Jumapili. 19 Mei. 2024

Tafakari

Jumamosi, Januari 28, 2017

Jumamosi, Januari 28, 2017,
Juma la 3 la Mwaka wa Kanisa

Kumbukumbu ya Mt. Tomas wa Akwino, Padre na Mwalimu wa Kanisa

Ebr 11:1-2, 8-19;
Lk 1: 69-75;
Mk 4: 35-41


KUMWAMINI YESU KWA MAISHA YETU!

Bahari na mawimba yana mtii Mungu kwasababu ni sehemu ya uumbaji wake. Na wala hakuna tatizo kubwa sana kwa Mungu ambalo anashindwa kulitatua. Hofu zetu hazina mwisho, matatizo yetu yanatusumbua, kwasababu sisi wenyewe tumechagua kuyakabili wenyewe kwa nguvu zetu. Wafuasi walikuwa ni watu wa kawaida kama sisi. Hata wakiwa kati ya Yesu wana ogopeshwa na gharika! Laiti kama Mwanadamu angelijua kukabidhi hofu zake na maumivu yake kwa Mungu!

Ni rahisi sana kukata tamaa katika maisha. Ni rahisi zaidi kuelekeza mwelekeo wote kwenye matatizo na kuacha mengine yanayo tuzunguka. Hata kama ingekuwa ni maneno ya hasira na ya kuumiza kutoka kwa wengine, matatizo ya kifamilia, matatizo ya umma, ukosefu wa fedha nk. Kuna kila sababu ya kila mmoja wetu kuanguka kwenye mtego wa hofu, kuchanganyikiwa, kuumia na kuwa na shauku. Lakini ilikuwa ni kwasababu ya sababu hizi Yesu aliruhusu tukio hili litokee akiwa na wafuasi wake. Alikuwa kwenye boti na wafuasi wake akaruhusu wafuasi wakumbwe na gharika kuu, wakati yeye akiwa amelala, ili aweze kuleta ujumbe wa kufaa kwetu sisi wote.

Katika habari hii, wafuasi walilenga kwenye kitu kimoja tuu: walikuwa waangamie! Bahari ilikuwa ikiwasukasuka na waliogopa maangamizi makubwa! Lakini kwa kupitia yote hayo, Yesu alikuwa pale akionekana amelala, akiwasubiri waweze kumwamsha. Na walipo mwamsha, alikemea gharika na hali ikawa shwari. Hili ni kweli pia katika maisha yetu. Sisi mara nyingi tunaruhusu matatizo mengi tunayopata yatutese na kutusukasuka. Ufunguo ni kwamba tunapaswa kugeuza macho yetu na kumwelekea Yesu. Muone mbele yako amelala, anakusubiri umwamshe. Yupo daima, akikusubiri na yupo tayari daima. Kumwamsha Bwana wetu ni rahisi kama ilivyo rahisi kugeuza macho yetu kutoka katika gharika na kusadiki uwezo wake wa Kimungu. Yote ni kuwa na Imani kwake tu. Imani kamili. Je, una mwamini yeye? Tumwache Yesu achukue nafasi ya kila kitu katika maisha yetu tuliopo. Anatupenda na kweli atatujali wote.

Sala: Bwana, ninakugeukia katikati ya changamoto za maisha na ninatamani kukuamsha uje katika maisha na kunisaidia. Ninatambua upo daima karibu yangu, ukinisubiri mimi nikuamini wewe kwa kila kitu. Nisaidie nielekeze macho yangu kwako na kuwa na Imani kamili katika mapendo yako. Yesu, nakuamini wewe. Amina.

Maoni


Ingia utoe maoni