Jumapili, Septemba 17, 2023
Jumapili, Septemba 17, 2023
Juma la 24 la Mwaka wa Kanisa
YbS 27:30-28:1-7
Zab. 103:1-4, 9-12
Rum. 14:7-9
Mt. 18:21-35
KILA MKRISTU NI LAZIMA AWE TAYARI KUSAMEHE WENGINE
Ndugu Zangu, tumesikia neno la Mungu, katika masomo yote matatu. Kama nilivyowadokeza katika utangulizi wangu, kwamba masomo yote, yanaongelea jambo lilio muhimu, katika maisha yetu ya kikristu. Nalo ni kuhusu msamaha. Katika Injili tumesikia, Yesu akiwahitaji wafuasi wake, kuishi maisha ya kusameheana, hivyo nasi wakristo, tunawajibika kuyaishi maisha haya. Kila mkristu ni lazima awe tayari kusamehe wengine, wakati wo wote na bila masharti ye yote. Je, sisi nasi tupo tayari kusamehe? Ni rahisi sana kwetu kuzungumzia kuhusu neno msamaha, lakini linapokufika wewe inakuwa vigumu sana kulitekeleza.
Hebu, tusikilize tukio hili linalowahusu wanawake wawili waliokuwa marafiki wakubwa. Japo nyumba zao zilikuwa siyo karibu sana, lakini mara nyingi walikuwa pamoja. Siku moja kulitokea kutokuelewana baina yao. Kwa sababu ya mambo Fulani-Fulani waliyoyajua wao. Na tangu siku hiyo, urafiki wao ukafikia kikomo na wakawa maadui wakubwa. Viongozi wengi wa dini, waliokuwa wakiufahamu urafiki wao kindani, hasa mapadre, walijitahidi kadiri ya uwezo wao kuwapatanisha, lakini hawakufanikiwa. Ikatokea kuwa wakati wa mgogoro wao huo mimi niliamishiwa maeneo waliyoishi. Kwa vile, niliwafahamu vizuri hawa akina mama, mimi nami niliamua kujaribu bahati yangu ya kuwapatanisha. Hivyo siku moja, nilienda nyumbani kwa mmoja wao, na kuanza kuzungumzia kuhusu neno msamaha. Hususani kwa rafiki yake. Nilimsisitiza kuhusu kusamehe na kusahau tofauti zilizopo baina yao, ili urafiki wao uweze kuendelea. Mnajua alinijibu nini? He! Niko tayari kuingia katika moto wa jehanamu, lakini siyo kumsamehe.
Hivyo tunaweza kuona katika tukio hili ni jinsi gani, mwanamama huyu, alivyokuwa na hasira, na kwamba yupo tayari kwenda jehanamu, lakini siyo kumsamehe mwenzake. Kama hivyo ndivyo tulivyo, tunawezaje kuisema, ile sala aliyotufundisha BY? Ambayo ni sala ya Baba Yetu. Katika sala hii tunasema “utusamehe makosa yetu, kama tunavyowasamehe na sisi wale waliotukosea”. Hii, ina maana kwamba, tunamwomba Mungu atusamehe makosa yetu kama vile, sisi tufanyavyo kwa wenzetu. Hamna shaka NZ, ni wazi kwamba inatuwia vigumu sana kuwasamehe wale waliotusababishia matatizo katika maisha yetu. Lakini swali linabaki, tunaweza kuendelea na kinyongo chetu mpaka lini?
Katika somo la kwanza, tumesikia jinsi hasira na kinyongo vinavyoumiza. Hivyo tunasisitizwa kuwasamehe jirani zetu. Na katika Injili, Yesu anatukumbusha kuhusu kusameheana hasa pale anapomwambia Petro, samehe siyo mara saba tu, bali mara saba sabini. Hivyo na sisi, tunatakiwa kuwasamehe majirani zetu zaidi ya mara saba. Ili tuweze kufanya hivyo tunahitaji kufanya nini?
Kwanza kabisa, ni lazima tusali. Tumwombe Mungu atupe neema ya kuweza kusamehe na pia kusahau. Halafu mwombee na yule aliyekugadhabisha. Wakati Yesu anapotutia moyo wa kuwapenda adui zetu, huwa anatupa pia neema za kutenda hayo. Pili, hebu tujaribu kutafakari ni mara ngapi, Mungu ametusamehe sisi. Yeye ametusamehe mara nyingi zaidi kuliko anavyopenda, sisi kuwasamehe wenzetu. Mungu ni mwenye kusamehe, ni mwenye upendo na ni mwenye huruma kwa wale wote wanaokiuka maagizo yake. Sasa tujiulize ni kwa muda gani, sisi tutaendeleza hasira yetu kwa jirani zetu? Tatu, tujaribu kubadilisha msimamo wetu. Tujaribu kuangalia wale waliotukosea katika muonekano tofauti. Siyo kama adui zetu, bali kama wanadamu na kama tulivyo sisi. Sisi sote tuna vipaji vinavyofanana kama vile, kupenda na kutokupenda, hobi tofauti, muhono tofauti kuhusu mazuri na mabaya na mbaya zaidi tunawaumiza wenzetu, maneno na matendo yetu. Hivyo, pia jirani zetu kama tulivyo, sisi nao pia wanatuumiza kama sisi tunavyoumiza wengine. Ndiyo maana basi, sisi nasi tunahitaji kupata msamaha kutoka kwa wenzetu, kama wao wanaohitaji kutoka kwetu. Kwa hiyo ni jukumu letu kuwasamehe wale waliotukosea.
Yesu alipokuwa pale msalabani aliwaombea watesi wake, “Baba, uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo” (Lk 23/34). Yesu aliwaona hawa kuwa ni watoto wa Baba ambao wamepotea njia. Kwa hiyo, ni lazima na sisi tuanze kuwaona adui zetu kama vile Yesu alivyowaona watesi wake, na anavyotuona sisi leo hii. Anza leo kutekeleza haya. Omba neema ya kusamehe wengine, na kukumbuka huruma ya Yesu kwetu. Na muone jirani yako au mtesi wako kama ulivyo wewe. Hapo ndipo tutaweza kusamehe na kusahau kama atufanyiavyo Baba yetu wa mbinguni. Katika misa ya leo tumwombe Mungu atupe neema hii ili tuweze kuwa kielelezo bora cha ukristo wetu popote pale tutakapo kuwa.
Maoni
Ingia utoe maoni