Jumamosi. 23 Novemba. 2024

Tafakari

Ijumaa, Oktoba 28, 2022

Ijumaa, Oktoba 28, 2022,
Juma la 30 la Mwaka wa Kanisa

Sikukuu ya Wat. Simoni na Yuda, Mitume.

Ef 2:19-22
Zab 18:2-5
Lk 6:12-16

UMOJA KATIKA WINGI !

Mungu humwalika mwanadamu daima katika kazi yake ya ukombozi. Yesu aliwachagua watu wa kawaida kabisa wa kipindi chake kuwa mitume wake. Anawapa nguvu na mamlaka na wakawa waaminifu katika kuendeleza kutimiza mapenzi ya Baba. Luka, anatuambia Yesu alienda mlimani kusali, na alikesha usiku kucha katika kusali. Ndipo baada ya kusali anawachagua mitume kumi na mbili. Na kati ya hao wawili ndio tunafanya sikukuu yao leo, Simoni na Yuda. Habari za hawa wawili zijulikanazo ni chache sana. Tunajua walichaguliwa na Yesu kuwa mitume wake. Mtume ni yule anayetumwa. Hawa walishirikiana kufanya kazi pamoja katika nchi ya Uajemi na huko waliuawa kwa ajili ya Kristo. Kwasababu hiyo sikukuu yao huadhimishwa pamoja. Mtume simoni aliitwa ‘Zeloti’ maana yake mwenye bidii kwasababu alifanya bidii kutangaza ujumbe kuhusu Yesu kokote. Mtume Yuda aliitwa ‘Tadayo’maanake ‘hodari’ili kumtofautisha na Yuda Iskarioti msaliti. Alikuwa ndugu yake Yakobo mdogo kama tunavyosoma katika Injili na kama anavyosema mwenyewe katika barua yake ‘Barua ya Yuda’na barua hii iliandikwa kwa ajili ya makanisa yaliokuwa karibu na nchi Takatifu kama alivyofanya nduguye Yakobo.

Unaweza kufikiria ni watu wa namna ghani aliokuwa nao Yesu. Petro aliyekuwa msemaji na mwenye hofu lakini bado Yesu alimchagua kuongoza. Yakobo na Yohane waliokuwa wakipigania kuwa karibu na Yesu katika ufalme walio utafsiri vibaya; Mathayo mtoza ushuru, nk. Tunaweza kufikiria kukaa kwao pamoja kulikuwa je hapo mwanzo. Pamoja na kutoelewana wao kwa wao waliponywa na upendo usiozuilika wa Yesu alioutoa kwao.

Somo la kwanza linamalizia vizuri kabisa: “tangu sasa ninyi si wageni tena wala wapitaji, bali ni wenyeji pamoja na watakatifu, watu wa nyumbani mwake Mungu”. (Efe 2:19). Je, tupo tayari kumruhusu Yesu atujenge kama watu wa nyumba yake, hata ikiwa nikuwa pamoja na wale tusiowapenda?

Sala:
Bwana Yesu, ninaomba upendo wako unipe nguvu kuwakubali wenzangu kama walivyo.
Amina.

Maoni


Ingia utoe maoni