Jumamosi. 23 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatano, Disemba 07, 2022

Jumatano, Desemba 7, 2022
Juma la 2 la Majilio

Kumbukumbu ya Mt. Ambrosi, Askofu na Mwalimu wa Kanisa

Isa 40: 25-31;
Zab 103: 1-4, 8, 10;
Mt 11: 28-30.



TUKABIDHI MIZIGO YETU TUPATE PUMZIKO KWA YESU!


Kuna hadithi maarufu ya mtu ambaye alikutana na kijana wa kiume akiwa amembeba mtoto mlemavu mgongoni mwake. Yule mtu alitamka, “huo uubebao ni mzigo mzito.” Yule kijana wa kiume alijibu, “Huu sio mzigo; huyu ni mdogo wangu!” hakuna mzigo ulio mzito kama utakuwa umebebwa kwa upendo. Yesu ametufundisha sisi nguvu ya upendo kupitia maneno yake na mifano yake. Katika ufalme wake, dhambi hazisamehewi tu bali zinafutwa kabisa, na uzima wa milele hutolewa kwa watu wake wote. Ni Yesu pekee anaweza kuinua mzigo wa dhambi na uzito wa kupoteza tumaini kutoka kwetu. Yesu anatumia mfano wa nira kuelezea ni namna gani tunaweza kubadilisha mzigo wa dhambi na kupoteza tumaini kuwa utukufu na nira ya uhuru dhidi ya dhambi.

Kipindi cha majilio kinatukumbusha kwamba Mungu Mwana alikuja duniani na akachukua hali ya ubinadamu wetu. Lakini ingawaje hakutenda dhambi, yeye aliruhusu kubeba mzigo wa dhambi zetu. Ili yeye kama Mungu, aweze kutuangalia nakutuambia kwamba anaelewa ni nini maana yake kwasababu yeye mwenyewe amebeba mzigo huo kwa ajili yetu. Aliingia katika hali hii kwasababu ya upendo aliokuwa nao kwetu ili atusaidie na sisi kuvumilia, kwa furaha, tunapokumbana na maisha yetu ya kila siku.

Je, ni namna gani tunaweza kujiweka katika nira ya mkombozi? Jibu linapatikana katika amri ‘jifunzeni kutoka kwangu’. Anatuita tutumikie, lakini tunafanya kazi hiyo na kuhudumia kwa nguvu atukirimiazo. Daima Yeye yupo karibu nasi kutupunguzia mizigo. Hili litafanyika kama tu tutayakabidhi maisha yetu kwake. Mizigo inakuwa mizito na haibebeki pale tu tunapojaribu kuichukua wenyewe, au kuimudu sisi wenyewe. Je, unauamini upendo wa Mungu na kukubali mapenzi yake katika maisha yako?

Sala:
Bwana, nakabidhi maisha yangu kwako na yote nilio nayo kwako. Ninakubali mwaliko wako. Asante kwa huruma yako na kunijali mimi kila wakati. Yesu nakuamini wewe.
Amina

Maoni


Ingia utoe maoni