Jumanne. 16 Aprili. 2024

Tafakari

Jumatatu, Aprili 17, 2023

Jumatatu, Aprili 17, 2023
JUMA LA PILI LA PASAKA

Mdo. 4:23-31
Zab. 2:1-9 (K) 13
Yn. 3:1-8

KUZALIWA MARA YA PILI KWA MAJI NA KWA ROHO

Ndugu zangu karibuni kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi hii ya leo. Sasa tumemaliza octava ya pasaka na habari tulizokuwa tunazisikia katika octava hii hasa katika injili zilihusu ufufuko, asubuhi ile jinsi Yesu alivyofufuka na kuiletea dunia furaha. Hivyo kila siku kwenye ile octava katika injili tulisikia habari ya Yesu kufufuka, asubuhi ile siku ya kwanza ya juma. Sasa, hiki kipindi kingine cha pasaka, tunaanza kusikia zaidi maana ya ufufuko na umuhimu wake na namna tuwezavyoshiriki katika ufufuko.

Hivyo, injili zitakazokuwa zinatumika zitatoka sehemu mbalimbali, sio lazima ziwe juu ya ile siku ambapo yesu alifufuka. Mfano, katika injili ya leo, tunakutana na mazungumzo kati ya Yesu na Nikodemus na Yesu anamwambia Nikodemo kwamba ili mtu kuurithi ufalme wa mbinguni, yabidi kuzaliwa mara ya pili kwa maji na kwa Roho-yaani yabidi kubatizwa, kumpokea Kristo na Roho mtakatifu atakayekufanya kuwa kiumbe kipya na kukufikisha mbinguni. Kwa namna nyingine, Yesu anamweleza Nikodemo kwamba yeyote anayetaka kwenda mbinguni, ni lazima akubali kuifia dhambi na kuiacha katika kaburi kama Yesu alivyofanya ili aweze kufufuka pamoja na Yesu na kuwa kiumbe kipya. Huo ndio ufufuko Yesu anaotueleza leo.

Katika somo la kwanza, tunaona kwamba wanafunzi wa Yesu walikuwa wanapigana ili watu waupate ufufuko huu, ili watu waache dhambi na kukubali kubatizwa na kumpokea Kristo. Huu ndio ufufuko ambao hata Yesu anamweleza Nikodemo. Mitume tunaowasikia katika somo la kwanza walipambana kweli kweli kuhakikisha kwamba wanahubiri, wanaambia watu waache dhambi na kumpokea Kristo na kubatizwa na kuwa viumbe vipya. Walitetea ufufuko huu hadi wakakubali kupelekwa gerezani ambako walichapwa na leo wanafunguliwa na wanapokutana na wakristo wenzao, wanamuomba Mungu aendelee kuwapa nguvu ya kufundisha ufufuko huu. Wanamuomba pia Mungu awape nguvu ya kutenda miujiza ili watu wapate kuamini na kumpokea zaidi Kristo na kweli walijitahidi na kufanikiwa sana katika hili.

Katika hili tunalokubwa la kujifunza ndugu zangu. Sisi lazima tukubali kuwa wahubiri wa ufufuko wa Bwana, yaani tuwaambie watu waache dhambi na kumpokea Kristo. Kwa kweli duniani tunavumiliana sana na kuruhusu dhambi zitendeke tena mbele ya macho yetu. mfano: unakuta mimi natambua kwamba mfanyabiashara wa maziwa huongeza maji katika maziwa yake ili apate faida awauziapo watu. Lakini mimi nakaa kimya na kuruhusu watoto wanaonunuliwa yale maziwa wanywe maji tu na kupatwa utapia mlo, ninapaswa kumwambia huyu mfanyabishara rafiki yangu kwamba acha tabia hizi, tusijidai kulindana lindana.

Au unakuta kwamba nafahamu kabisa mtu fulani duka lake yeye ananunua bidhaa za magendo zilizofeki na kuja kuwauzia watu. Mimi nakaa kimya, mwisho wa siku watu wanauziwa simu feki, vifaa vya umeme feki na betri feki. Au mimi katika duka langu najua kabisa bidhaa ninayomuuzia huyu mtu ni feki lakini nakaa tu kimya. Jamani hapa duniani tuoneane huruma, tulindane, tusikubali wengine wadhulumiwe au kupatwa na shida. Namna hii ndiyo tuwezayo kusema kwamba hakika tunaishi ufufuko tulioletewa na Kristo. Tumsifu Yesu Kristo.

Maoni


Ingia utoe maoni