Jumapili, Oktoba 23, 2022
Jumapili, Oktoba 23, 2022
Dominika ya 30 ya Mwaka C wa Kanisa
YbS 35: 12-14, 16-18
Zab 34: 2-3, 17-19, 23
2 Tim 4: 6-8, 16-18
Lk 18: 9-14
KUKUBALIWA NA MUNGU!
Katika somo la kwanza, nabii Yoshua Bin sira, anawaonya matajiri na viongozi waliowakandamiza wanyonge, yatima na wajane. Tena wakichukuwa mali zao nakujipatia utajiri, huku wakitolea sehemu ya mali hiyo ya udhalimu kama sadaka yao kwa Mungu. Nabii anawaandikia, nakuwaambia Mungu hapokei sadaka ya namna hiyo. Sadaka zitokanazo na udhalimu na uonevu wa wanyonge na maskini hazina kibali machoni pa Mungu. Kilio cha yatima na wajane kinamfikia Mungu haraka kabisa, anawaasa watu hao kuacha hali hiyo kwani Mungu hatakawia kujibu sala za wanyonge wake. Mungu yupo karibu na maskini na wanao onewa daima. Wanapo mwita yeye huja mara. Na zaidi sana anawaeleza kwamba sala ya mtu mnyenyekevu hupasua mawingu na haitatulia mpaka itakapo mfikia Mungu. Kumbe tunapo mwendea Mungu kwa moyo wa unyenyekevu na wa kweli, sala yetu hupenya na kumfikia yeye.
“Mungu huwapinga wenye majivuno, lakini huwapa neema wanyenyekevu” (1 Pt 5:5). Injili ya leo ni Injili ambayo kila Muumini anapaswa kuwa makini kwa karibu kabisa. Ni kuhusu juu ya mfano aliotoa Yesu wa waamini wawili, Mfarisayo na mtoza ushuru. Ni vizuri kutambua kuwa wote wawili walikuwa waumini waliokuwa wakisali kwa Mungu mmoja, ni vizuri pia kutambua wote walikuwa katika dini moja na wote walikuwa katika kanisa(sinagogi) moja. Wote walikuwa ni waamini wanaoingia katika sinagogi na kusali sala za kila siku. Lakini sisi tunaona nini? Mwisho wa sala mmoja wao anaenda nyumbani kwa Amani lakini mwingine sivyo. Sisi wote, tuna mwamini Mungu, tunapaswa tuwe makini na ujumbe huu sio tuu kujifunza kutolea sadaka yenye kibali machoni pa Mungu bali kuishi maisha ya Imani ambayo yatatuongoza katika kustahilishwa na sio kuja kusikitishwa siku ya mwisho.
Mafarisayo walikuwa ni watu ambao walijipa nidhamu na kujitoa kabisa katika dini yao. walikuwa ni waamini makini waliojitoa maisha yao kwa kusali kila mara na kushika neno la Mungu. Walitoa zaka za mapato yao yote sio tu kiasi kile walichotakiwa kutoa. Wakati Mfarisayo alivyosema katika mfano huu wa Yesu “mimi sio kama watu wengine: wanyanganyi, wadhalimu, wazinzi, wala sio kama huyu mtoza ushuru. Mimi ninafunga mara mbili kwa juma; hutoa zaka katika mapato yangu yote”. (Lk 18:11-12) hakuwa anatania. Ni wakristo wachache wanaweza kufikia kiwango hichi cha mafarisayo. Lakini walipungukiwa kitu.
Watoza ushuru, kwa upande mwingine, kwa ujumla walikuwa wakichukuliwa kama watu walio na maadili hafifu. Kwasababu Watoza ushuru walifanya kazi kwa ajili ya wapagani Wakirumi, walijichanganya nao, na mara nyingi kuchukua fedha zisizo halali kutoka kwao, na inasemekana walikuwa katika hali ya unajisi. Kama dini ya kipindi hicho ilivyokuwa, watoza ushuru walichukuliwa kama wadhambi wa wakubwa sana tena wahadharani walio njiani kuelekea motoni. Lakini Watoza ushuru walijua pia sauti ya wengi si mara zote ni sauti ya Mungu. Walitumainia ukombozi sio kutokana na faida ya dini yeyote au faida ya maadili yao flani bali katika neema ya huruma ya Mungu.
