Jumamosi. 23 Novemba. 2024

Tafakari

Jumamosi, Februari 11, 2023

Jumamosi, Februari 11, 2023
Juma la 5 la Mwaka wa Kanisa

Kumbukumbu ya Bikira Maria wa Lurdi na Siku ya kuwaombea Wagonjwa Ulimwenguni

Mwa 3:9-24;
Zab 90: 2-6, 12-13;
Mk 8: 1-10.

Au (Masomo ya kumbukumbu)
Is 66:10-14;
Jdt 13: 18-19;
Yn 2: 1-11.

JE UNA NJAA YA MUNGU?

Sehemu ya Injili inaweza kuonekana katika hali mbali mbali inayo funua huruma ya Yesu. Kulikuwa na mkusanyiko mkubwa ulio wahusianisha Wayahudi pia Wayunani, waume na wake pamoja na watoto. Na wote walikuwa na kitu kimoja tu muhimu. Walikuwa na njaa. Walikuwa na njaa ya mafundisho ya Yesu-ni kitu kipi kingine kinacho weza kuwaweka pamoja namna ile kwa siku tatu? Na kwasababu ya njaa yao ya kiroho, walihisi pia njaa ya kimwili. Je, ulishawahi kuwa na njaa ya Mungu? Ulishawahi kuhisi kutaka kuwa na Mungu zaidi ya kutaka kukaa mahali na kupata mambo mengine ya maisha?

Umati walikuwa wamevutwa sana na Yesu kiasi kwamba walikaa siku tatu wakiwa naye, wakimsikiliza wakiwa katika jangwa pamoja na kwamba hawakuwa na chakula. Walimchagua Yesu zaidi ya chakula na faraja ya nyumbani kwao. Inaonesha ni kwa jinsi ghani walivyokuwa wamevutwa naye. Hakuna kitu kingine kilichokuwa na thamani, walitaka tu wawe na Yesu. Ujumbe huu pia unaonesha jinsi Yesu alivyo onesha kujali watu. Moyo wake ulijazwa na huruma juu yao. Alifurahi pia kwa uwepo wao lakini pia alijali pia kuhusu usalama wao wa mwili hata kuliko wao wenyewe. Yesu, baada ya kutambua tatizo la watu kuwa bila chakula kwa muda mrefu anawaalika pia Mitume wake watambue tatizo hilo. Pengine, Yesu alitaka mitume waweze kuwa na upendo na kujali watu katika mioyo yao. Pengine, ilikuwa ni wakati ambapo alikuwa akiwajaribu na kuwafundisha wawe wakiwaza kuhusu mahitaji ya watu. Yesu alitaka mioyo yao isukumwe na “huruma kwa ule umati” kama yeye alivyokuwa.

Tuangalie pia leo: je, Yesu ni kiini cha maisha yako? Je, mioyo yetu inasukumwa na tamaa ya kutaka kuwa naye zaidi ya chochote kile? Je, tunatambua jinsi Yesu anavyo tujali? Je tupo tayari kuruhusu upendo na huruma anayo tupa Yesu, kuipeleka kwa wengine pia? Ni kwa jinsi hii tu twaweza kuitwa wafuasi wake.

Sala:
Bwana, nisaidie niweze kuvutwa kwako kwa tamaa kubwa kabisa. Nisaidie niweze kukuona wewe kama kiini na chanzo cha yote ninayo tafuta. Ninaomba nikuchague wewe zaidi ya yote, nikikuamini wewe na kufahamu kwamba wewe ndiye utakaye ridhisha hamu ya moyo wangu. Nikiwa navutwa kwako nisaidie moyo wangu ujazwe na huruma nyingi kwa wote. Yesu, nakuamini wewe.
Amina.

Maoni


Ingia utoe maoni