Alhamisi. 21 Novemba. 2024

Tafakari

Jumamosi, Julai 23, 2016

Jumamosi, 23 Julai 2016,
Juma la 16 la Mwaka C wa Kanisa

Yer 7: 1-11;
Zab 83: 3-6, 8, 11;
Mt 13: 24-30


KUPALILIA MOYO!

Katika Injili tunamsikia Yesu akielezea kuhusu ngano na magugu. Bwana shamba amepanda mbegu njema, lakini adui akapanda magugu katika shamba lake. Mungu aliiumba mioyo yetu ikiwa na hali nzuri, uwezo wakuona mazuri na kuyafanya. Adui akapanda ndani yetu hali ya kutenda maovu, ambayo kwa njia ya hiyo mara nyingi tunakataa lililo jema, tufauti na hali ya kujitambua aliyotupa Mungu hapo awali na ahadi zake. Bwana shamba katika mfano huu anajua kwamba ni yule adui aliyeyafanya haya. Ana uvumilivu wakuyaacha yote mawili yakuwe pamoja, akijua kwamba pamoja na magugu bado anamatumaini yakupata matunda katika shamba lake.

Tunaposhindwa kutekeleza mapenzi na ahadi tulizomuahidia Mungu katika maisha yetu, tutambue kuwa Mungu anatuelewa sisi zaidi kuliko sisi tunavyofikiri. Anatumbua tamaa yetu ya ndani ya kutaka kumpendeza. Yeye pia anamatumaini kwamba pamoja na kuanguka kwetu bado tuna nafasi ya kuzaa matunda mema. Mbaya kwetu ni kama tutaruhusu ngano izidiwe na magugu, kwa kukata tamaa na kuacha kumrudia kila wakati tuangukapo. Lililo jema tusikate tamaa, kila wakati kujishughulisha kumrudia angalao tuoneshe matunda mema licha ya mahangaiko yetu yakujikuta katika hali ya dhambi kila wakati na hali ya kuweza kutenda dhambi ndani yetu.

Kila wakati tutambue Mungu ameruhusu muda uwepo wakutubu na kumrudia. Pengine tumeona mambo mengi yanatokea ambayo hayapendezi machoni petu, tunajiuliza kwanini Mungu asiingilie kati na kurekebisha mambo, tunajiuliza Mungu haoni? Kwanini Mungu anaruhusu wenye dhambi waishi na walio wema? Au kwanini wabaya wanawatesa watu wa Mungu? Pengine jibu tunalo katika Injili ya leo, yaache magugu na ngano yamee pamoja siku yaja kila mti utagundulika kwa matunda yake. Mungu hafurahii kuangamia kwa mtu muovu, anapenda wote watubu wamrudie yeye, yeye anaruhusu muda uwepo wakutubu ili tuweze kuzaa matunda mema, tutumie muda uliopo kujipatanisha na Mungu. Pengine tujiulize, Umeungama lini? Kama ni muda mrefu ni kwanini? Pengine una mpango ghani? Tutumie muda vizuri ndugu yangu. Tujipatanishe na Mungu daima. Tusiridhike na dhambi zetu.

Sala: Yesu, naomba neno lako lenye wokovu liondoe mzizi wa dhambi kutoka ndani kabisa mwa moyo wangu. Amina.

Maoni


Ingia utoe maoni