Ijumaa. 19 Aprili. 2024

Tafakari

Jumapili, Machi 26, 2023

Jumapili, Machi 26, 2023
Juma la 5 la Kwaresima

Eze 37: 12-14;
Zab 130: 1-8;
Rum 8: 8-11;
Yn 11: 1-45.


WATU WA UFUFUKO


Giza, na ukimya, vilifunika kifo kadiri ya tamadunii za Wayahudi. Ni vigumu kupata maelezo kuhusu kutoharibika kwa roho au ufufuko wa wafu katika Agano la Kale. Ayubu alisema “kuna matumaini kwa mti; kama ukikatwa unaweza kuchipua tena, machipukizi mapya yatatokea tena. Lakini mwanadamu anavyokatwa, huanguka chini na huvuta pumzi yake ya mwisho-atakuwa wapi? Maji ya bahari yanaweza kutoweka, mito kukauka, lakini yule anayelala chini hawezi kuamka tena; mbingu zitaisha kabla hajaamka, kabla hajaamka usingizini.” (Ayubu 14:7-12). Biblia ilihifadhi kumbukumbu ya jinsi jambo lilivyokuwa gumu ili kutukumbusha ni kwa jinsi ghani giza lilitisha katika kaburi, kabla ya ufufuko na mwanga wa Pasaka duniani. Lakini pia mzaburi analeta matumaini. “Nijapopita katika giza la mauti, sintaogopa mbaya, kwani wewe Bwana wa uhai utakuwa pamoja nami”

“Kifo” kinaonekana kutisha kwa watu wengi, lakini ni wazi kwamba hakuna kitu tulicho na uhakika nacho katika maisha zaidi ya kifo. Wengi wetu tunazungukwa na hofu, baada ya kifo kuna nini? Wafuasi hawakuwa na tofauti. Hali yote inayo wazunguka inaonekana kutisha, na kwa upande mwingine Yesu anatabiri kuwa kifo chake kipo karibu na kwa upande mwingine wanawaogopa Wayahudi amabao walitaka kumpiga Yesu mawe mpaka afe. Kwa kipindi hichi tunaona jibu laTomasi lilivyo na mashaka “twende na sisi tukafe pamoja naye”. Ni hakika kwamba hofu ya kifo iliwakumba wafuasi. Yesu kwa kumfufua Lazaro kutoka wafu anataka kuwafunulia mitume na watu wengine kwamba yeye ni nani “YEYE NI UFUFUO NA UZIMA”.

Kifo ni nini?
Katika Injili ya leo, Yesu anakwepa kutumia neno ‘kufa’ badala yake anatumia ‘kupumzika’ akionesha kifo cha Lazaro. Kifo kilionekana kuwa ni kitu hasi na pia mwisho wa kitu. Lakini Yesu kwa kutumia neno “kupumzika’ anataka kuwaambia wafuasi kwamba kifo sio mwisho wa kila kitu, bali njia ya kupitia kutoka hali moja kwenda hali nyingine ya maisha. Kifo ni njia ya kupitia kutoka maisha haya ya duniani kuelekea maisha ya milele, njia ambayo imefunguliwa kwa ufufuko wa Yesu.

Ufufuko ni nini?
Wayahudi waliamini kwamba ni Mungu mwenyewe anaweza kurudisha uhai. Yesu anatumia kifo cha Lazaro kuonesha kweli yeye ni mwana wa Mungu, kwa kumfufua kutoka wafu. Lazaro ambaye alikuwa amekufa kwa siku nne, sasa anakuwa hai. Lazaro aliyekuwa amekufa sasa anatembea kutoka kaburini. Wayahudi waliamini kuhusu ufufuo wa wafu lakini ilikuwa mpaka dunia itakapopita. Na hapa wanaona kitu ambacho kina washangaza, mtu ambaye alikuwa amekufa kwa siku nne, anakuwa hai tena. Walio shuhudia waliamini kabisa Yesu sio nabii wa kawaida wala mwalimu wa kawaida bali Mungu mwenyewe. Yesu anaendelea kuonesha kwamba ufufuko sio tukio baada ya kifo, bali linaanza duniani kwa kuishi ukiwa umeunganika na Yesu.

Katika somo la kwanza katika kitabu cha nabii Ezekieli, anatangaza tukio ambalo Mungu anaenda kulitenda, muujiza wa ajabu. Mungu analeta uhai katika mifupa iliokauka. Mungu atafunua makaburi ambayo walikuwa wamefungwa, atawafanya watoke katika makaburi yao na kuwaongoza tena katika Nchi yao. Roho wa Mungu aliingia kila mahali na maisha yakaanza. Yalianza wakati wa mwanzo wa dunia, wakati Mungu anamuumba mwanadamu kutoka mavumbini, alimpulizia pumzi ya uhai na mwanadamu akaishi (Mwa 2:7). Hakuna kinacho shindikana kwa Roho wa Mungu. Anaweza kuleta maisha pia hata katika mifupa iliyo kauka kabisa.

Katika somo la pili, Paulo anatuambia, Yesu akiwa mtu kama sisi, alikufa. Lakini alifufuka. Yesu ana Roho kamili wa Mungu, ni kwamba ana ndani yake uhai wa Kimungu ambao hauwezi kufa. Yesu alikuwa na uhai huu wa Kimungu ndani yake. Roho wa Mungu alimfufua, na kumtambulisha katika utukufu wa Baba. Wale walio batizwa katika roho wake, katika maisha yake, hawafi tena. Maisha yetu katika ulimwengu huu yataisha, yatafika mwisho, lakini haitakuwa mwisho wa kila kitu. Roho aliye mfufua Yesu atatufua na kuipatia uzima wa milele miili Yetu inayo kufa.

Mkristo haamini katika kifo na ufufuko kama kitu ambacho kitatokea mwisho wa dunia. Ana amini kwamba mtu aliyekombolewa na Yesu hafi. Yesu alitangaza kwa Martha kwamba “kila anaye niamini mimi hatakufa kamwe”(Mtari wa 26). Pasaka inakaribia ni majuma mawili tu yajayo, na waliyo wengi tunatazama ufuko kama tukio litakalo tokea baadae. Tunashindwa kuishi kama watu wa ufufuko. Kwaresima inaonekana kama maombolezo, kujinyima, toba, lakini kwa hakika kwaresima ni kipindi cha kujifunza jinsi ya kuishi maisha ya ufufuko. Yesu amekuja kutukomboa sisi, sio tu baada ya kifo chetu bali pia tukiwa hai. Tukiwa na matumaini na tukiishi Imani katika ufufuko tuishi kama watu wa ufufuko kuanzia leo. Na yeye aliyempa Lazaro uhai kwa hakika atatupa sisi uhai, uhai tele.

Sala:
Bwana, wewe ni ufufuo na uzima. Nisaidie niondokane a muonekano wangu mbaya kuhusu uzima na kifo. Ninaomba nikuwe katika Imani ya roho wa uzima aliye ndani mwangu. Ninakuomba niweze kutambua Uzima wa Kimungu ndani mwangu. Ninaomba nitoke katika hofu zangu, na kwenda katika maisha ya ufufuo. Yesu, nakuamini wewe.
Amina

Maoni


Ingia utoe maoni