Ijumaa. 22 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatatu, Oktoba 23, 2023

Jumatatu, Oktoba 23, 2023.
Juma la 29 la Mwaka

Rom 4: 20-25;
Lk 1: 69-75 (K) 68;
Lk 12: 13-21.


MALI INAWEZA KUNUNUA FURAHA?

Haikuwa kitu cha ajabu kwa watu wa Palestina kumsumbua Rabi kwa swala ambalo lilikuwa linamsumbua. Hivyo leo msikilizaji mmoja alimuomba Yesu awe muamuzi kati yake na ndugu yake kuhusu mali zao. Kadiri ya sheria za Kiyahudi za urithi, Mtoto wa kiume mkubwa kuliko wote alipewa urithi mara mbili (Kumb 21:16-17). Huyu aliyekuja kwa Yesu ni mdogo ambaye alihitaji ugawaji sawa wa mali za Baba yao, tofauti na kufuata sheria ya Kiyahudi inavyosema. Kwa kutumia mfano Yesu anatoa maana mpya ya sheria ya zamani ambapo haki itatendeka sawa kwa wote. Yesu anasema kwamba furaha ya kweli haipatikani kwa kuwa na mali nyingi hata kidogo.

Katika mfano huu, huyu tajiri alipata mali nyingi sana kiasi cha kutaka kubomoa ghala zake na kujenga nyingine kubwa ili aweze kuhifadhi mali zake. Na tazama kumbe mali yote hataitumia tena kwani roho yake inahitajika na Mungu. Tofauti katika haya ni utajiri wa dunia na utajiri ambao Mungu anauhitaji kwa baadae. Ni wazi kuwa unaweza kuwa tajiri katika hali zote mbili, lakini kuliweza hili kunahitajika majitoleo ya kweli na kujitambua.

Changamoto ya kwanza kabisa katika Injili hii ni kuachana na tamaa ya mali. Si kwamba utajiri wa dunia ni mbaya, ila ni wazi kwamba ni kishawishi kikubwa. Kishawishi ni kujikabidhi katika mali za ulimwengu na kuridhika na hivyo kumsahau Mungu. Mali inapaswa kutambulika kabisa kwamba ni kishawishi kikubwa sana ambacho mtu aweza kumwacha Mungu mbali na hivyo mtu binafsi anapaswa kujiangalia sana.

Tafakari, juu ya tamaa yako ya mali. Acha Injili hii ikupe changamoto kuhusu tamaa yako ya kupenda mali. Kuwa mwaminifu na tazama moyo wako. Je, unapoteza muda mwingi ukiwaza kuhusu mali zako na fedha? Mtafute Mungu awe wa kwanza na mengine yote atayaleta yeye.

Sala:
Bwana, ninatamani kweli kuwa tajiri katika neema na huruma, zaidi ya mali. Nisaidie mimi niweze kuweka mbele zaidi yale mambo unayopenda na kutakaswa katika tamaa zangu. Yesu nakuamini wewe.
Amina.

Maoni


Ingia utoe maoni