Ijumaa. 29 Machi. 2024

Tafakari

Jumanne, Aprili 18, 2023

Jumanne, Aprili 18, 2023
Juma la 2 la Pasaka

Mdo 4: 32-37
Zab 92: 1-2, 5
Yn 3: 7-15


KUZALIWA UPYA!


Sehemu ya Injili ya leo inafunga kwa kuonesha Yesu akijilinganisha mwenyewe na yule nyoka wa shaba katika jangwa la Sinai (Hes 21:9). Wayahudi wale wote walionyanyua macho yao na kumtazama yule nyoka wa shaba waliponywa na madonda na maumivu wa wale nyoka wa moto. Sisi ambao tunatazama kwa Imani kwa Yesu tunapaswa kupata maisha mapya sasa. Kama vile Kristo alivyoteseka na kuingia katika utukufu hata wafuasi wake pia watapatwa na hayo hayo. Hakuna njia nyingine. Maisha ya Mkristo yanabeba mateso, yananabeba pia kufa kinafsi lakini macho yote ambayo yamekazwa kwa Yesu yanaondoa mashaka yote.

Leo pia katika somo la kwanza tunaona pia jumuiya ya kwanza wakiamua kuchagua kuishi pamoja maisha ya ufukara uliojaa upendo wa ajabu. Walikubali hata kuvunja ile hali ya kuwa na mali binafsi na kuamua kuwa na vitu vyote katika umoja. Hali hii liliwezekana kwasababu waliungana kwa moyo mmoja na roho mmoja katika Kristo ambaye wote walimwamini na kumuishi katika maisha yao. Wakristo wasasa sio wote waliotayari kutoa mali zao kwasababu ya Kristo, kanisa halimlazimishi mtu kufanya hivyo ila ni lazima mtu aguswe mwenyewe kutoka moyoni. Lakini kilicho cha muhimu kabisa ni kuhakikisha parokia zetu na nyumba zetu za kitawa pia zinabaki katika moyo mmoja na roho mmoja katika Kristo. Kujitoa kwa hali zote na kukamilishana na kuleta furaha katika jumuiya yetu ya kuabudu pamoja. Inapendeza kabisa kuona kama Parokia inakuwa na hii hali ya moyo mmoja na roho moja katika Kristo.

Wengi wetu tunamfahamu Mungu kwa njia ya pilli. Tunamfahamu Mungu kwa yale ambayo tumeambiwa na wengine au yale ambayo tumesoma kutoka katika vitabu, nk. Moyo mmoja na Roho moja katika Kristo inakuja kwa kuona upendo wa Yesu aliokufa na kufufuka kwa jili yetu. Tunaona upendo huu kwa kukubali kuzaliwa upya katika maisha mapya. Ni kwa njia ya kujikita katika huo upendo wa Mungu unaobadilisha na kuwa wapya. Tunamuomba Mungu tuzaliwe upya kwa maisha mapya na kubaki katika upendo wa Kristo.

Sala:
Njoo, Roho Mtakatifu na utufanye upya.
Amina.

Maoni


Ingia utoe maoni