Kumwamini tu Mungu haimuokoi yeyote. Mt. Yakobo anatuambia hata shetani mwenyewe anamwamini Mungu na anatetemeka kwa hofu. (Yk 2:19). Mafarisayo katika Injili walimwamini Mungu kama Mungu aliye na ubaguzi, Mungu anaye wapenda watu wema tu na kuwachukia wabaya. Kwa hiyo mafarisayo kwa haraka walijua tu kuwapenda watu wema kama wao tu, na kuwaangalia wengine kama waovu na wadhambi kabisa kama watoza ushuru. Yesu anatoa mfano huu juu ya mafarisayo kwasababu “walijiamini wenyewe kwamba ni wenye haki na kuwachukulia wengine wadhambi” (mstari wa. 9). Mtoza ushuru kwa upande mwingine, hakujiaminisha mwenyewe, au kwa kitu kingine bali kwa huruma ya Mungu. Akisimama mbali, tena bila kujaribu kutazama mbinguni, anapiga kifua akiomba “Mungu, nionee huruma mimi mdhambi” huyu ndiye mtu aliyeenda nyumbani akiwa na Amani na Mungu na sio yule mfarisayo aliyejiwekea haki.
Sisi pia kama Mafarisayo na watoza ushuru tunakuja mbele ya Mungu kila wakati kumwabudu na kusali. Sisi pia tunategemea kurudi nyumbani tukiwa na Amani na Mungu. Tujifunze kutoka kwa Mtoza ushuru siri ya kumwabudu Mungu katika hali ya kukubaliwa naye. Katika hali ya unyofu na unyenyekevu, katika hali ya kuwaombea wenzetu sio kuorodhesha dhambi zao.
Kwanza kabisa, tunapaswa tusiwasikilize watu na hata nafsi zetu zinapotuambia Mungu ana hasira sana nasi, na kwamba hawezi kutusamehe. Pili, tunapaswa kukubali dhambi zetu na kujikabidhi na kuamini huruma ya Mungu ambayo ni kubwa kuliko dhambi yeyote tuliotenda. Na mwisho kabisa, tumuahidi Mungu tusije kuwaona wengine wadhambi na kuwahukumu bali tuwasaidie katika tamaa yao yakumtafuta Mungu, kama vile mtoza ushuru leo anavyotusaidia katika tamaa yetu yakumtafuta Mungu. Kumbuka, mara zote na nyakati zote, Mungu anawapinga wenye majivuno, lakini anawapa wanyenyekevu neema. Njia ya kwenda kwenye utakatifu wa kweli ni njia ya unyenyekevu. Ni vigumu kuwa mtakatifu bila unyenyekevu. Unyenyekevu una upendo ndani yake kama msingi wa fadhila zote za Kikristu. Watakatifu wote bila kumuacha yeyote walikuwa wanyenyekevu kabisa. Sala ya Mtoza ushuru ni sala ambayo watakatifu wengi waliisali kila mara na nyakati zote “Ee Mungu, unionee huruma mimi mdhambi”. Ndio maana watakatifu licha ya njia yao nzuri ya utakatifu ya maisha yao, bado walihudhuria sakramenti ya kitubio kila mara kama kiini cha maisha yao.
Katika Mwaka huu wa huruma ya Mungu na siku zote za maisha yetu, tujipatanishe na Mungu kila mara kwa sakramenti ya Kitubio bila kuwa na wasi wasi, tusiwe na wasi wasi juu ya huruma ya Mungu. Sakramenti ya kitubio inatusaidia kukuwa katika kiini cha unyenyekevu na katika mstari wa utakatifu. Tukifanya hivyo tutaweza kusema kama Paulo anavyosema katika somo la pili kwamba amevipiga vita vilivyo vizuri na mwendo ameumaliza. Paulo aliteseka mahakamani huko Rumi na hakuna aliye mtetea kwasababu wakristo waliogopa utawala wa Kirumi. Paulo alisali na alikuwa na matumaini kwa Mungu. Paulo tofauti kabisa na yule mfarisayo tuliemuona katika somo la Injili, anasali akiwaombea Wakristo wenzake waliojua kabisa amefungwa gerezani lakini hawakwenda kumtetea, yeye anawaombea kwa Mungu asiwahesabie hatia kwa jambo hilo. Paulo anatupa mfano wa pekee wakuwaombea ndugu zetu. Tusiwe wabinafsi hata katika kusali, tusiwaombee wenzetu mabaya bali tuwaombee mema ili kwa wema huo sisi nasi tutakuwa tumeiga tabia ya Kimungu ya kuwapenda watu wote. Daima tujione sisi wote ni wadhambi tunaohitaji neema ya Mungu. Na daima tutafute huruma yake kwa mioyo ya unyenyekevu wa kweli.
Sala:
Bwana Yesu, ulijinyenyekesha mwenyewe kwenye mti wa msalaba, tujaze neema ya unyenyekevu ili tuweze kukubalika na kuwa wema machoni pako.
Amina
Maoni
Ingia utoe maoni