Jumamosi. 23 Novemba. 2024

Tafakari

Alhamisi, Machi 16, 2023

Alhamisi, Machi 16, 2023
Juma la 3 la Kwaresima

Yer 7:23-28;
Zab 95:1-2, 6-9;
Lk 11:14-23


JE, TUME NYAMAZISHWA KUHUBIRI INJILI?


Leo, katika Injili Yesu analaumiwa kwa kutoa pepo kwa kutumia mkuu wa pepo. Wapinzani wa Yesu walishindwa kuona kidole cha Mungu ndani ya Yesu kwa huruma yake kwa wagonjwa. Hali hii inaonesha wazi kutokuamini kwa Mafarisayo na viongozi wa Wayahudi kwamba Yesu ni Masiha. Injili ya leo inaongeleo mtu ambaye alikuwa bubu kwasababu ya pepo. Wakati pepo alivyotolewa na Yesu, huyu mtu aliyekuwa bubu alianza kuongea, watu wakashangaa sana. Ni hakika kwamba huyu pepo alikuwa amemshika huyu mtu kiasi kwamba alikandamizwa kabisa mpaka akashindwa kuongea. Baada ya kuwekwa huru kutoka katika huyu pepo, ana anza kuongea kwa uhuru.

Ingawaje hatuwezi kuhisi uwepo wa pepo katika hali kama hii, lakini katika hali fulani tunakutana na ukandamizaji kama wa huyu pepo wa kutufanya tubaki kimya. Yule muovu anajaribu kutuogopesha kiasi kwamba tunakuwa waoga kutangaza Injili kwa uhuru na kwa uaminifu, na kwa jinsi Mungu anavyopenda ujumbe wake uwafikie watu. “pepo wa ububu” anaweza kututawala, kutuchanganya au kutujaza hofu fulani wakati muda umefika wa kushirikisha Imani yetu na wengine. Ingawaje ni vigumu kuanguka moja kwa moja mikononi mwao, lakini mara nyingi tunajaribiwa kila mara na wao. Yesu ana nguvu kamilifu juu ya pepo wa aina zote, yeye hasiti kuwanyamazisha pepo hao kama ukimruhusu. Yesu anataka kutuweka huru ili tuweze kuongea kwa kuhubiri neno lake la upendo bila kujibakiza ili wengine waweze kumfahamu yeye na upendo wake mkamilifu. Mwache yeye akutumie kama moja ya chombo cha ukweli na upendo.

Sala:
Bwana, wakati mwingine naingiwa na hofu na kuwa kimya na kushindwa kutangaza neno lako vizuri kwa wale wahitaji. Wakati mwingine nahisi kama nimefungwa kinywa kuongea, au kuchanganyikiwa niseme nini. Bwana naomba unifungue kinywa changu niweze kuongea, Bwana wangu, ili niweze kuwa chombo chako kitakatifu cha neno lako na kwa ujasiri na uaminifu niweze kutangaza neno lako kwa wote walio wahitaji. Yesu, nakuamini wewe.
Amina

Maoni


Ingia utoe maoni