Jumatatu, Juni 12, 2023
Jumatatu, Juni 12, 2023
Juma la 10 la Mwaka
2 Kor 1: 1-7;
Zab 34: 2-9;
Mt 5: 1-12
HERI WALIO…..!
Yesu leo anaanza mazungumzo yake kwa maneno ya pekee ya heri. Zipo heri nane, kila moja ikianza kwa “heri walio..”. Yesu anatumia neno hili la heri ambalo kwa Kigirini ni Makarios ambalo ndani yake halibebi tuu furaha bali linabeba neno bahati nzuri ya kupata baraka maalumu. Kwahiyo tunaweza kusema, “heri walio…” au “Wanabahati kweli walio….”
Ufalme wake ni ufalme uliojaa huruma na msamaha. Na kama tutakavyokuwa tayari kuwasamehe wenzetu tutajikuta pia wenzetu wanatusamehe tunapo wakosea. Katika sala ya Bwana, ambayo ni sala ya Ufalme, huwa tunaomba hili, “tusamehe dhambi zetu kama na sisi tunavyo wasamehe waliotukosea”. Kwa kawaida ni vigumu sana kwa wale walio katika ufalme huu kutokusamehe, wao kawaida ni wepesi kusamehe na kukaribisha amani. Hii haimaanishi kwamba tuwatendee kila ubaya. Haki pia lazima iwepo. Kupinga na kukataa uovu haina maana ya kuacha kusamehe na kuponya vidonda vilivyo sababishwa na wengine.
Na huruma inayoeleweka katika nyanja ya kujali wengine ndio inayojenga Ufalme huu ndani ya mtu. Mtu huyu sio kwamba anaona huruma kwa wanaoteseka tuu bali anajua pia jinsi yakujiingiza katika matatizo ya wengine na kuhuzunika nao katika hali yao. Hii ndio sifa aliokuwa nayo Yesu katika hali zote. Aliingia katika maisha ya watu na kukaa nao na kuleta furaha na matumaini mapya.
Sala:
Nisaidie niweze kuwa mpole na mwenye huruma, maskini wa roho, mwenye kuleta Amani na mtu mwenye kukubali mateso. Nisaidie mimi niweze kupokea kwa shauku na kwa furaha ufalme wako. Yesu nakuamini wewe.
Amina
Maoni
Ingia utoe maoni