Jumamosi. 23 Novemba. 2024

Tafakari

Jumanne, Februari 07, 2023

Jumanne, Februari 7, 2023
Juma la 5 la Mwaka wa Kanisa

Mwa 1:20 - 2:4;
Zab 8: 4-9;
Mk 7: 1-13.

KENGELE YA KANISA!


Kengele ya Kanisani inalia kuwata watu waingie kanisani lakini yenyewe haiingii. Ni hivyo pia matendo yetu yaweza kuwaongoza watu kwa Mungu lakini, kumbe sisi wenyewe tupo mbali na Mungu. Katika Injili ya leo, waandishi na Mafarisayo wanawatuhumu wanafunzi wa Yesu kwa kuvunja mapokeo ya wazee kwa kutokunawa mikono yao kabla ya kula milo yao. Yesu alikemea unafiki wao, kwa kunukuu maneno ya nabii Isaya. Wanafiki hukiri jambo moja na hufanyia mazoezi kitu kingine. Wanakiri kwa midomo yao kwamba wanamwabudu Mungu na kufuata amri zake, lakini katika maisha yao halisi wanaishi kinyume na amri za Mungu. Ni watu ambao ni watakatifu mbele za watu, lakini sio watakatifu mbele za Mungu. Watu huona matendo ya nche na kuhukumu, lakini Mungu aichunguzaye mioyo, hutoa hukumu ya mtu toka ndani. Ibaada ya wanafiki ni ya bure kabisa. Huweka mioyo yao mbali na Mungu na kumwabudu, hawatoi sifa kwa Mungu wala haiwaletei baraka. Mungu hapendezwi na sadaka au matoleo au sala au Sakramenti, wakati mioyo ipo mbali naye (Isa 1:15). Tumwombe Mungu atusaidiye tumtukuze yeye kweli kwa matendo yetu na maneno yetu, tuishi kweli tunachokiamini, ili sifa na utukufu ziwe kwa Mungu na isiwe kwaajili ya utukufu wetu binafsi.

Je, ni ujumbe ghani muhimu ambao tunaopaswa kuuchukua kwa ajili yetu wenyewe? Tunapaswa kujifunza mambo mawili ya kweli. Kwanza kabisa, mapenzi ya Mungu yanapaswa kuendesha maisha yetu na kuwa chanzo cha kila kitu. Mapenzi yake, sheria zake, ni msingi wetu. Mungu ameanzisha ukweli kama msingi wa maisha ya mwanadamu na tunapaswa kukumbatia sheria zake kwa unyenyekevu. Ukweli wake ni pamoja na yote yaliofunuliwa kuhusu Imani yetu, katika maandiko matakatifu na katika Kanisa, na yote tunayosikia Mungu akiongea nasi katika maisha yetu. Mafarisayo kwa kukosa unyenyekevu, hawakuweza kuona ukweli huu. Na badala yake, wakashikilia mawazo yao na mitazamo yao pekee. Mungu anawahukumu kwa kukosa mapendo katika hili.

Pili, tutambue kuwa tunapo kumbatia sheria ya utakatifu, na mapenzi yake katika maisha yetu, tutakuwa wasafi moyoni na tutakuwa huru kumpenda hata kwa muonekano wetu wa nje. Tuta mwabudu kutoka moyoni na haya yataonekana katika maneno yetu na matendo yetu. Lakini hili haliwezi kutokea kama hatutaanza na sheria yake ya Kimungu.

Sala:
Bwana, nisaidie niweze kupenda sheria yako Takatifu. Nisaidie niweze kuikumbatia kwa moyo wangu wote. Nina amini yote uliyo ongea tangu miaka yote. Nina amini yote unayo ongea ndani ya moyo wangu kuhusu maisha yangu. Nipe neema niweze kukumbatia mapenzi yako matakatifu, na katika kushikana nayo, niweze kubadilishwa ndani na nje. Yesu, nakuamini wewe.
Amina

Maoni


Ingia utoe maoni