muhimu sana kwake kuliko viumbe vingine vyote. Tusikose nafasi hii yakuwa watoto wa Mwanga.

Sala:
Bwana, nimekukosea kwasababu ya dhambi zangu, ujinga wangu, na giza langu. Nisamehe kwakutokuja kwako tangu mwanzoni. Ninakuomba nitambue kwamba mimi ni mtoto wa Mwanga. Yesu, nakuamini wewe.
Amina

Maoni


Ingia utoe maoni