Jumanne, Oktoba 10, 2023
Jumanne, Oktoba 10, 2023
Juma la 27 la Mwaka
Yon 3: 1-10
Zab 130: 1-4, 7-8 (K) 3;
Lk 10: 38-42.
UWE IMARA NA TAMBUA MIMI NI MUNGU!
Leo tutasikia nabii Yona ambaye anawahubiria watu wa Ninawi juu ya kuangamizwa kwao kwasababu ya dhambi zao. Lakini pia tunasikia juu ya Mungu, kama Mungu kweli alikuwa ameamua kweli kuwaangamiza si asinge mwambia Yona aende? Ukweli unaweza kuona kwamba Mungu ana huruma kweli kweli, alipenda watubu wapate kuishi! Lakini pia Yona kukataa kwake kuongea kwa niaba ya Mungu pengine Mungu angemuangamiza lakini bado alimuonesha huruma. Mungu ni mwingi wa huruma si mwepesi wa hasira. Bwana kama ungehesabu maovu yetu, nani angesimama? (Zab 130:1). Watu wa Ninawi walifanya uamuzi sahihi kwa kubadili njia zao. Mungu aliona juhudi zao akawakomboa.
Wakati Yesu alivyo watembelea Martha na Maria, Martha alikuwa akijishughulisha jikoni na pale Maria anakaa karibu na miguu ya Yesu huku akimsikiliza akiongea. Martha anamuomba Yesu amwambie Maria amsaidie. Yesu anamwambia Martha ana hofu na mambo mengi, wakati Maria amechagua njia sahihi zaidi. Tunaweza kushangaa kwani Martha hakuwa anafanya jambo lilo sahihi ambalo angepaswa kufanya?
Katika maisha yetu ya kila siku pia, mara nyingi tunafanya kazi tena na tena na wakati mwingine tunasahau kwanini kumekuwa na muda maalumu wa kazi. Watu wa ndoa wake kwa waume, wanapoteza muda mwingi katika kazi, na kuwa na muda kidogo tena sana wakuwa pamoja wao kwa wao na pia kuwa na watoto wao. Mapadre na wale wa maisha ya wakfu, hujikuta wanakuwa na muda mwingi wa kufanya utume na kazi nyingi na hata kuwa na muda mchache wakuwa pamoja na kwasababu ya kuchoka huenda kuacha kusali. Na hii huaribu maisha ya jumuiya kwasababu muda wa kupanga mambo pamoja hukosekana. Leo tujiunge na Mt. Fransisko alivyo waambia ndugu zake, “roho ya kazi isizime roho ya sala”. Siku zote waweza kujikuta muda hautoshi wa kumaliza kazi, hivyo ni bora kuwa na kiasi kwa kila kitu bila kusahau lililo la muhimu zaidi ambalo tutaliishi baada ya maisha yetu hapa duniani.
Sala:
Bwana, nisaidie niweze kukusikia wewe ukiniambia niache ninacho fanya niweze kupumzika katika pumziko lako Takatifu katika sala. Ninaomba niweze kuwa na muda huo kila siku wa kuwa nawe na kuzungumza nawe katika sala. Yesu nakuamini wewe.
Amina .
Maoni
Ingia utoe maoni